http://www.fortunecity.com/victorian/abbey/313/ukweli.html
UKWELI NI HUU (KUUSUTA UWONGO) Aman Thani Fairooz Dibaji Kitabu
Hichi Ukweli Ni Huu (Kuusuta Uwongo) Utukufu Na Neema Ya Zanzibar
Zanzibar Na Ubaguzi Kabla Ya Mavamizi Ubaguzi Umeanzishwa Zanzibar
Wakati Wa Serikali Yenye Kujiita Ya "Mapinduzi" Elimu Na Matibabu
Bure! Taalimu Matibabu Hali Za Maisha Neema Zilikuwepo Kuanza
Harakati Za Siasa Sheikh Ali Muhsin Kwenda Nchi Za Ulaya Ikiwemo Na
Uingereza Kupigania Uchaguzi Wa "Common Roll" (Mtu Mmoja Kura
Moja). Kuasisiwa HizbulWattan (Zanzibar Nationalist Party) Wakoloni
Dhidi Ya Hizbu, Uhuru Na Umoja Wa Zanzibar Makao Makuu Ya Hizbu
Hizbu Kumleta Zanzibar Seyyid AbdulRahman (Babu) Natija Ya Safari
Ya Sheikh Ali Muhsin Wakoloni Na Nyerere Ndio Waasisi Wa
AfroShirazi Uchaguzi Wa Mwanzo Juni 1957 Kwanini Sheikh Ali Muhsin
Aliamua Kusimama N'gambo Badala Ya Majumba Ya Mawe? Kwenye Shari
Huzaliwa Kheri Kukuwa Kwa Harakati Za Siasa Ati Husemwa Kuwa Hizbu
Imefeli! Kugawanyika Kwa AfroShirazi Kuasisiwa Kwa Zanzibar And
Pemba Peoples' Party (ZPPP) Tume Ya Sir Hillary Blood Uchaguzi Wa
Pili, Januari 1961 Uchaguzi Wa Tatu Juni 1961 Ushirikiano Wa
ZNP/ZPPP Kutokufaulu Mazungumzo Ya Mwanzo Ya Katiba Ya Uhuru
AfroShirazi Iliandaa Machafuko Siku Ya Uchaguzi Muungano Wa
ZNP/ZPPP, Waunda Serikali Kutokufaulu Mazungumzo Ya Mwanzo Ya
Katiba Ya Uhuru Babu Kutoka Katika Hizbu Dhamiri Za Babu Kufungwa
Gerezani Kwa Seyyid AbdulRahman Babu Kutolewa Gerezani Babu Babu Na
Fisadi Yake Ya Mwisho Kipi Kilicho Mpelekea Babu Kuchukua Khatua
Kama Hizo Uchaguzi Wa Julai 1963 Nyerere Anasema Wakoloni
Walipendelea Kuiacha Serikali Ya Zanzibar Mikononi Mwa Hizbu
Mkutano Wa Katiba Ya Uhuru. Uhuru Wa Zanzibar Sherehe Za Uhuru
Yaitwayo "Mapinduzi" Kuuliwa Kwa Muhsin, Suleiman Na Ahmed 1
Kifo Cha Ali Mzee Mbalia "Skolashipu" Za Misri Yaliyo Nifika
Nafsi Yangu Na Hayo Yenye Kuitwa "Mapinduzi" Maafa Ya Gerezani
Kufungwa Kifungo Cha Miaka 10 Gerezani Kiasi Cha Kazi Alichokuwa
Akifanyishwa Mfungwa Maovu Waliyotendewa "Wafungwa Wa Kisiasa"
Kutolewa Gerezani Nakimbilia DarEsSalaam Mahabusi Wadhulumiwa Wa
Mwalimu Nyerere Mateso Ya "Kwa Ba Mkwe" Maisha Ya Gereza Langoni
Nyakati Za Kufanyishwa Kazi "Wafungwa Wa Sisasa" Ufungwa Wa Karume
Ni Zaidi Ya Utumwa Kurejeshewa Uhuru Wetu Kuuliwa Wananchi
Msikitini Kuuliwa Kwa Wananchi Wengine Namna Walivyo Uliwa Wafungwa
Waliyokufa Gerezani (1) Mzee Mohammed Mbaba (2) Maalim Harun Ustadh
(3) Idi Hassan (4) Ramadhan Ibrahim Saadalla Wameuliwa Vifungoni
Wafungwa Wengine Wauliwa "Wafungwa Wa Siasa" Bado Waendelea Kuuliwa
Aliyonizungumziya Twala Yalomfika Othman Shariff Kuteswa Na Kuuliwa
Othman Shariff Kufungwa Na Kuuliwa Saleh Saadalla Karume Kuanza
Kumbadilikia Twala Mwisho Wa Twala Makomred Wamechangia Maafa
Yaliopo Nchini Kwanini Mwalimu Nyerere Alikataa Kuwapeleka Zanzibar
Watuhumiwa Wa Kesi Ya Ukhaini? Siri Hii Ni Kubwa Sana!! Serikali Ya
Mavamizi Ya Zanzibar Bado Imo Na Ubaguzi Wake Nilitakiwa Nitoke
Nchini Namna Nilivyoondoka Kuukimbia Wattani Wangu Kuleta Ahli
Zangu Dubai Mengineyo Kwa Ufupi Mwalimu Na Uislamu Mwalimu Na
Utumwa Porojo La Mitaani Demokrasi Ya Vyama Vingi (MultiParty
Democracy) Vipi Kuifikilia Demokrasi Shukrani DIBAJI Namshukuru
Mwenye Enzi Mungu Mwenye Wingi wa Rehema Kubwa na Ndogo kuniwezesha
kuandika kijitabu hiki ambacho nimejaribu kiasi nilichoweza
kuyaeleza yale yaliyotokea katika Nchi yetu, Zanzibar. Na
yaliyonitokelea mimi mwenyewe na yaliyowatokelea Wananchi wenzangu
kutokana na hayo yenye kuitwa, "Mapinduzi" yaliyofanyika katika
Visiwa vyetu mnamo taarikh 12 Januari, 1964. Haya ninayoyaandika ni
kiasi ya hayo niyajuayo mimi tu; hapana shaka yapo mengi ambayo
sikupata kuyajuwa. Bali nataraji watatokea wenzangu nao,
wakayaeleza waliyotendewa au waliyoyaona yakitendwa. 2
Nafanya haya si kwa makusudio yoyote mengine zaidi ya kutaka
kueleza ukweli wa yaliyotendeka katika Nchi yetu ili Wananchi
wenzangu (na ndugu zetu wa Tanganyika, bali na ulimwengu, pia) na
khasa wale waliokuwa wadogo, na wale ambao hawajaja duniani wakati
huo waweze kuyafahamu japo kwa uchache yaliyotendeka katika Nchi
yao kwa hayo yenyekuitwa "Mapinduzi". Ikiwa katika kuyaelezea haya,
kutahitajia kumtaja mtu au watu kwa njia yoyote, itakuwa nafanya
hivyo kwa kutokana na maudhui ninayo izungumza wala si kwa ajili ya
kusengenya au kukejeli au kudharau au kwa kutia illa za namna
fulani, hashaa! Bali kwa vile dhamiri ya kukiandika kijitabu hiki
ni kuelezea ukweli wa mambo yalivyokuwa, basi sitochelea kulieleza
lolote madhali kwa kufanya hivyo ndio itakuwa natimiliza lengo
nililolikusudia, nalo ni kuueleza ukweli. Kutokana na hayo,
nachukuwa nafsi yangu masuliya yote yatayotokea katika maandishi
haya. Muhimu, nawaomba wasomaji wangu wajishughulishe zaidi na hayo
niliyokusudia kuyaeleza, kwani hayo hayana shaka yoyote, ni kweli
tupu. Na nawaomba wasijishughulishe na makosa madogo madogo, kama
vile ya upigaji chapa, makosa ya lugha au juu ya utaratibu wa
uwandishi. Ikiwa litatokea suala lolote, au ikiwa lolote
halitafahamika, basi wakurejelewa ni mimi. Inshallah, nitajaribu
kama nitavyoweza kutanzua kila lililotanzika na ikiwa nitashindwa,
basi sitoona taabu kutaka msamaha. Mwenye kukamilika kwa yote ni
Mwenye Enzi Mungu. Tunamuomba Mwenye Enzi Mungu ajaaliye haya
tunayoyaeleza yapate kusomwa, kuzingatiwa na kufahamika na
ipatikane faida ndani yake kwa kutumiwa kwa kheri. Kubwa ya kheri
hizo ni kusahihisha palipo haribika, kuiondosha haramu, kuomba toba
na kutenda mema, kwani mema huondowa mabaya. Mwenye Enzi Mungu
atupe taufiq, Amin. Aman Thani Fairooz P.O. Box 10836 Telephone
04850802 Dubai United Arab Emirates Januari, 1995
3
KITABU HICHI Kidogobasi, Chungutamu. Kwa hakika Kitabu hichi ni
kidogo basi. Lakini, kama alivyosema muandishi kuwa kaandika kwa
ufupi, bali ufupi wa kutosheleza faida yake. Yoyote atakaye kisoma
kitabu hichi kwa kutaka kufahamu na bila ya mawazo yake kudhibitiwa
na kupenda au kuchukiya, basi hapana shaka atapata faida. Atafahamu
jinsi wananchi wa Zanzibar walivyokuwa katika harakati zao za
kuwania uhuru wa nchi yao kutokana na ukoloni wa Muingereza.
Harakati ambazo zalianza kabla ya miaka ya 1940. Pia ataweza
kufahamu ni nani walioanzisha harakati hizo, namna zilivyopata
kuungwa mkono na wananchi na namna zilivyokuwa zikiendeleya. Pia
atapata kufahamu jinsi ya pingamizi zilivyokuwa. Atafahamu
pingamizi hizo zilivyoanzia, nani aliyezianzisha na kuzipalilia na
kuzikuza. Atafahamu natija yake! Pia atafahamu vipi wananchi chini
ya uwongozi wa vyama vyao ZNP/ZPPP walivyokuwa wakizikabili
pingamizi hizo. Na zaidi atafahamu juhudi za waongozi wa ZNP/ZPPP
katika kutaka mafahamiano na ushirikiano na wananchi wenziao ASP na
nini ulikuwa muelekeo wa waongozi wa ASP, muelekeo ambao mara
nyingi ulikuwa ukiathirika kwa uwongozi na fikra zilizokuwa
zikipangwa na kuletwa kutoka nje ya nchi. Chungutamu. Kweli ni
chungu! Lakini ni wajibu isemwe na kubainishwa. Uchungu uliyomo
ndani ya kitabu hichi ni kuona jinsi wananchi walivyohangaika kwa
jasho, mali na hata damu zao kwa kuwania uhuru wao kutokana na
ukoloni wa Muingereza, lakini kwa sababu ya husda, chuki na ufisadi
uhuru huo haukuachiwa kuishi zaidi ya siku thalathini! Isitoshe,
sio kuwa uhuru huo ulipotezwa kwa kutumiliwa njiya za usalama,
sivyo, bali kwa fujo! Fujo ambalo natija yake ni kupotezwa Dola ya
Zanzibar, roho za wananchi, heshima ya binaadamu, mali za watu na
mwisho kuwachwa wananchi kuishi ndani ya haramu. Utamu japo kwa
hakika sio utamu ni kwa vile kuweza wananchi kupata kuufahamu
UKWELI ambao kwa muda wa zaidi ya miaka thalathini umekuwa
ukifunikwa kwa UWONGO. Lakini, kama yalivyo maumbile, kweli daima
huibuka. Tunamshukuru Mwenye Enzi Mungu kwa kudhihiri kitabu hichi
na kuweza kuufahamisha umma, bali na ulimwengu, maafa
yaliofikishiwa Zanzibar, Nchi na Wananchi. Msomaji, na pengine hata
asimuliwaye haya, huenda akasema, yaaleiti yalielezwa haya kiasi
cha miaka ishirini liyopita, au kabla ya hapo. Hivyo ni kweli!
Lakini kila kitu kwa majaaliwa, na kuchelewa kwengine kuna kheri
zake kama kwengine kunavyo shari zake. Kheri katika kuchelewa
kudhihiri kitabu hichi ni kuwa vijana waliokuwa wadogo wakati wa
maafa ya Zanzibar leo ni watu wazima, wenye uwezo wa kufikiri,
kuamua na kutenda. Kwa hivyo wanahitajia kuujuwa Ukweli. Wao si kwa
ajili ya Kuusuta Uwongo, hashaa!! Bali ni kwa ajili ya kuujuwa
ukweli, kisha iwe ni mafunzo kutokana na yaliotendeka. Watasoma, na
Inshallah watayafahamu na kuyatumia. Na haya ndio khasa makusudio
na faida ya kitabu hichi. Kutumia kwao huko kwanza iwe ni kwa
kuepusha yasitendeke tena maafa yaliyotendwa, kufuatilia hilo au
yote mawili sambamba ni kwa kufanyakazi katika kujenga palipo
bomolewa. Kubomowa daima ni rahisi kuliko kujenga, kujenga kunataka
umoja na ushirikano wa kila mmoja wetu. Kwa hivyo ni waajibu wa
kila mmoja wetu kushirikiana, bega kwa bega, kwa nia na nguvu moja
kufanyakazi kuirejesha Zanzibar. Kwanza, kuirejesha katika ramani
ya ulimwengu ili iwe na jina na pahala pake kuwa ni Dola kaamili na
iliyo huru. Kisha, bali ndio la muhimu, kuirejesha katika neema
zake. Hichi ni kitabu cha kusomwa na kila Mzanzibari, bali na ndugu
zetu wa Tanganyika, pia. Abdulla Ali (Baba)
4
UKWELI NI HUU (KUUSUTA UWONGO) Nimelichagua jina hili la UKWELI
NI HUU KUUSUTA UWONGO, baada ya kuyasikia na kuyasoma me ngi ya
uwongo na hata yakafika kusomeshwa watoto wetu katika maskuli ya
Zanzibar kukhusu hayo yenye kuitwa "MAPINDUZI" yaliyofanyika katika
visiwa vyetu vya Zanzibar mnamo taarikh 12 Januari 1964. Kabla ya
kuingia katika hayo, ningependa ku waambia wasomaji wangu wote kuwa
mimi si mjuzi hata kidogo wa fani hii ya uandishi; tena ni mbovu
sana katika "spellings" na ka tika "nahau" za Kiswahili cha kisasa.
Pia nawaomba radhi kwa Kiswahili changu cha kizamani. Bali,
kutokana na huo uzushi na kupotezwa kwa makusudi ukweli wa hayo
yaliofanyika kukhusu hayo yenye kuitwa "mapinduzi" nimeona sina
budi illa ni kujitolea hivyo hivyo juu ya upungufu wangu katika
fani hii ya uandishi. Lakini ukweli lazima niudhihirishe ili
vichipukizi vyetu viweze kuyaelewa vilivyo yaliyotendeka katika
nchi yao. Kwani wengi walikuwa wadogo na wengine walikuwa hata
hawajazaliwa katika wakati huo. Ilivyokuwa Kiswahili ni lugha yangu
ya kuzaliwa, basi ninaiandika kama ninavyoisema. Si shughuliki na
"kua au kuwa, aliniambia au aliniambiya, ameuawa au ameuwawa kenda
au kaenda, amekwenda au ameenda". Hayo kwa wataalamu wa lugha ni
mambo muhimu lakini kwa mimi nakutakeni msamaha juu ya hayo. Muhimu
ya kuyaangaliya na kuyazingatiya ni yale nikusudiayo kuyaeleza,
kwani hayo ndio muhimu na ndio ya kweli tupu isiyokuwa na dosari
hata chembe. La mwanzo nitakalo kuombeni mlifahamu uzuri ni ile
hakika kuwa hayo yaliyofanyika katika visiwa vyetu taarikh 12
Januari 1964, hayakuwa "MAPINDUZI" wala hayafai hata kidogo kuitwa
'mapinduzi' kwa maana asili ya neno. Bali kwa maana zote yalikuwa
khasa ni "MAVAMIZI", yaani kwa Kiingereza "INVASION". Mapinduzi
lazima yapangwe, yaongozwe na yatekelezwe na wananchi wenyewe kwa
maslaha ya nchi na wananchi wake. Sasa tukiangalia hayo
yaliotendeka Zanzibar, yalipangwa, yaliongozwa na yalitekelezwa na
WAGENI kutoka nchi za nje za jirani zetu. (Ni wao wala si wananchi
ndio waliochukua ngawira kubwa kubwa). Haya yanathibitika zaidi kwa
vile kuwa huyo jamadari aliyeyaongoza hayo 'mavamizi' ni John
Okello na wa chini yake walikuwa Injini na Mfaranyaki. Nani kati ya
hao aliyekuwa kitovu chake kimezikwa visiwani? Okello amezaliwa na
amekulia kwao Uganda, Injini amezaliwa na amekuliya kwao Kenya na
Mfaranyaki amezaliwa na amekuliya kwao Tanganyika. Wote hao
walikuja Zanzibar wakiwa watu wazima na shughuli zao, wamekuja
kutafuta kibarua na kukimbia kodi za kichwa katika nchi zao.
Liangalie hilo waliloliita "Baraza la Mapinduzi". Utaona sehemu
kubwa ya wanachama wa Baraza hilo walikuwa si Wazanzibari, laa kwa
kuzaliwa wala kwa kuchukua Tajnisi (Kuandikisha Uraia). John
Okello, Khamis Darweshi, Seif Bakari, Said Natepe, Said Washoto,
Muhammed Mfaume, Edington Kisasi, Mohammed Abdalla Kaujore.
Ukiwaacha wengineo ambao nao vile vile walikuwa si wananchi wa
Zanzibar kwa kuzaliwa, bali wao walikuja Zanzibar wakiwa katika
migongo ya wazee wao na waliendelea kuishi humo visiwani kwa maisha
yao yote. Na wakachukuliwa kama ni Wazanzibari. UTUKUFU NA NEEMA YA
ZANZIBAR Mwenyezi Mungu amevipa visiwa hivi viwili yaani Unguja na
Pemba bahati ya utukufu kwa kila jambo lake. Hayo yaliendelea tokea
karne na karne mpaka pale ulipotendwa ufisadi wa taarikh 12 Januari
1964, ndipo neema na utukufu wa Zanzibar ulipoanza kutoweka. Hapo
tena, badala ya zumari kuwa likipulizwa Zanzibar, watu wa maziwani
(Bara) walikuwa wakihemkwa, ikawa linapulizwa Bara, tuliopo
visiwani tunahemkwa! ZANZIBAR NA UBAGUZI KABLA YA MAVAMIZI
Nathubutu kusema bila ya wasiwasi wowote kuwa Zanzibar hakukuwepo
ubaguzi wa namna yoyote kwa maana khasa na ya wazi ya neno UBAGUZI.
Kwanza Wazanzibari ni watu waliochanganya sana damu hata sio rahisi
kuweza kumtambua mtu kuwa ni mwenye kutokana na asili ya kabila
fulani kwa kuangalia rangi yake au pua yake au masikio yake au kimo
chake au kwa jina lake. Jee, watu hao watabaguana namna gani?
Malipo ya wafanyakazi serikalini yalikuwa hayakupangwa kiukabila.
Wala serikali haikuwa na sehemu maalumu katika maskuli wala katika
mahospitali kuwa zimetengwa kwa ajili ya watu wa makabila
fulani.
5
Katika nchi za jirani zetu, Tanganyika, Kenya na Uganda kote
huko kulikuwepo na ubaguzi uliyokuwa ukiongozwa na serikali za nchi
hizo. Malipo ya mishahara ya wafanyakazi yalikuwa yakilipwa
kutokana na makabila yao wala si kutokana na ujuzi wao wa kazi.
Kulikuwepo "African Scale, Asian Scale na European Scale".
Madaktari, Mainjinia, Waalimu na wowote nawawe wana elimu na ujuzi
na maarifa ya namna moja, yaani wote sawa sawa kwa elimu na ujuzi
wa kazi zao, lakini mishahara yao ilikuwa tafauti kutokana na
makabila yao. Waafrika ndio wenye kulipwa malipo ya chini kabisa
kuliko wote. Wazungu walikuwa ndio wenye kulipwa mishahara minono
(hata baadhi yao walikuwa hawana elimu yoyote isipokuwa huwo Uzungu
wao), waliowafuatia ni Waasia. Vyoo vya njiani (Public Toilets) na
sehemu za kungojelea usafiri wa reli navyo vile vile vilikuwa
vikitumika kwa ubaguzi wa kikabila. Waafrika waliekewa vyoo vyao na
sehemu zao za kungojelea usafiri. Wazungu walikuwa na sehemu zao na
Waasia walikuwa na sehemu zao, wote mbali mbali. Lilikuwa ni kosa
na kuvunja sheria ikiwa imetokea kwa yoyote kuingia katika sehemu
isiyo kuwa amekhusika nayo. Khasa Muafrika awe ameingia au amekaa
katika sehemu za Waasia au za Wazungu. Katika Tanganyika, Kenya na
Uganda kote huko kulikuwa na Kodi ya Kichwa. Kodi hiyo ilikuwa
ikilipwa na kila mtu aliyekwishafika balegh katika umri wake. Nayo
pia ikitekelezwa kwa njia za ubaguzi wa kikabila. Waasia na
Wazungu, wao hata ikiwa wamechelewa kulipa kodi zao, basi walikuwa
hawakamatwi majiani wala hawaendewi majumbani mwao kukamatwa.
Lakini, Waafrika walikuwa wakisakwa majiani na wakiendewa majumbani
mwao mnamo pinga pinga za usiku. Na wakikamatwa, basi walikuwa
wakifungwa kamba za viunoni au hufungwa ncha ya shati la huyu na la
huyu kisha walikuwa wakiongozwa mmoja nyuma ya mmoja na huku
wakipigwa mateke na kusukumwa mpaka wakifikishwa Bomani. Huko ikiwa
hawatokuwa na cha kulipa basi walikuwa wakihukumiwa na kufungwa.
Kutokana na hali kama hizo, ndipo wengi kati ya wananchi wa nchi
hizo, khasa kutoka Tanganyika walikimbia kutoka makwao na kuhamia
Zanzibar kwa sababu ya kufuata hali njema za kimaisha. Zanzibar
hakukuwepo kodi za kichwa wala ubaguzi wa vyooni wala malipo ya
mishahara wala wa namna yo yote. Ilikuwa njema atakae naaje.
UBAGUZI UMEANZISHWA ZANZIBAR WAKATI WA SERIKALI YENYE KUJIITA YA
"MAPINDUZI" Mara tu baada ya kufika hiyo serikali ya 'mavamizi'
katika Zanzibar ubaguzi wa ukabila ulianzishwa. Kila "mrangi rangi"
kama walivyokuwa wakiwaita wenyewe, yaani wenye asili za Kiarabu,
za Kihindi na za Kingazija walianza kutolewa makazini bila ya
kupewa hata haki zao za ufanyaji wa kazi. Mashamba, majumba na hata
mabiashara yao yalichukuliwa kwa nguvu na kupewa wageni ikiwa ni
tunzo la ukatili na maovu waliyowafanyia wananchi katika nchi yao.
Serikali ya 'mavamizi' ya Zanzibar ilitangaza rasmi kupitia vyombo
vya khabari vya serikali kukhusu ubaguzi katika Taalimu. Waafrika,
wakipasi au wasipasi bali idadi yao ya kuingia katika "Form One" ya
"secondary school" ilikuwa ni 77 katika mia (77%), Waarabu 16
katika asili mia (16%), Wahindi 6 katika mia (6%), na Wangazija
MMOJA katika mia! (1%). Si hayo tu, bali serikali ya 'mavamizi'
imetumia fedha za umma kwa ajili ya kujijengea hospitali yao wao tu
Wanachama wa Baraza la Mapinduzi na familia zao na wameita,
"Mapinduzi Wing". Vitanda, mabetishiti, foronya za mito, vyombo vya
kulia kama sahani, vikombe, visu na nyuma (forks) vyote viliagiziwa
kutoka Ulaya. Ilikuwa ikitokea Mheshimiwa kulazwa huko, basi na
mkewe alikuwa akihamia huko huko na kulala kitanda kimoja kama
kwamba wamo katika siku za fungati! Haya yakitendeka wakati
wananchi wanyonge hawana hata dawa mahospitalini! Huo ulikuwa ndio
usawa, sio ubaguzi! ELIMU NA MATIBABU BURE! Tunaambiwa na serikali
yenye kujiita ya 'mapinduzi' kuwa elimu na matibabu yameanza kuwa
bure kwa wananchi baada ya kupatikana kwa Serikali ya 'mapinduzi'!
Huu ni uwongo uliokuwa hauna hata kifuniko. Toka lini elimu na
matibabu yalikuwa kwa malipo katika Zanzibar? Tangu kuanzishwa kwa
skuli ya serikali na Sayyid Ali bin Hamoud na toka kuanzishwa kwa
matibabu katika mahospitali, kamwe hayajapata kuwa ya malipo. Toka
kwa kuangaliwa na madaktari mpaka kwa madawa, chakula, na mpaka
kulala kwa kutibiwa katika mahospitali kulikuwa bure. TAALIMU
Wananchi na wageni, kuanzia chumba cha kwanza yaani (standard one)
mpaka kufikia chumba cha nane (standard eight), masomo yalikuwa
bure kwa wote. Sio hivyo tu, kila mwanafunzi alikuwa na deski lake
peke yake la kukalia na kila mwanafunzi alikuwa akipewa madaftari
ya kuandikia bure, vitabu vya 6
kusomea bure, kalamu za kuandikia bure, vidawa vya wino na wino
wake bure hata blotting papers (la kukaushia wino) pia wakipewa
bure. Na kila Ijumaa wanafunzi walikuwa wakipewa sabuni za kufulia
bure. Skuli za mashamba, wanafunzi walikuwa wakipewa kifungua
kinywa kunde na uji kabla ya kuingia katika vyumba vya masomo,
bure. Kuanzia chumba cha tisa mpaka cha 12, na baada ya muda katika
miaka ya 1950 kuanzia chumba cha saba mpaka cha 12, wazee
walitakiwa wasaidie kitu kidogo katika masomo ya watoto wao. Malipo
hayo yalikuwa ya kitu kidogo sana na si kila mzee alikuwa akilipa
ada hizo. Wengi sana katika wazee walikuwa hawalipi hata senti
moja. Na hao waliokuwa wakilipa, wengi wao walikuwa wakilipa
kuanzia Shs. tano mpaka Shs. 20 kwa wingi kila baada ya miezi
mitatu au mine. Kabla ya mzee kuwa alipe au asilipe, kulikuwepo
taratibu maalumu zilizokuwa zikifanywa. Mzee wa mtoto alikuwa
akipelekewa "questionnaire" (karatasi) yenye masuala yaliyokhusu
mapato yake, kazi yake na idadi ya watu wake wa nyumbani. Kwa
kutaka kuhakikisha uwezo wa mzee huyo, basi akipelekewa waraka huo
kwanza Sheha wa mtaa kuhakikisha yale yalioandikwa na akisha Sheha
humpelekea Mudiri wake na Mudiri humpelekea D.C. wake. Baada ya
khatuwa hizi ndio tena hapo hutolewa uamuzi wa kulipa au wa
kutokulipa, na kama kulipa alipe kiwango gani. Kutokana na mipango
kama hiyo, zaidi ya 70 katika mia (70%) ya wazee watoto wao
walikuwa wakisoma bila ya kulipiwa kitu chochote na kiasi cha 20
katika mia (20%) walikuwa wakilipiwa kitu kidogo na kiasi cha 10
katika mia (10%) ndio waliyokuwa wakilipiwa idadi kamili ambayo
ilikuwa chini ya Shillingi 200, kwa mwaka mzima. Wengi waliokuwa
wakilipa kima hicho, walikuwa ni wazee wenye asili za Kihindi.
Wanaoitwa Waafrika na wanaoitwa Waarabu hayo yalikuwa si maji yao.
Muhimu katika hayo si kulipa au kuto kulipa, muhimu ni thamani
(quality) ya elimu iliyokuwa ikipatikana siku hizo, jee leo
inapatikana? Hilo ndilo suala muhimu la kujiuliza na kulizingatia.
Ikiwa hiyo isemwayo leo kuwa elimu bure, na imekuwa wanafunzi
hawana madeski ya kukalia, hawana vitabu vya kusomea, wala chochote
cha kusomea, bali zaidi hawana hata walimu wenye ujuzi wa
kusomesha; basi bure kama hiyo ni "bure ghali". Kwa hiyo bure, basi
watoto wetu leo wametokwa na vibyongo kwa kuinama wakati wa
kuandika. Wakirejea kutoka maskuli utadhania wanatoka kuchimba
makaburi kwa mavumbi yalivyo watapakaa kwa kusota chini. Elimu
bure! Wanafunzi wakipotezewa wakati wao wa masomo kwa kuchezeshwa
ngoma za sindimba na kuimbishwa majimbo ya kanisani ati huitwa,
"Kwaya". Kuanzia Disemba wanafunzi walikuwa wakianzishwa mazowezi
ya kucheza ngoma na kuimba hizo kwaya pamoja na magwaride kwa ajili
ya kujiweka tayari kwa sherehe za hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'
katika mwezi wa Januari. Wakimaliza tu, hawawahi hata kushusha
pumzi wanangojewa kwa sherehe za kuasisiwa kwa Chama cha
AfroShirazi, 2 2 (February 2). Wakimaliza tu, hawawahi hata kunywa
maji, wanazolewa tena kwa mazowezi ya sherehe za "Muungano" April
26. Hawawahi hata kukaa kitako, wanabebwa tena kwa mazowezi ya
Sikukuu ya Wafanyakazi "May Day". Hapo hupumua kidogo kisha
huzolewa tena kwa mazowezi ya kusherehekea, "Saba Saba", July 7.
Hawawahi hata kwenda chafya, hunyakuliwa tena kwa mazowezi ya
sherehe za "Elimu Bure"! Septemba. Wakimaliza hapo wanazolewa tena
kwa mazowezi ya sherehe za "Uhuru wa Tanganyika" Desemba.
Ukiangalia utaona kuwa mwaka mzima badala ya watoto wetu
kusomeshwa, walikuwa wakichezeshwa ngoma, kuchezeshwa magwaride na
kuimbishwa manyimbo ya kanisani. Bado ati husemwa ELIMU BURE, kweli
bure, lakini BURE KWA MJINGA! Kwa kweli kiwango cha elimu Zanzibar
kimeanguka kiasi kikubwa sana, kiasi cha kuitwa, "chini ya sufuri".
Imefika hadi leo kuwa mwanafunzi aliyemaliza hicho wanachokiita,
"kidato cha nne" (Form IV), ukimwambia aandike barua ya kuomba kazi
kwa lugha ya Kiingereza, anashindwa hata kujaribu kuandika na ikiwa
atajaribu, basi kichwa huwa miguu na miguu huwa kichwa. Hapo
yalipokuwepo masomo ya kweli na walimu wa kweli wenye kufunzwa
wakafunzika katika fani ya kusomesha, wanafunzi waliyomaliza chumba
cha nane ilikuwa wakiandika Kiingereza, utawavulia kofia. MATIBABU
Tukija katika matibabu, ndiko tutakako kukuta kumeporomoka vibaya
kabisa. Hospitali hazina madawa, hazina vifaa vya matibabu, hakuna
hata vitanda na mabetishiti ya kutosha. Wagonjwa wanatakiwa wakenda
kutaka matibabu, wachukue zana zao wenyewe tokea pamba, gauze,
vijembe vya kunyolea na 7
hata chupa za "Drips" pia wende nazo. Shuka za kutandika
vitandani, mito na foronya zake na nguo za kujifunikia wakati wa
kulala vyote hivyo lazima wendenavyo mwenyewe; kama si hivyo basi
hatapata matibabu. Ubavuni mwao wakitazama wanaiyona "Mapinduzi
Wing" bwana na bibi wanaingia na kutoka! Tokea miaka yalipoanzishwa
mahospitali ya serikali Zanzibar, matibabu yalikuwa bure kwa wote.
Kwa wananchi, kwa wageni na hata kwa wapita njia. Kuangaliwa na
daktari kulikuwa bure, dawa bure, ukilazwa kwa ajili ya matibabu,
bure. Na hospitali zilikuwa hospitali kweli kwa kila kitu. Madawa
ya kila maradhi yalikuwepo. Madaktari wenye ujuzi wa kazi zao,
waliosomeshwa wakakhitimu walikuwepo wa kutosha. Sivyo kama ilivyo
hivi sasa, wauguzaji (Staff Nurses) ndio madaktari, tena wa kufika
kuuchana na kuupasua mwili wa binadamu! Kwenye nchi yenye sheria,
pindi likitokea lolote, basi ushahidi wa watu kama hao, hauwezi
kukubalika katika mahakama za sheria, kuwa ni ushahidi wa
kidaktari. Lakini ndio kama ule msemo wa Kiswahili, "likikosekana
la mama, hata la punda hufaa". Ni kweli kulikuwepo katika hospitali
kuu ya serikali sehemu maalumu za kulala wagonjwa wa kulipa. Lakini
hayo yalikuwa kwa kupenda kwake mwenyewe huyo mgonjwa. Malipo
yenyewe yalikuwa kwa watu wenye kufanyakazi za serikali, walikuwa
wakilipa Shs. sita kwa siku, na waliyokuwa hawafanyi kazi za
serikali, walikuwa wakilipa Shs.12 kwa siku. Kwa hakika hakukuepo
tafauti kubwa baina ya huko kwa malipo na kwa bila ya malipo.
Tafauti ziliyokuwepo baina ya sehemu za kulala wagonjwa kwa malipo
na sehemu za bure ni za nyongeza tu, sio kwa ya lazima. Kwa
mahitajio ya kimatibabu kulikuwa hakuna tafauti hata kidogo.
Tafauti zenyewe zilikuwa kama hizi: Katika upande wa malipo,
wagonjwa walikuwa wakipewa panjama za kulalia, vyakula vyao
wakiletewa katika sinia na sahani zao zilikuwa za kaure na walikuwa
wakipewa chai ya kitandani (bedtea) na pia walikuwa wakipewa chai
ya alaasiri (afternoon tea). Pia walikuwa wakipewa taula ya
kujifutia maji baada ya kukoga. Chakula kikubwa kilikuwa wali na
mchuzi wa nyama na kibakuli cha puding. Upande wa wagonjwa wa bure,
wao walikuwa wakiletewa vyakula vyao bila ya kutiliwa katika sinia
na sahani zao zilikuwa za senti (aluminium), chai walikuwa
wakitiliwa katika makopo ya senti. Hapakuwa na tafauti kubwa ya
chakula isipokuwa wao badala ya kupewa chai ya kitandani, wakipewa
uji. Wagonjwa wote wa kulipa na wa bure walikuwa wakipewa matunda
na mboga. Na ikiwa mgonjwa ameandikiwa na daktari chakula maalumu
kutokana na maradhi yake, basi alikuwa akipewa chakula hicho (bila
ya malipo) sawa sawa na mgonjwa aliyekuwa katika sehemu za malipo
ikiwa maradhi yao ni ya namna moja. Madaktari na wauguzaji walikuwa
ndio hao hao na matibabu yalikuwa ndio hayo hayo kwa wote, wa
kulipa na wa bure. Leo tuambiwayo kuwa matibabu bure, mgonjwa
akenda hospitali baada ya kuangaliwa na daktari (pengine na
muuguzaji "nurse" tu) na akaandikiwa dawa, akifika kwa watoa dawa
jawabu analolipata ni kuwa, "dawa hizi hazipo. Kanunue nje"! Jawabu
kama hizo ni za kila siku. Ukenda kuwaangalia wagonjwa waliolazwa,
ukianza tu kupanda ngazi, unakaribishwa na harufu za mikojo na za
mashonde kutoka vyooni. Hospitali haina maji ya kutosha. Ukiingia
katika vyumba vya kulala wagonjwa, unawakuta mapaka wanacheza
foliti kwa jinsi ya uchafu uliomo ndani. Makunguru wanaruka huku na
huku humo vyumbani, wanapitia dirisha hili na kutokea jengine.
Sakafu zinanata kwa uchafu. Sasa watizame hao wagonjwa namna
walivyo lala humo vitandani. Vichekesho khasa. Wengine wamejifunika
kanga za kisutu, wengine za mkeka, wengine za visima, na za namna
mbali mbali. Utadhania watoto wa kizamani walipokuwa wakitiwa
kumbini (kutahiriwa) Mabetishiti yaliyotandikwa vitandani kwa
ilivyokuwa kila mmoja amekuja na lake, basi, huyu katandika jeupe
la mfuto, huyu lililofumwa tausi na huku limeandikwa KARIBU MGENI,
na kwa kipembeni ya chumba utaona mengine yameandikwa FURAHA YA
BIHARUSI, na jengine limeandikwa kwa maandishi ya nakshi SINA
MWENGINEWE, au MAPENZI YETU YA UTOTONI, au MIMI NA WEWE HATULISHANI
YAMINI, mradi huwa rangi rangire. Hospital zimepoteza jina na
thamani yake kwa kila upande, haziwezi hata kidogo kutowa huduma
zitarajiwazo. Hiyo ndio hali ya hayo yanayoambiwa matibabu ya bure!
Lakini haya yote yanaowapata ni wananchi wa kawaida tu. Ama wenyewe
wakina fulani na fulani pamoja na watoto wao, wao bukheri wa sururu
hata hawana khabari nayo wala hawayasikii licha kuyaona. Khalafu
kwa kuudanganya umma ati husema, "Tumeondoa serikali ya kisultani
na kibwanyenye!". Wakati wa huo Usultan, Mfalme wa nchi hajapata
kuwa na hospitali yake peke yake. Yeye pamoja na ukoo wake wakenda
katika hospitali hiyo hiyo wanayokwenda watu wa kawaida. Aliyekuwa
Mfalme wa nchi, Seyyid Abdulla Bin Khalifa Bin Haroub, 8
alipopata maradhi, alilala katika hospitali hiyo hiyo na
alifanyiwa operesheni katika hospitali hiyo hiyo wanayotibiwa watu
wa kawaida. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sehemu yao ya kutibiwa
waliita "European Wing". Kutokana na makelele ya wananchi, khasa
kutokana na makala yaliyokuwa yakiandikwa katika gazeti la wananchi
la "Mwongozi", sehemu hiyo ilibadilishwa jina na badala ya kuitwa
"European Wing", ikaitwa "West Wing". Kutokea wakati huo ilikuwa
wazi kwa yoyote mwenye kupenda kwenda katika sehemu hiyo ikiwa
yutayari kulipa ada zilizowekwa. Leo baada ya mapinduzi ya kuleta
usawa na kuondoa usultani na ubwanyenye, mheshimiwa akiumwa na
mdudu upande basi mbio anachukua ndege anakwenda zake Uingereza au
Ujarumani kwa matibabu. Ikiwa matibabu yapo nchini bure, mbona wao
wanayakimbia na kuyafuatia ya malipo, tena katika nchi za n'gambu
na kwa kutumia pesa za wanyonge kwa matibabu yao? Sasa ipi
inayostahiki kuitwa serikali ya kibwanyenye? Hii ya waheshimiwa
waliyojitenga mbali na umma au ile ya waliyokuwa wakiishi pamoja na
umma? Mwenye macho haambiwi tizama! Unaweza kuwadanganya baadhi ya
watu baadhi ya siku, lakini huwezi kuwadanganya watu wote siku
zote. HALI ZA MAISHA Matunda makubwa waliyopata wananchi wa
visiwani wa Unguja na Pemba kutokana na hayo yenyekuitwa,
'mapinduzi', ni shida za kimaisha katika kila upande. Vyakula
havinunuliki, nguo hazikamatiki. Mradi wananchi wamo katika
kuhiliki kwa maisha yalivyo magumu. Vijana wamekuwa wazee kwa
shida. Sokoni kunaitwa, "Uwanja wa Mapambano". Na kweli, ukenda
sokoni basi upanie kweli kweli kwani fungu la mihogo sita ikiwa
huna Shs.200, hulichukui. Mkungu wa ndizi ya mtwike, Shs.3000, nazi
moja Shs.50, pilipili za mchuzi fungu Shs.30 mpaka 50, kicha cha
mboga ya mchicha kuanzia Shs.70 mpaka kuteremka Shs.50. Fungu la
machungwa sita yaliyotukuka kidogo, Shs.200 na yaliyokuwa madogo,
Shs.100. Takriban watu wote wamekuwa Mabaniani, hawali nyama kwani
kilo ya nyama ni Shs.1200! Mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya
kiwango cha chini ambao ndio wengi, ni Shs.7000! Mtu, yeye na mkewe
na watoto wawili, inambidi, tena kwa kujibana, atumie Shs.1000 kwa
siku kwa chakula cha asubuhi na cha mchana. Kwa hivyo inamlazimu
apate Shs.30,000 kwa mwezi. Ikishakuwa mshahara wake ni Shs.7000
kwa mwezi, hizo 23,000, atazipata wapi? Kutokana na hali kama hizo
za kimaisha, ndio utaona kuwa toka waongozi wa serikali mpaka
wafanyajikazi wa chini wanaishi kwa magendo. "Corruption" (rushwa)
katika nchi imefika katika kilele cha juu kabisa. Tunakubali kuwa
ulimwengu wote umeingiwa na shida za kimaisha lakini huwepo sababu
maalumu ambazo kwa Zanzibar Alhamdulillahi hazijatokea na Inshallah
zisitokee. Mara nyingi watu hukutwa na shida za kimaisha katika
nchi zao kwa kutokana na hali za mabadiliko kama kutokupata mvua,
kutokea mifuriko ya maji, kutokea moto wa misituni, kutokea
mitetemeko ya ardhi au vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kama nilivyo
tangulia kusema shida kama hizo, Alhamdulilah hazikufika katika
nchi yetu. Sasa kipi kilicho sababisha taabu na dhiki zote hizi za
kimaisha? Hili ni suala ambalo kila mwananchi lazima ajiulize,
ikiwa tutajiuliza kwa insafu basi jawabu halitokuwa zito kulipata.
Mpaka Januari 11, 1964, pishi moja ya mchele ilikuwa baina ya Shs.
nne mpaka tano. (Pishi moja ni sawa na kilo tatu). Ina maana ya
kuwa kilo tatu za mchele zilikuwa Shs. nne mpaka tano. Na
zilikuwepo kabila mbali mbali za mchele yaani namna kwa namna.
Neema zote zilizokuwepo Visiwani Zanzibar, Mwenyezi Mungu
ameziondosha kwa kutokana na maovu yaliyoletwa na hayo yenye kuitwa
"Mapinduzi". Ni kama wale watu waliyo mchinja bata aliyekuwa
akitaga mayai ya dhahabu. Dhulma zilizofanywa za kupoteza roho za
viumbe wa Mwenyezi Mungu, bila ya kuwa na kosa lolote la kisheria,
mali za watu zimechukuliwa kwa nguvu kutokana na wenye haki nazo.
Natija ya hayo imekuwa leo sehemu kubwa sana ya vyakula vinavyouzwa
masokoni vinatokana na ardhi zilizoporwa. Kwa hivyo, wananchi
wanalishwa vyakula vya haramu. Na wale waliokuwa wamenunua majumba
ambayo wanajua ni yenye kutokana na kuibiwa kutoka kwa wenye haki
nayo, basi wajue kuwa Sala zao wanazo zisali katika majumba hayo,
Mwenyezi Mungu hazikubali. Na ni hivyo hivyo, kwa wale walionunua
mashamba yaliyoporwa kutokana na wenye haki nayo, basi na wao wajue
kuwa vyakula wanavyo vivuna katika mashamba hayo ni vyakula vya
haramu. Kwa hivyo, wao wanakula haramu na wakiviuza, wao, ndio
watao chukua dhima ya kuwalisha wenziwao vyakula vya haramu.
Kutokana na 9
hali kama hizo zilizokuwa zimefanyika katika nchi, ndio ikawa
kila lifanywalo haliwi. Na ikiwa hapatofanywa TOBA ya kweli, basi
nawaje wowote wataokuja, ikiwa wataendelea na mwendo wa kurithi
mwendo wa kidhalimu waliyoukuta, basi hapana litalo weza kutengenea
ila itakuwa kuziba kiraka hapa na kupasuka pengine. Kauli ya
Mwenyezi Mungu kattu haiwezi kwenda kombo. Mwenyezi Mungu Anasema
kuwa: "Hazidi mwenye kudhulumu illa khasara". NEEMA ZILIKUWEPO
Katika huo wakati unaoitwa wa kikoloni, Serikali ya Zanzibar
ilikuwa ikiendesha mambo yake yote kama kujenga maskuli,
mahospitali, mabarabara, kununua meli za usafiri, pamoja na
kuyahudumia na kulipa mishahara ya wafanyakazi tokea wa kigeni
mpaka wananchi. Na hao wafanyakazi wa kigeni ambao wengi wao
walikuwa Wazungu, basi juu ya mishahara yao walikuwa wakipewa posho
maalumu (Inducement Allowances), pia walikuwa wakilipiwa nauli za
kuwaleta na kuwarejesha na za wakati wa likizo zao. Yote hayo na
mengineyo yakifanywa kutokana na mapato ya ushuru tu wa forodha.
Serikali hii yenye kujiita ya "Mapinduzi", ni wao peke yao ndio
wenye kununua bidhaa muhimu zote za nchi kama vile, karafuu, mbata
na pilipili hoho kutoka kwa wananchi kwa bei wazitakazo wao wenyewe
na wakaziuza kwa bei ziliopo katika masoko ya ulimwengu. Isitoshe,
serikali hii haina gharama za kuwalipa hao Wazungu kama ilivyokuwa
hapo zamani, sasa ilikuwaje hata ifike serikali kuwa haina fedha
hata za kuwalipa mishahara wafanyakazi wake wa kienyeji? Hapana
shaka sababu kubwa ya hayo ni hii dhulma iendeleayo hadi hii leo,
uwendeshaji mpotofu, ukiongozwa na siasa ya husda na uroho wa
madaraka na kipato, siasa ya "Chukuwa Chako Mapema"! (CCM). Siasa
ambayo immefanya mwananchi kuwa hana uwezo wala itibari yoyote
katika nchi yake. Kwa hali za kimaisha nchini mwananchi hawezi
kukaa akatua na kufikiri na kupanga juu ya maendeleo ya nchi yake,
yeye anafikiri juu ya cha jiyo tu! Siasa mbovu hii iliopangwa
makusudi imemzuiliya na kumnyima mwananchi uwezo na njia za
kujiendeleza, laa si katika kimaisha, walaa si katika kiutamaduni
au kielimu. Inatilia nguvu mizizi ya siasa yake ile ile ilioanziwa,
nayo ni "Mwenye Elimu ni Aduwi" KUANZA HARAKATI ZA SIASA Kabla ya
Serikali ya Kiingereza kuiingiza Zanzibar chini ya Himaya yake,
Zanzibar ilikuwa ni Dola kamili iliyokuwa ina shughuli zake
(ikiamiliana) na ulimwengu wote. Mara tu Muingereza alipoitia
Zanzibar katika makucha yake mnano mwaka 1890, kila jambo kubwa na
dogo lilikuwa lazima liamuliwe kutoka Uingereza. Mfalme wa nchi
alifanywa kuwa ni alama tu ya Dola, hakuwa na uwezo katika kukata
shauri juu ya uwendeshaji wa nchi. Kama ilivyo kawaida ya wakoloni
popote ulimwenguni wanapotawala, lazima watumie mbinu za kuwagawa
wananchi (ili waendeleze utawala wao) kutokana na hali za namna
fulani ziliopo katika nchi. Ikiwa kwa njia za kidini, ukabila,
urangi, utajiri, uwezo wa kimaisha na hata umadhehebu. Katika
Zanzibar Muingereza alitumia njia za kuwagawa wananchi kwa kutumia
asili za makabila yao. Aliwafanya wenye asili za Kiarabu wajione
kuwa wao tu ndio wenye haki za utawala kwa vile ilivyokuwa Mfalme
wa nchi anatokana na asili zao. Aliwafanya Washirazi yaani,
Wahadimu, Watumbatu na Wapemba wajione kuwa wao tu ndio wenye kila
haki za nchi kwa vile ilivyokuwa wao ndio waliyokwenda kuwaita
Waarabu (kutoka kwao Oman) kuja kuwasaidia kumuondoa Mreno.
Aliwafanya Waafrika (weusi) wajione kuwa wao tu ndio wenye
kusitahiki utawala wa Zanzibar kwa vile Zanzibar imo katika Bara la
Afrika. Na alichukua uchumi wote wa nchi na kuuweka katika mikono
ya wenye asili za Kihindi kuwa wao ndio raia wa Kiingereza sahihi
wa tangu asli, kwa uwezo wao wa kimaisha wakajiona kuwa wao ni
wabora kuliko wengine katika nchi. Kutokana na hali kama hizo,
wananchi walianza kujigawa mafungu kwa mafungu na walianza kufungua
Jumuiya zao za Kikabila. Waarabu walifungua yao, Washirazi
walifungua yao, Waafrika walifungua yao na Wahindi walifungua yao
na Wangazija wakafungua yao. Na ndani ya hizo hizo, zilijitokeza
zengine na kila moja ilikuwa ikijitapa kwa upande wake. Kwa muda
mkubwa jumuiya hizo zilikuwepo katika nchi na hazikuweza kupata
wala kufanya lolote kwa maslahi ya nchi. Kubwa walilokuwa
wakilipata ni kualikwa chai ya alaasiri kwenye Bustani ya Jumba la
Balozi wa Kiingereza, na kualikwa katika siku ya kuzaliwa Mfalme wa
Kiingereza na Mfalme wa nchi na kualikwa kutembelea manuwari za
Kiingereza zinapofanya ziara kuitembelea Zanzibar. Katika miaka ya
10
1920 Muingereza katika njama zake za kuzidi kuwafarikisha
wananchi ili aendelee kuwatumia katika kuendeleza utawala wake,
alianzisha kuwateuwa (appoint) wananchi kwa kuwatia katika Baraza
la Kutunga Sheria (Legislative Council) kwa njia za kikabila.
Aliwateua hatimaye Waarabu wane, Waafrika wane, Wahindi watatu na
Mzungu mmoja. Na upande wa Serikali walikuwemo wakurugenzi wa idara
wa Kiingereza kutoka idara mbali mbali za serikali walioteuliwa
vile vile, hao walizidi kwa wingi katika baraza hilo kuliko raia.
Mwendo huo uliendelezwa kwa muda wa miaka 28 na hapakuweza
kupatikana lolote la maslaha ya nchi. Miaka nenda miaka rudi, nchi
haikuwa na maendeleo yoyote kukhusu mabadiliko ya Katiba itayo
wawezesha wananchi kuendesha wenyewe shughuli za nchi yao bila ya
kuingiliwa na yoyote. Katika mwaka 1953 na 1954, Jumuiya ya Waarabu
(Arab Association) iliamua kumpelekea Balozi wa Kiingereza madai ya
kutaka yaletwe mabadiliko ya Katiba yatayo wawezesha wananchi wa
Zanzibar kuchagua wajumbe wao wa kuwapeleka katika Baraza la
Kutunga Sheria kwa njia ya uchaguzi wa Kura Moja Kwa Mtu Mmoja (One
Man One Vote). Na miongoni mwa madai yao, walidai uondolewe mtindo
wa kuwateua wananchi kwa njia za kikabila katika kila jambo la
nchi. Pia walitaka baada ya kupatikana kwa matokeo ya uchaguzi huo,
paanzishwe mazungumzo ya taratibu za kupatikana kwa Uhuru kamili wa
Zanzibar. Balozi wa Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar
wakati huo akiitwa Mr. Renkin. Balozi huyo alikataa hata kuyatia
maanani madai hayo. Jumuiya ya Waarabu walipoona hawakuweza kupata
natija yoyote katika madai yao, bali hata hayakuzingatiwa, waliamua
kuanzisha mgomo kwa kuwazuia wajumbe wao kushiriki katika vikao vya
Baraza la Kutunga Sheria na katika vikao vya Kamati za Mabaraza
yote waliyoteuliwa kushiriki. Mgomo huo ulichukua muda wa miezi 18
bara bara. Jambo la kulizingatia katika suala hili ni kuwa, madai
hayo kutokana na Jumuiya ya Waarabu hawakuyafanya kwa maslahi yao
binafsi zao, bali kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari wote bila
ya kujali asili za makabila yao. Haya yanajithibisha zaidi kwa vile
ukiangaliya idadi ya hao waliyokuwa wakiitwa (au wanaoitwa) Waarabu
katika Zanzibar, walikuwa ni kiasi cha 16 katika 100 (16%). Juu ya
hivyo waliamua kuziachilia mbali nyadhifa walizopewa, sio hivyo tu,
bali kutoa muhanga nafsi zao wakiweka mbele maslahi ya nchi. Bahati
mbaya hawakupata kuungwa mkono na wananchi wenziwao wenye asili za
makabila mengine juu yakuwa walizungumza nao na waliwataka
washirikiane katika madai hayo. Mmoja kati yao (alioteuliwa
kushiriki katika Baraza la Kutunga Sheria akiwa ni mwenye asili ya
Kiarabu), alipinga uamuzi wa Jumuiya yake na alihudhuria katika
kikao cha Baraza la Kutunga Sheria wakati wenzake walipokuwa
wamesha amua kugomea. Matokeo yake, alitokea mwananchi mwenye
uchungu na nchi yake na kumpiga bwana huyu kwa visu. Kwa bahati
mbaya alikufa kutokana na pigo hilo. SHEIKH ALI MUHSIN KWENDA NCHI
ZA ULAYA IKIWEMO NA UINGEREZA KUPIGANIA UCHAGUZI WA "COMMON ROLL"
(MTU MMOJA KURA MOJA). Wakati Jumuiya ya Waarabu ilipokuwa katika
hekaheka za mgomo wao wa kuto kushiriki katika Mabaraza yote ya
Serikali kwa madai ya kutaka papatikane mabadiliko ya Katiba yatayo
wawezesha wananchi kuchagua wawakilishi wao wa Baraza la Kutunga
Sheria kwa njia ya uchaguzi wa "One Man One Vote" na kusita
kuteuliwa kutokana na asili ya makabila yao, mwananchi mwenzao
mwenye uchungu wa nchi yake alifunga safari (kwa gharama zake
mwenyewe) kwenda kupigania maslahi ya nchi yake, akiendeleza madai
ya wananchi wenziwe huko nyumbani. Wakati Sheikh Ali Muhsin
alipokuwa katika hekaheka hizo huko Uingereza, alikutana na Seyyid
AbdulRahman Mohammed (Babu) na waliweza kushirikiana katika juhudi
hizo. Katika harakati hizo Sheikh Ali alikutana na waongozi mbali
mbali wa kisiasa na wengi wao walimshajiisha juu ya kuendelea na
juhudi za ugombozi wa nchi yake na walimpa kila msaada (moral
support). Huko Uingereza alipata kuzungumza na wakuu wa Serikali ya
Kiingereza, wakuu wa upande wa Upinzani na wakuu wa Vyama vya
Wafanyakazi. Pia alikutana na wakuu wa vyama na jumuiya mbali mbali
zenye kupigania kuondoka kwa ukoloni katika Afrika na katika sehemu
zengine za ulimwengu. KUASISIWA HIZBULWATTAN (ZANZIBAR NATIONALIST
PARTY) Wakati Sheikh Ali Muhsin akiwemo katika safari zake huko
nchi za Ulaya, huko nyumbani walichomoza wananchi wengine waliokuwa
nao na ghera na mapenzi ya nchi yao. (wote, isipokuwa mmoja tu kati
11
yao Sheikh Abdalla Mahmoud walikuwa si Waarabu) Wananchi hao
walikutana kuzingatia na kutafakari juu ya kupotea kwa nchi yao
kutokana na mbinu za mkoloni za kuwagawa wananchi kwa kutumia asili
za makabila yao. Wananchi hao waliibuka na amuo la kuanzisha Umoja
wa Wananchi wa Unguja na Pemba. Umoja ambao kila raia wa Zanzibar
atastahiki kuwemo bila ya kujali asili ya kabila yake wala Imani ya
Dini yake, la umuhimu ni URAIA wake. Hichi kilikuwa ndio chama cha
kwanza na pekee katika nchi kuasisiwa kwa kufuatia misingi ya
Uwananchi. Wananchi waasisi hao walikuwa ni, Sheikh Vuai Kiteweo,
Sheikh Miraj Shaalab, Maalim Zaid Mbarouk, Maalim Maksud Fikirini,
Maalim Mwandoa Khamis, Maalim Wazir Ali bin Maalim, Sheikh Haji
Hussain Ahmed, Sheikh Othman Soud, Sheikh Abdulla Mahmoud Kombo (wa
Makunduchi), Sheikh Ramadhan Tosir (Ramadhan Madafu), Maalim Hija
(wa Ndijani), Sheikh Ame, Sheikh Abdulla Mali, Sheikh Haji Kombo
(wa Kiboje), Sheikh Abdalla Mahmoud na wenziwe wachache. Kwahivyo
wale wenye kusema na kutangaza kuwa Hizbu (ZNP) iliasisiwa na
Waarabu au kilikuwa chama cha Waarabu, hapana shaka wanakosea, amma
kwa kutokujuwa ukweli ulivyo au wanasema hivyo kwa makusudio ya
kutafuta maslaha yao. Ukweli na hakika ilivyo ni kuwa Hizbu
haikuasisiwa na Waarabu wala hakijapata kuwa Chama cha Waarabu. Na
kama Hizbu kingelikuwa ni Chama cha Waarabu, basi kisingeweza
kupata ushindi katika chaguzi zilizofanyika za (One Man One Vote)
kwani idadi ya hao wenyekuitwa Waarabu nchini ilikuwa ndogo;
kwahivyo idadi yao hiyo haingaliwezesha kukipa (hicho kisemwacho ni
chama chao) voti za ushindi. Madai hayo ni miongoni mwa maneno na
mbinu za kufitinisha na kuwagawa wananchi kwa kuuwogopa umoja wao.
Hapana shaka zimetungwa na wakoloni na kuimbwa na vibaraka vyao,
kwa maslahi yao. Mabwana hao tuliowataja hapo juu wakiwa ndio
waasisi wa Chama cha HizbulWattan, wao ndio waliyomuendea Sheikh
Ali Muhsin nyumbani kwake baada ya kurejea kutoka safarini na
kumueleza kukhusu kuasisi kwa chama chao na nini dhamiri zilizo
wapelekea kuasisi chama hicho. Baada ya kumueleza, walimtaka na
yeye awaunge mkono kwa kujiunga katika chama. Sheikh Ali Muhsin
alipoona kuwa hayo wayatakayo wananchi wenzake ndio hayo hayo
ayatakayo na kuyapigia mbio daima basi, hapo hapo aliamua kujiunga
na kushirikiana nao. Baada yakujiunga, waasisi hao walimtaka Sheikh
Ali Muhsin aanze kuzungumza na nduguze wenye asili za Kiarabu bali
na kila anaefahamiana nae ili wajiunge na wananchi wenziwao. Sheikh
Ali aliupokea na kuanza kuutekeleza ujumbe huo. Miongoni mwa wa
mwanzo (kati ya hao wenye kuitwa Waarabu) kujiunga na Umoja huo ni,
Sheikh Badr Muhammed Barwani, Sheikh Ahmed Seif Kharusi, Sheikh
Amour Zahor Ismaily, Sheikh Ali Ahmed Riyamy Sheikh Nassor bin Isa
Ismaily na Sheikh Ahmed Khalfan Naamani haikuchukuwa muda ila nao
walijiunga. WAKOLONI DHIDI YA HIZBU, UHURU NA UMOJA WA ZANZIBAR
Serikali ya kikoloni ilipoona Umoja wa Hizbu umesimama na kila siku
unazidi kuungwa mkono na wananchi wa kila pembe na kila aina,
walizidi kuogopea maslahi yao. Kwa kuhifadhi maslahi yao walianza
kuuandama Umoja huo HizbulWattan nje ndani, usiku na mchana kwa
kuwatumilia baadhi ya wananchi wafanyakazi wa Idara ya Utawala
khasa Mamudiri na Masheha. Vitumishi hivyo vilifunga njuga na
kuingia mitaani na viamboni katika juhudi za kuuvunja Umoja huo wa
HizbulWattan. Kwa kiasi fulani hapo mwanzoni waliweza kufanikiwa,
kwani walitumilia mbinu za kuwatisha wananchi; baadhi kwa kuwaambia
kuwa, chama hiki azma zake ni kuleta michafuko katika nchi na kwa
baadhi ya wananchi wakiwaambia kuwa chama hiki kinataka kumuondoa
Mfalme. Kila mmoja wakimpigia mdundo waliofikiria kuwa utaweza
kumshitusha na kukiepuka chama hiki. Bali wananchi hawakuchukuwa
muda illa waliweza kuzielewa mbinu zao hizo na kuwaepuka na badala
yake kuzidi kuungana na wananchi wenziwao. MAKAO MAKUU YA HIZBU
Kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa "Common Roll Election, yaani, "Mtu
Mmoja Kura Moja", katika Zanzibar mnamo mwaka 1957, mwananchi,
mzalendo Sheikh Mahmoud wa Mtendeni aliyekuwa mwishoni
akijishughulisha na utengezaji wa saa, alijitolea kwa kukipa Chama
jumba lake la ghorofa moja lililokuwepo mtaa wa Mwembetanga kuwa ni
Makao Makuu ya Chama. Alilitoa jumba hilo bila ya kupokea kodi hata
senti moja. Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwanzo wa 1957,
Hizbu iliyaondoa Makao Makuu yake kutoka Mwembetanga na kuhamia
Mkunazini karibu na Msikiti Gofu. Baada ya kuwepo hapo kwa muda,
ndio iliweza kununua jumba lake wenyewe katika mtaa wa Darajani
12
na kulifanya ndio Makao Makuu ya Chama. Jumba hilo, baada ya
'Mavamizi' ya Januari 12, 1964, liliporwa na Serikali ya 'Mavamizi'
na kufanywa Makao Makuu ya AfroShirazi Youth League. Kama ilivyo
hali ya majengo mengi mengineo humo nchini, jumba hilo limetupwa
bila ya matengenezo wala matumizi ya faida. Na linaachwa kubomka
pole pole. Haya sio ajabu, bali haya yanazidi kuthibitisha jinsi
hao viongozi wa Zanzibar walivyokuwa hawana uchungu na Nchi bali na
chochote cha nchi. HIZBU KUMLETA ZANZIBAR SEYYID ABDULRAHMAN (BABU)
Miezi michache kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa 1957, Chama cha
HizbulWattan kilimleta Babu Zanzibar ili ashirikiane na wananchi
wenziwe katika harakati za kisiasa. Baada ya kufika Zanzibar, Hizbu
ilimteuwa kuwa Katibu Mtendaji wa Chama (Excutive Secretary).
Kutokana na maarifa aliyokuwa nayo katika mipango ya kuendesha
chama cha kisiasa, Babu baada ya muda mdogo alianzisha Umoja wa
Vijana (Youth Own Union) (YOU). Kwa msaada na ushirikiano wa
waongozi wenziwe na wananchi Babu alifanya kazi kubwa katika
kukijenga Chama cha Hizbu ndani na nje ya nchi. Lakini, kwa bahati
mbaya, kama alivyokuwa hodari katika kukijenga, ndivyo alivyojaribu
kwa uhodari au ilivyo khasa kwa kiujanja kutaka kukibomoa baada ya
kushindwa kufikilia maslahi yake binafsi kwa kukitumilia chama.
(Baadae tutaeleza aliyoyatenda katika kukibomoa chama na kuifisidi
nchi). Alipojiunga Sheikh Ali Muhsin katika chama cha HizbulWattan
Zanzibar Nationalist Party (ZNP) aliwapa shauri wakuu wa Chama
kumtaka Babu achukue mafunzo katika kuendesha chama na baadae aje
asaidie katika uendeshaji wa ZNP. Wakuu wakapendezewa na shauri
hiyo, na Babu akawafik. Sheikh Ali hapo tena aliiomba Labour Party
ya huko Uingereza kwa kupitia kwa (wasta wa) Mr. John Hatch na Mrs.
Eirene White M.P. na Labour Party ikakubali kumpokea Babu kwa
mafunzo. Mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi sita. ZNP (Hizbu)
ililipia gharama zote za kimaisha kwa muda huo na za safari. Katika
muda huo pia aliendelea kulipwa mshahara akiwa ni Executive
Secretary wa Chama ZNP. Utaona dhahiri kuwa imani ya Hizbu juu ya
elimu na maarifa haikufungika sehemu mmoja tu, bali ilikuwa ni kwa
kila upande. Hizbu iliamini kuwa uwongozi mwema wa chama na nchi
utapatikana kutokana na watu wenye ujuzi na maarifa, kwa hivyo
iliona umuhimu wa kumpatia mafunzo na elimu ifaayo Katibu Mtendaji
wake khasa, na wengine wafuatie. NATIJA YA SAFARI YA SHEIKH ALI
MUHSIN Kama tulivyoeleza hapo mwanzoni kuwa Sheikh Ali Muhsin
alizitembelea baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na Uingereza kwa ajili
ya kugombania kupatikana kwa mabadiliko ya Katiba ya Kuanzishwa kwa
uchaguzi wa "Common Roll" yaani "One Man One Vote" katika Zanzibar.
Natija ya safari hiyo, Serikali ya Kiingereza, ilimleta Zanzibar
Mr. Coutts akiwa ni mchunguzi juu ya maendeleo ya Katiba. Mchunguzi
huyo alifika Zanzibar kati ya mwaka wa 1956. Chama cha Hizbu
kilifanya maandamano makubwa kwa kumpokea Mr. Coutts hapo kiwanja
cha Ndege cha Kiembe Samaki siku aliyofika Zanzibar. Waandamanaji
walichukuwa mabango yaliyokuwa yameandikwa: "TUNATAKA UCHAGUZI WA
ONE MAN ONE VOTE" "TUNATAKA UHURU WA NCHI YETU" "TUMECHOKA
KUTAWALIWA'' ''TUNAPINGA "UBAGUZI WA RANGI NA WA UKABILA" Mjumbe
huyo alipokuwa nchini alikutana na wananchi pamoja na wakaazi mbali
mbali wa nchini. Alionana hata na watu binafsi. Na alipokea risala
(za maandishi na za mdomo) kutoka vyama mbali mbali vya kikabila na
vya kidini. Chama cha Hizbu nao walionana na mjumbe huyo na
walimkabidhi risala yao yenye kutilia nguvu matakwa yao, matakwa
ambayo ndio msingi wa ujumbe wake wa kuja Zanzibar. Inafaa
ifahamike kuwa tangu kufika kwa mchunguzi huyo na mpaka kuondoka
hapakuwepo chama cha kisiasa nchini isipokuwa kimoja tu
HizbulWattan. Vyama vyote vya kisiasa vyengine viliasisiwa baadae.
Kwahivyo HizbulWattan ndicho chama cha mwanzo cha kisiasa kuasisiwa
Zanzibar. Mr. Coutts alipomaliza shughuli zake alirejea kwao. Baada
ya muda alileta mapendekezo ya uchunguzi wake kwa Balozi wa
Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar. Katika mapendekezo
yake hayo, Mr. Coutts alikubali kuwa Zanzibar inafaa kuanzishwa
uchaguzi wa "Common Roll" yaani uchaguzi wa kwa pamoja, bila ya
kujali khitilafu za kabila. Lakini alipendekeza kuwa uchaguzi
uanzie kwa viti sita na vilivyobakia viendelee katika mpango ule
ule wa kuteuliwa na Balozi wa Serikali ya Kiingereza kwa
kushauriana na Mfalme wa nchi. Pia katika mapendekezo yake, Bwana
Coutts alitaka Balozi wa 13
Kiingereza aendelee kuwa Mwenye Kiti wa Baraza la Kutunga Sheria
na watumishi wa Serikali ya Kiingereza waendelee kuwa waongozi wa
upande wa Serikali. Hizbu haikuridhika hata kidogo na mapendekezo
hayo, kwa vile asli ya madaai yao ni kuwa Wawakilishi wote wa
Baraza la Kutunga Sheria wawe ni wananchi waliyo chaguliwa na
wananchi kwa uchaguzi wa "One Man One Vote". Juu ya hivyo, Hizbu
ilikubali kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuona kuwa msingi wa
matakwa yao ulipatikana; nao ni kuanzishwa kwa uchaguzi wa "Common
Roll". Kwa kukubaliwa misingi hii Zanzibar ikawa ndiyo nchi ya
mwanzo katika Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na ya Kusini
kuanzishwa uchguzi kama huo. Baada ya kupatikana haya HizbulWattan
ilizidisha juhudi za kuwafahamisha wananchi misingi na faida ya
kuchaguwa Wawakilishi wao kwa kupitia uchaguzi huo. WAKOLONI NA
NYERERE NDIO WAASISI WA AFROSHIRAZI Wakuu wa Serikali wa Idara ya
Utawala, Zanzibar baada ya kuona kuwa mpaka kuondoka kwa mchunguzi
Coutts Zanzibar na mpaka kuleta mapendekezo ya uchunguzi wake,
hapakuweza kuasisiwa chama chengine cha kisiasa nchni ili kipate
kushindana na HizbulWattan (ZNP), waliamua kumtumilia Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere. Wakoloni walimtumilia Mwalimu kwa kuja
Zanzibar kujaribu kuwashawishi waongozi wa vyama viwili vya
kikabila waweze kuungana na kuasisi chama kimoja cha kisiasa ili
kiweze kushiriki katika uchaguzi na kiweze kuwa pingamizi kwa Chama
cha Hizbu. Katika ripoti ya Mr. Penny aliyekuwa Muangalizi wa
Uchaguzi aliandika, "Ofisi yangu na Idara ya Utawala zilisaidia
kuundwa kwa AfroShirazi na kwahivyo ikaokolewa Zanzibar na kuwa na
utawala wa chama kimoja wa namna ya khatari." Mwalimu Nyerere
alikuja Zanzibar pamoja na Sheikh Zubeir Mtemvu mnamo mwisho wa
mwaka 1956. Mwalimu pamoja na ujumbe wake alikutana na waongozi wa
African Association, Sheikh Abeid Amani Karume, Bwana Mtumwa
Borafia na Bwana Boniface. Waongozi wa Shirazi Association
aliokutana nao Nyerere katika ujumbe wake huo ni, Sheikh Ameir
Tajo, Sheikh Thabit Kombo Jecha na Sheikh Othman Shariff Musa.
Mkutano huo ulifanyika katika nyumba ya Sheikh Abeid Amani Karume
iliyokuwepo mtaa wa Kachorora, Mwembe Kisonge. Nyumba hiyo kwa
wakati huo, ilikuwa ikikaliwa na Maalim Haji Ali Mnoga na Bwana
Hija Saleh Hija. Njama hizo za wakoloni pamoja na Mwalimu Nyerere
zilifanikiwa. Taarikhi 2 Februari 1957, miezi michache tu kabla ya
kufikia uchaguzi wa mwanzo wa Juni, 1957 Chama cha AfroShirazi
kiliasisiwa rasmi (kikiwa ni muungano wa jumuiya mbili za kikabila
yaani "African Association na Shirazi Association"). Karume akawa
Rais wa chama, Sheikh Ameir Tajo Makamo wa Rais na Sheikh Thabit
Kombo Katibu Mkuu. Uwongozi wa chama haukwenda kwa mzalendo,
haukwenda laa kwa Sheikh Ameir Tajo walaa kwa Sheikh Thabit Kombo,
walaa kwa Sheikh Othaman Shariff, bali kwa Mzee Karume. Mbinu na
njama za kuuwangamiza Uzanzibari zilianzwa zamani. UCHAGUZI WA
MWANZO JUNI 1957 Kutokana na mapendekezo ya uchunguzi wa Bwana
Coutts kukhusu uchaguzi, uchaguzi wa mwanzo ulifanyika, June, 1957.
Na kwa uchaguzi huo ndio wananchi wa Unguja na Pemba kwa mara ya
kwanza waliweza kushiriki katika kuwachagua Wawakilishi wao wa
Baraza la Kutunga Sheria la nchi yao. Uchaguzi huu ulikuwa wa viti
sita. Majimbo mane yalikuwa kwa Unguja na mawili Pemba. Majimbo
sita hayo yaligaiwa kama hivi: Unguja: Majumba ya Mawe Unguja:
N'gambo Unguja: Kaskazini Unguja: Kusini Pemba: Kaskazini Pemba:
Kusini Sheikh Ali Muhsin alisimama katika jimbo la N'gambo akiwa ni
Mwakilishi wa HizbulWattan, akishindania na Sheikh Abeid Karume
akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi, na Sheikh Ibuni Saleh alisimama
katika jimbo hilo hilo akiwa ni mgombea huru. (independent
candidate). Bwana Rutti Bulsara alisimama katika jimbo la Majumba
ya Mawe akiwa Mwakilishi wa Hizbu na washindani wake wakiwa, Bwana
Choudhry, Mwakilishi wa Muslim Association, Bwana Anverali Hassan
Virji, mgombea huru na Bwana AbdulQadir 14
Mukri, akiwa naye pia ni mgombea huru. Sheikh Amour Zahor
alisimama jimbo la Kusini akiwa ni Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh
Ameir Tajo akiwa ni Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo.
Sheikh Haji Muhammad alisimama katika jimbo la Kaskazini akiwa
mgombea huru akiungwa mkono na Hizbu, Sheikh Daud Mahmoud yeye
alikuwa Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo. Hizbu
ilimuunga mkono Sheikh Haji Muhammad kwa kuamini kuwa ana fikra za
kizalendo, na kutarajia kuwa hayuko mbali bali naye atajiunga na
wananchi wenziwe ndani ya HizbulWattan; na hakika ikawa hivyo.
Pemba Kusini alisimama Sheikh Rashid bin Ali Khaify akiwa
Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh Muhammed Shamte Hamad alisimama jimbo
hilo akiwa mgombea huru. Pia alisimama katika jimbo hilo Sheikh
Abdalla bin Suleiman Busaidy, akiwa naye ni mgombea huru. Pemba
Kaskazini, alisimama Sheikh Rashid Hamad Othman akiwa Mwakilishi wa
Hizbu, Sheikh Ali Shariff Musa akiwa mgombea huru na Sheikh Shaaban
Soud Mponda akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi. Matokeo ya uchaguzi
huo, Chama cha AfroShirazi kilipata viti vitatu Unguja na
hakikuweza kupata hata kiti kimoja Pemba. HizbulWattan ilishindwa
kupata hata kiti kimoja laa Unguja wala Pemba. Viti viwili vya
Pemba vilichukuliwa na wagombea huru wake, yaani Sheikh Muhammed
Shamte na Sheikh Ali Shariff, baadae waliviunga viti vyao kwenye
AfroShirazi na kuwa na viti vitano katika Baraza jipya la Kutunga
Sheria. Kiti kimoja cha Nyumba za Mawe, kilichukuliwa na Bwana
Chodhry Mwakilishi wa Muslim Association. Natija hii ya uchaguzi
inathibitisha kuwa Hizbu ni chama kilicho asisiwa bila ya kutokana
na asili ya chama au jumuiya ya kikabila iliyokuwepo nchini kwa
muda, kama vile ilivyokuwa hali kwa AfroShirazi. Na kwa vile
HizbulWattan ilikuwa ndio kwanza chama kichanga haikustaajbu kwa
kutopata hata kiti kimoja katika uchaguzi huu, kwani kilikuwa bado
hakijawafikilia wananchi kwa wingi. Amma AfroShirazi ambayo ni
muungano wa jumuiya mbili za kikabila, jumuiya ambazo kwa muda
zilikuwa zishakuwepo nchini hakikupata taabu kupata ushindi wa
uchaguzi huu, kwani wanachama wake ndio walewale. Tafauti na
HizbulWattan ambayo ilibidi ikuwe kwa kupitia kwa wananchi pole
pole. KWANINI SHEIKH ALI MUHSIN ALIAMUA KUSIMAMA N'GAMBO BADALA YA
MAJUMBA YA MAWE? Sheikh Ali alikuwa na hakika mia juu ya mia kuwa
hatoweza kumshinda mpinzani wake katika sehemu hiyo kama alivyokuwa
na hakika kuwa angeweza kupata ushinde ingekuwa amesimama katika
Jimbo la Majumba ya Mawe. Lakini alitaka kuthibitisha kuwa kura
chache za wananchi wenye asili mbali mbali zilikuwa pia nazo zina
umuhimu katika kuendeleza siasa ya chama, si kasoro kuliko kura
nyingi ambazo angeweza kuzipata katika Majumba ya Mawe. Lengo
lilikuwa ni kuondoa ukabila na urangi. Kura 918 ndizo alizozipata,
lakini zilikuwa na umuhimu mkubwa kwa chama na ziliongezea kumpa
moyo zaidi katika kuendelea na juhudi za ugombozi wa nchi. Uchaguzi
ulifanyika kwa salama na ulimalizika kwa salama ingawa wakoloni
walijaribu kutaka zitokee fujo wakati wa uandikishaji wa uchaguzi.
Kwani badala ya wao (wakiwa ndio serikali) kuchukua dhamana ya
kuchunguwa na kuhakikisha ni nani mwenye kustahiki kuchagua na
kuchaguliwa, kazi hiyo waliitupia vyama vya siasa. Kweli sheria
waliziweka za kuwa ni raia wa Zanzibar tu ndiye mwenye haki ya
uandikishaji na upigaji wa kura, lakini sharia hizo hawakuzilinda
na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa. Matokeo yake kulitokea kupingana
na kuzozana baina ya watu wenyewe kwa wenyewe na hayo ndiyo
yaliyozidi kupalilia chuki na ukhasama. Katika uchaguzi huu, wageni
wengi khasa kutoka Tanganyika ambao walikuwa wakiishi Zanzibar
walipenya katika kujiandikisha na walipiga kura. Hata hivyo, si
haba uchaguzi uliweza kufanyika kwa salama bila ya kutokea fujo la
namna yoyote. KWENYE SHARI HUZALIWA KHERI Kushindwa HizbulWattan
katika uchaguzi wa mwanzo, ndiko kuliko zidi kuwazinduwa wananchi
na kujitokeza paruwanja katika kusimama bega kwa bega na wananchi,
wazalendo wenziwao katika juhudi za kuigomboa nchi yao kutokana na
ukoloni wa Kiingereza. Baada ya kumalizika kwa machofu ya pirika
pirika za uchaguzi, Chama cha Hizbu kilitayarisha mkutano maalumu
wa hadhara katika Jumba la Seyyid Khalifa Hall (sasa ati linaitwa
"Karume House"). Umma wa kike na wa kiume uliomiminika siku hiyo
ulikuwa wa aina ya peke yake. Haukupata kutokea tangu kuanza kwa
harakati za kisiasa katika Zanzibar. Kwa jinsi mabibi walivyokuja
kwa wingi kwenye mkutana huo, ililazimu wanaume wote waliyokuwemo
katika ukumbi wa jumba hilo watoke nje kwa kuwapisha mabibi.
Wanaume, wao walikaa katika uwanja wa Bustani ya jumba hilo. Siku
hiyo ndipo wanawake walipodai wawe na Sehemu yao katika Chama, na
wapate kura sawa na wanaume. Waliopiga kifua mbele kati yao ni
BiZuhura bt Saleh, 15
BiSharifa Ahmed na BiZamzam Sultan. Kuanzia siku hiyo, kila
usiku uchao, wananchi wake kwa waume walikuwa wakijitokeza kwa
wingi katika kujiunga na Chama cha Wazalendo wenziwao. Waongozi wa
chama kwa kulingana na umma unavyozidi kujiunga na chama kila siku
ilibidi watengeneze mipango kukhusu kueneza mafunzo na siasa ya
chama kila upande. KUKUWA KWA HARAKATI ZA SIASA Baada ya kumalizika
kwa uchaguzi wa Juni 1957, Hizbu ilianza kutayarisha mipango ya
kueneza fikra na siasa ya chama kwa Unguja na Pemba kwa mjini na
mashamba. Natija ya juhudi hizo haikuchukuwa muda illa zilidhihiri.
Matawi ya Hizbu yalikuwa yakifunguliwa kila siku Unguja na Pemba,
mjini na mashamba. Kila Tawi lilikuwa na skuli ya kusomeshea vijana
na watu wazima (wa kike na wa kiume) waliokuwa hawakuwahi kuingia
skuli wakati wa udogo wao. Vilevile kila Tawi lilikuwa ni kituo cha
kutoa "Huduma ya Kwanza" (First Aid) kwa wenye kufikwa na maradhi
madogo madogo. Vijana wa Youth Own Union ndio waliyokuwa walimu wa
kusomesha na ndio waliyokuwa waganga wa kutibu maradhi madogo
madogo. Sheikh Juma Aley, aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali
ya ZNP/ZPPP, yeye ndiye aliyekuwa akiwapa vijana hao mafunzo ya
haraka juu ya namna ya kusomesha. Dr. Said Aboud Bin Tahir, yeye
alikuwa akiwapa mafunzo juu ya matibabu madogo madogo. Sheikh Ali
Makka na Sheikh Juma Ali (dogo dogo), wao wakijitolea kwa kuwapa
wogonjwa matibabu katika kituo cha matibabu cha Hizbu kilichokuwepo
katika jumba la Makao Makuu ya Chama, hapo Darajani. Katika kituo
hicho vilikuwepo kila vifao vyenye kuhitajika kwa matibabu.
Wagonjwa walikuwa wakiangaliwa na wakitibiwa bila ya malipo yoyote
na bila ya kutizamwa msimamo wao wa kisiasa. MuHizbu na MuAfro wote
walikuwa wakipata matibabu sawa sawa. Pia katika Makao Makuu hayo
ya chama kulikuwepo na sehemu ya "Welfare" ambayo ilikuwa
ikijishughulisha na mambo ya kutoa misaada ya dharura kwa mwananchi
yoyote (si kwa wananchama wa Hizbu tu). Sehemu hiyo ya "Welfare"
ilikuwa na gari mbili za kuchukulia wagonjwa (ambulance) kutoka
majumbani mwao kwa wale waliokuwa hawawezi kwenda kwa miguu yao au
wanaishi katika sehemu zilizo mbali na hospitali, kama mashamba na
sehemu zengine. Pia sehemu hiyo ya "Welfare" ilikuwa ikishughulikia
kuweka majina ya wananchi wanaojitolea kutoa damu kwa kuwasaidia
wagonjwa. Ilifika hadi hospitali kuu ya serikali wakihitajia damu
kwa sababu ya wagonjwa, wakenda katika sehemu hiyo ya "Welfare" ya
Hizbu kuomba watu wa kutoa damu. Vilevile ilifika wakati mmoja
hospitali ya serikali kuazima dawa fulani kutoka katika kituo cha
Hizbu cha matibabu. Sehemu hiyo ya "Welfare" ilikuwa chini ya
uangalizi wa Seyyid Hashim Bin Abubakar Bin Salim, Bibi Aisha Salim
(maarufu Bibi Aisha wa YOU au Aisha Mtumbatu) na Bibi Azza Mohammed
Seif (mamewatoto wa Sheikh Ali Muhsin). Miongoni mwa harakati za
Hizbu katika kuwahudumia wananchi, wazee na vijana wa kiume na wa
kike walijitolea bila ya malipo kwa ujenzi wa njia ya Nungwi.
Mwishowe Serikali ikaingia kusaidia katika ujenzi huo kwa kuleta
mipango ya siku moja kuwalipa na siku moja ya kujitolea. Yaani
katika siku 30, wakilipwa siku 15. Mpango huo ukiitwa "Jisaidie
Nikusaidie". Vilevile Mahizbu kwa kuendeleza huduma kwa wananchi
wenziwao walijitolea kuijenga njia ya Uzi toka mwanzo mpaka mwisho,
kwa kuunganisha kisiwa cha Uzi na kisiwa kikubwa cha Unguja hapo
Unguja Ukuu. Pia walijitolea kuwapelekea maji ndugu zao wa Tumbatu.
Wakati wananchi wa Tumbatu walipokuwa na shida kubwa ya maji Chama
kilikodi matishali na kupakia mapipa ya maji kutoka mjini mpaka
Tumbatu. Ikiwa nitaendelea kutaja ya kheri yaliokuwa yakifanywa na
Chama cha Hizbu katika kuwahudumia wananchi, basi itanifanya
nisiendelee na hayo niliyo yakusudia khasa kuzungumza na wananchi
wenzangu. Kwahivyo, haya machache yanatosha kukupeni sura na fikra
namna gani Chama cha Hizbu kilivyokuwa kikiendeshwa. Na kutokana na
maendesho kama hayo, ndipo kila uchao wananchi walikuwa wakijiunga
na Wazalendo wenziwao. ATI HUSEMWA KUWA HIZBU IMEFELI! Ikiwa Hizbu
imefeli, iliyofuzu ni ipi!? Yaliyofanywa na Hizbu kikiwa ni chama
tu cha siasa, basi serikali ya Zanzibar hii iliyokuwepo ya
"Mavamizi" kwa muda wa miaka 30 (1964 - 1994) haijaweza kuyafanya.
Hospitali za serikali kuwa hazina hata vidonge vya Panadol licha ya
Penicillin, ndio kufuzu huko? Skuli za serikali kuwa hazina hata
madeski ya kukalia, licha walimu wajuzi wa kusomesha, ndio kufuzu
huko? 16
Wanafunzi wa Chuo cha Kujifunza Uwalimu hawana hata matandiko
wala mashuka katika vitanda vyao. Chakula ni cha mipango mipango na
wakati mwingi wanafunzi wanalala na njaa kwa ukosefu wa chakula cha
kutosha. Huko, ndiko kuffuzu! Barabara hazipitiki kwa uchafu wa
maji ya makaro. Katika kila taa 10 za njiani, taa mbili tu ndizo
zinazowaka na muwako wenyewe utadhani globu ya kurunzi (tochi)
uchwara. Huko ndio kufuzu? Baada ya miaka 30 ya utawala wa Serikali
yenye kujiita ya 'mapinduzi', kiwanja cha ndege cha Zanzibar hakina
hata kiti kimoja cha kukalia wajao kuwashindikiza wasafiri wao.
Ikiwa huko ndio kufuzu, basi hatujui kufeli kutakuwa na sura gani!
Inaweza kuwa huko ndio kufuzu, yategemea nia na azma za waongozi wa
hizo serikali. Bali kwa nchi na wananchi huko hata kwa lugha gani
hakuitwi kufuzu, bali ni kudamirika. Kudamirika ambako ni sawa na
kuteremkiwa na balaa, kwani iteremkapo balaa ya Mwenye Enzi Mungu
(kwa maasi ya binaadamu) humfika mwema na mbaya. Maafa ya Zanzibar
yamemteremkia kila mwananchi, mwema na mbaya, (Inshallah wako hao
wema). Sababu kubwa ya hivyo ni kuwa juu ya maovu yaliofanywa na
yaendeleayo kufanywa hakuna tena kukatazana maovu na kufahamishana
kutenda mema, na hapo ndipo Mwenye Enzi Mungu azidishapo nakama
Zake. Mwenye Enzi Mungu tunakuomba utunusuru. KUGAWANYIKA KWA
AFROSHIRAZI Mwanzoni mwa 1959 kulitokea mgawanyiko wa waongozi wa
Chama cha AfroShirazi. Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Ali Shariff
waliamua kujitoa katika chama na kwa kutoka kwao, kulifuatiwa na
wanachama wengi nyuma yao khasa Pemba. Katika wakati huo huo, Chama
cha AfroShirazi kilimfukuza katika chama Sheikh Ameir Tajo kwa
singizio la kuwa alikwenda kuwaombea msaada wa fedha vijana wa YASU
(Young African Social Union) kwa Sir Tayabali Karemjee kwa ajili ya
ujenzi wa klabu (club) yao iliyokuwepo Miembeni, bila ya kuiarifu
kamati kuu ya AfroShirazi. Sababu kubwa zilizompelekea Sheikh
Mohammed Shamte na wenziwe kujitoa katika Chama cha AfroShirazi ni
zenye kutokana na hisia za uwananchi khalisi kwa nchi yake. Hisia
zake za kisiasa na nyendo zake pamoja na matarajio yake juu ya nchi
yake yalikuwa ya kutaka kutumikia upatikane uhuru wa Zanzibar.
Uhuru utaongozwa na Wazanzibari wenyewe bila ya kuchukua amri au
shauri kutoka pahala pengine popote. Sheikh Karume yeye alikuwa
hawezi kufanya lolote bila ya kuzungumza na Mwalimu Nyerere na kama
itavyoamuliwa na Mwalimu, ndivyo hivyo hivyo atavyofuata hata ikiwa
si maslahi kwa Zanzibar (na mara nyingi hivyo ndivyo ilivyokuwa).
Sheikh Mohammed Shamte, hayo yeye alikuwa hayakubali; kwahivyo
daima walikuwa wakibuburushana mpaka mambo yalipofika hadi ya
kufanywa mikutano ya Kamati Kuu ya Chama bila ya kuarifiwa Sheikh
Mohammed kwa kukhofiwa kuwa akiwepo ataleta upingaji juu ya baadhi
ya mambo. Ilipofika kiwango hichi, maji kuzidi unga, Sheikh
Mohammed na Sheikh Ali Shariff walijitoa katika AfroShirazi.
KUASISIWA KWA ZANZIBAR AND PEMBA PEOPLES' PARTY (ZPPP) Chama cha
Z.P.P.P. kiliasisiwa Novemba, 1959. Raisi wa Chama alikuwa Sheikh
Mohammed Shamte Hamad na Naibu Raisi alikuwa Sheikh Ameir Tajo.
Makao Makuu ya Chama yalikuwa Malindi Zanzibar. Z.P.P.P. kilikuwa
Chama cha wananchi wa Unguja na Pemba. Kwa Unguja hakikuweza kupata
wanachama wengi kwa wakati huo lakini kwa Pemba kiliweza kupata
wananchi wengi kujiunga katika chama. Misingi na dhamiri ya
Z.P.P.P. ikilingana na ya HizbulWattan. Nayo ni kufanyakazi kwa
pamoja Wazanzibari wote, bila ya kubali rangi, kabila au imani zao
za kidini katika kugombania kupatikana Uhuru wa Zanzibar kwa ajili
ya mslahi ya wananchi wote. Waongozi wa HizbulWattan hawakuwa na
shaka yoyote juu ya uzalendo wa Sheikh Muhammed Shamte na wenziwe,
kwahivyo walikuwa wakiamini kuwa iko siku wataweza kufanyakazi
pamoja. TUME YA SIR HILLARY BLOOD Katika Mei, 1960 Serikali ya
Kiingereza baada ya juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na Chama cha
Hizbu juu ya kutaka yapatikane maendeleo zaidi juu ya mabadiliko ya
Katiba katika nchi, walimleta Sir Hillary Blood kutoka Uingereza
akiwa ni mchunguzi wa mabadiliko ya Katiba. (Huyu ni wa pili, wa
kwanza alikuwa Mr. Coutts). Hizbu kama kawaida yao waliandaa
maandamano makubwa kutoka kiwanja cha ndege cha Kiembe Samaki mpaka
mbele ya nyumba ya Balozi wa Kiingereza. Waandamanaji wote wa kike
na wa kiume, walichukuwa mabango yaliyoandikwa neno moja tu, "UHURU
1960".
17
Sir Hillary Blood alipofika Zanzibar alivikuta vyama vitatu vya
siasa, Zanzibar Nationalist Party (ZNP) yaani HizbulWattan,
AfroShirazi Party yaani A.S.P. na Zanzibar and Pemba Peoples' Party
yaani Z.P.P.P. Vyama vyote vitatu vilimpelekea Sir Hillary Blood
risala za matakwa yao na vilevile Sir Hillary alipokea risala
kutoka katika vyama vya wafanyakazi na kutoka kwa watu binafsi. Pia
alizungumza na kuchukua fikra na nasaha kutoka kwa watu mbali
mbali. Risala ya Hizbu na risala ya Z.P.P.P. zililingana sana
katika matakwa yao. Zote mbili zilitaka Wawakilishi wote wa Baraza
la Kutunga Sheria wawe wananchi waliyochaguliwa katika uchaguzi wa
"One Man One Vote". Na baada ya matokeo ya uchaguzi huo yafuatiye
mazungumzo ya Uhuru kamili wa Zanzibar. Ama risala ya AfroShirazi
Party, ilitaka Wawakilishi wote wa Baraza la Kutunga Sheria wawe 25
na katika hao 22 wawe ndio wa kuchaguliwa kwa njia ya uchaguzi na
watatu waliyobakia wawe miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali ya
Kiingereza waliopo nchini, hawa wateuliwe na Balozi wa Kiingereza.
Kwa faida ya wasomaji, nitazinukulu sehemu muhimu za risala zote
tatu, yaani ya Hizbu, ya AfroShirazi na ya ZPPP. Kwa kufanya hivyo
hapana shaka itakuwa faida zaidi kwa wananchi na khasa kwa
vichipukizi vyetu, na wao wapate kujionea kwa macho yao, chama gani
kilichokuwa kikiwakumbatia na kuwataka wakoloni waendelee katika
uwongozi wa Serikali ya Zanzibar. Pia wapate vilevile kujionea
wenyewe vyama gani vilivyokuwa vikitaka upatikane Uhuru kamili wa
nchi. Risala ya Hizbu ilikuwa kama hivi: "......It is unnecessary
now to argue whether or not it is our right to rule ourselves
compeletely and whether or not we have the capacity to do so. Those
days are over. There are now no two sides to the question.
".......In framing the recomendations regard should be paid to Her
Majesty's Government's view that the legislature should become
predominantly elective in character and that the executive should
be reorganized to permit the establishment of a ministerial system.
"......Under any circumstances you will be failing in your duty and
mocking the people of Zanzibar if you recommand anything less than
full independence for the country". Risala ya Z.P.P.P. ilikuwa kama
hivi: ".....That the Zanzibar and Pemba Peoples' Party feels that
this Sultanate should be given full independence within the British
Commonwealth soon after the next election. "....That the
Legislative Council should be of 30 members and that all 30 seats
should be contested on Common Roll Election as stipulated in your
terms of reference". Risala ya AfroShirazi Party ilikuwa kama hivi:
".......the AfroShirazi Party believes and recommends that the
Legislative Assembly should consist of no more than 25 seats of
which three seats should be reserved for exofficio members. The
rest should all be open seats to be fought in Common Roll Election.
"......The exOfficio members should be the Minister for Justice,
Minister of Finance and Minister of Defence and External Affairs.
"......It will indeed be fitting, and we entreat Her Majesty's
Government, that 30th October, 1960, should mark the granting of
selfgovernment to the people of these islands". Mimi sitoongeza
langu ila ninawaachia wasomaji baada ya kuzisoma risala zote tatu
waamuwe wenyewe, ni wepi hao waliyokuwa bado wakitaka kurambatia
urojo wa wakoloni. Ikiwa Wizara ya Uadilifu, Wizara ya Fedha na
Wizara ya Ulinzi na Mambo ya Nje, ziwe katika mikono ya wakoloni,
sasa wananchi watakuwa wamejitawala kitu gani? Ndio wenye kuitambua
siasa ya AfroShirazi, na kwa kujidhihirisha zaidi kwa kimaandishi
kama hivi, hawakustaajabu walipomuona Karume ameyatia mambo yote
muhimu kwa nchi, chini ya amri ya Serikali ya Muungano ambayo kwa
ukweli ni Serikali ya Tanganyika, chini ya amri ya kidikteta ya
Bwana Nyerere. Umoja wa Vijana wa Youth Own Union walikasirishwa
sana na mapendekezo ya Sir Hillary Blood. Kwa kuthibitisha uchukivu
wao, waliandaa mkutano maalumu wa hadhara katika mtaa wa Mwembe
Sanda, Miembeni, mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi.
Baada ya kusomwa mapendekezo ya 18
Mchunguzi huyo mbele ya wananchi, ilikubaliwa kuilani na
kuichoma moto ripoti hiyo, kwa vile ilivyo kwenda sana katika
kudharau matakwa ya wananchi. Pia ilikubaliwa katika mkutano huo
kumpelekea Sir Hillary risala maalumu kutoka kwa Umoja wa Vijana wa
Youth Own Union ya kupinga mapendekezo yake aliyoyatoa kukhusu
maendeleo ya Katiba katika Zanzibar. Mapendekezo aliyoyatoa Sir
Hillary Blood katika uchunguzi wake ni kuwa viti 22 tu viwe vya
kuchaguliwa katika uchaguzi wa "Common Roll Election" na viti
vinane viendelee kuwa vya kuteuliwa na Balozi wa Kiingereza kwa
kushauriana na Mfalme wa nchi, yaani vyote viwe 30. Mapendekezo
yake haya hayakuwa mbali na yale ya Chama cha AfroShirazi. Kama
tulivyoona hapo juu katika risala yao, AfroShirazi wao
walipendekeza kuwa viti vyote visizidi 25, kati ya hivyo vitatu
viwe vya wajumbe wa kuteuliwa na kuchukuwa nafasi muhimu katika
serikali. UCHAGUZI WA PILI, JANUARI 1961 Baada ya miaka mitatu
unusu tokea kufanyika kwa uchaguzi wa mara ya mwanzo, Juni 1957,
ulifanywa uchaguzi mwengine, katika Januari, 1961. Safari hii,
mabibi nao walipata fursa ya kushiriki katika uchaguzi. Uchaguzi
huu ulikuwa wa viti 22. Vyama vyote vitatu vilishiriki kwa
ukamilifu. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa, AfroShirazi walipata
viti 10, Hizbu viti tisa na ZPPP viti vitatu. Kwa natija hii,
hapakuwa na chama kilichoweza kuunda Serikali ila kwa kushirikiana
na chama chengine. Balozi wa Kiingereza Sir George Mooring
aliwaalika waongozi wa vyama viwili vikubwa, yaani Hizbu na
AfroShirazi kwa kuzungumzia tatizo liliokuwepo juu ya utaratibu wa
kuweza kuunda serikali. Baada ya mazungumzo marefu ya hivi na hivi
mwongozi wa Chama cha Hizbu, Sheikh Ali Muhsin alitoa shauri la
kutaka ifanywe serikali ya pamoja ya vyama vyote vitatu. Mwongozi
wa Chama cha AfroShirazi, Sheikh Abeid Amani Karume, yeye aliipinga
shauri hiyo na badala yake alitaka matokeo ya uchaguzi huo yafutwe
na pafanywe uchaguzi mwengine. Baada ya kuzozana zozana na
pasipatikane natija yoyote ya kurahisisha tatizo hilo, Balozi wa
Kiingereza, Sir George Mooring alimpa kila kiongozi katika hao
wawili muda wa wiki moja ajaribu kupata waakilishi waliyochaguliwa
kuchanganya viti vyao pamoja naye ili aweze kupata wingi wa viti
vya kumuwezesha kuunda serikali. Fursa hiyo kwanza alipewa Sheikh
Abeid Amani Karume kwa kuwa Chama chake kilipata kiti kimoja zaidi
kuliko Chama cha Hizbu. Wakati Karume alipokuwa katika juhudi za
kuzungumza na Chama cha ZPPP, kwa kuwataka waviunge viti vyao
vitatu upande wa Chama cha AfroShirazi, baadhi ya watumishi wa
Serikali wa kikoloni na khasa wa Idara ya Utawala, nao waliingia
kazini kwa kufunga njuga kwa njia za siri siri. Miongoni mwa
utumishi wao ilikuwa ni kukisaidia Chama cha Afro waweze kupata
viti vya kutosha waunde serikali. Kwa kutaka kutekeleza utumishi
wao huo walizungumza na Sheikh Othman Shariff na walimtaka afanye
kila njia na kila jitihada mpaka ampate Sheikh Mohammed Shamte
akubali kuvipeleka viti vyao (vya ZPPP) vitatu upande wa
AfroShirazi. Kwa ilivyokuwa Sheikh Othman aliahidiwa malipo fulani
fulani kama vile kulipiwa deni la nyumba yake ya "Kijipu House"
iliyokuwepo Gongoni, Zanzibar, na mengineyo yaliyokhusika na mambo
ya kisiasa, aliukubali utumwa huo. Na kwa kuwepo makhusiano ya
kuowana baina yake na Sheikh Mohammed Shamte, yaani Sheikh Mohammed
Shamte alimuowa binti wa Sheikh Issa Shariff (mtoto wa kaka yake
Sheikh Othman Shariff), na vilevile mmoja katika hao washindi
watatu wa ZPPP, alikuwa ni kaka yake yeye Othman, yaani, Sheikh Ali
Shariff, basi Sheikh Othaman aliona itamuwiya rakhisi kufuzu utumwa
huo. Othman aliingia mbioni kwa "Full speed". Baada ya kuona
jitihada zake zote alizozifanya za kumtaka Sheikh Mohammed Shamte
ayakubali matakwa yake zimefeli, alianza kumtishia kaka yake Sheikh
Ali Shariff kwa kumwambia kuwa, "Ikiwa na wewe hukubali kufuata
shauri yangu, basi hutoniona tena baada ya leo. Afadhali nijiuwe
kuliko kuona umeungana na Hizbu". Kwa kutaka kutimiza tishio lake
hilo kwa kaka yake, Sheikh Othman alitoka kwake na asijulikane
aliko kwenda, kwa muda mkubwa sana. Alijificha! Zogo la kutafutwa
Sheikh Othman lilianza mjini, vijana wa YASU upande wao na Polisi
upande wake. Kaka yake, Sheikh Ali Shariff aliingiwa na khofu na
kihoro kwa mapenzi ya ndugu yake. Aliwambia vijana wa YASU
wamtafute Sheikh Othman na watapomwona wamwambie kuwa yeye (Ali
Shariff) ameikubali shauri yake ya kukiunga kiti chake katika
upande wa 19
AfroShirazi. Haukupita muda mkubwa baada ya hapo, ila Sheikh
Othman alirejea kwake kutoka huko alikojificha, kwani baadhi ya hao
vijana wa YASU walikuwa wakijuwa mpango huo alioufanya Sheikh
Othman na wakijua wapi alipojificha. Kwa hivyo, walipopata uhakika
kwa Sheikh Ali Shariff wa kukubali kujiunga na AfroShirazi, mara tu
walizifikisha salamu hizo kwa Sheikh Othman. Muda wa wiki aliopewa
Karume ulimalizika kwa kupata kiti kimoja tu zaidi, yaani kiti cha
Sheikh Ali Shariff. Kwa kutowezakana kuunda Serikali kwa viti
walivyokuwa navyo AfroShirazi hadi wakati huo, basi Balozi wa
Kiingereza alimpa Sheikh Ali Muhsin naye muda wa wiki ajaribu
kupata waakilishi wa kujiunga naye ili aweze kupata wingi wa
kutosha wa kuwezesha kuunda serikali. Sheikh Ali pamoja na wenziwe
hawakuchukua muda mrefu ila waliweza kukubaliana na Sheikh Mohammed
Shamte na Sheikh Bakari Mohammed wote wawili hao wakiwa ni washindi
wa ZPPP kuviunga viti vyao upande wa Hizbu. Muda wa wiki mbili
ulimalizika na ikawa kila upande wanavyo viti kumi na moja.
Ilivyokuwa hali ndio hivyo, Balozi wa Kiingereza alitoa uamuzi wake
kuwa pafanywe Serikali ya Mshikizo ya muda wa miezi sita na baada
ya hapo pafanywe uchaguzi mwengine. Mwongozi wa Hizbu, Sheikh Ali
Muhsin, ilipokuwa hali imefika hadi hii alizidi kumnasihi mwongozi
mwenziwe Sheikh Karume kwa kumtaka atizame na kuyapa umuhimu
maslahi ya nchi kuliko ya vyama. Alimnasihi waondoe mzozo na
wakubaliane kuunda Serikali ya pamoja. Alizidi kwa kumfahamisha
Sheikh Karume kuwa kufanya hivyo kutainusuru nchi na kuingia katika
uchaguzi mwengine, ambao ni gharama na pia kukhatarisha usalama.
Pia alimueleza kuwa kuunda Serikali ya pamoja itawezesha nchi bila
ya kuchelewa zaidi kufikilia Uhuru. Sheikh Karume akiwa keshakuwa
na mipango na matakwa yake, mbali na maslahi ya nchi, yote haya
aliyakataa katakata na alishikilia fikra iliyotolewa na Balozi wa
Kiingereza ya kufanywa Serikali ya Mshikizo na kufanywa uchaguzi
baada ya miezi sita. Baada ya kuwa hakuna jengine isipokuwa
kutekelezeka shauri hiyo iliyotolewa na Balozi, lilizuka tatizo
jengine nalo ni, nani ataye kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali hiyo
ya Mshikizo? Sheikh Ali Muhsin alipendelea nafasi hiyo apewe raia
aliyekuwa na uzowevu juu ya mambo au uwendeshaji wa serikali.
Kwahivyo, alipendelea nafasi hiyo ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya
Mshikizo apewe Sheikh Ahmed Lakha, ambaye ni Mzanzibari, mwenye
ujuzi, maarifa, itibari na hakuwa mwenye kujiambatisha na chama
chochote. Mwongozi wa AfroShirazi Sheikh Abeid Amani Karume
alikataa katakata kukhusu nafasi hiyo kupewa Sheikh Ahmed Lakha.
Yeye alitaka nafasi hiyo apewe Bwana Roberts, mfanyakazi wa
Serikali ya Kiingereza ambaye wakati huo alikuwa ni "Chief
Secretary" wa Serikali ya Zanzibar na pia ndiye aliyekuwa akikamata
nafasi ya Ubalozi wa Kiingereza wakati Balozi akiwa katika likizo.
Shauri ya mzee Karume ndiyo iliyokubaliwa na Balozi, Sir George
Mooring na Bwana Roberts akawa Waziri Kiongozi wa mwanzo wa
Serikali ya Mshikizo ya Zanzibar. Ukifuatia na kuzingatia utatambua
kuwa katika harakati za kisiasa hizi zilizopita muda wote huu,
fikra za ASP daima zilikuwa zikilingana na kukubaliana na fikra na
matakwa ya kikoloni. UCHAGUZI WA TATU JUNI 1961 Kwa kuchelea natija
ya uchaguzi huu kutokea kama ile ya uchaguzi uliopita (wa Januari,
1961) hata kutokumkinika chama kimoja pekee kuunda Serikali kwa
idadi ya viti walivyokuwa navyo, katika uchaguzi huu liliongezwa
jimbo moja na kufanya idadi ya viti vyote 23 badala ya 22.
Ushirikiano Wa ZNP/ZPPP Katika uchaguzi huu, Hizbu na ZPPP
walikubaliana na walitangaza rasmi kuwa watashirikiana katika
kusimamisha wagombea wao kwa pamoja. Yaani, jimbo litalo simamiwa
na mgombea wa Hizbu, ZPPP haitoweka mgombea wake bali wanachama
wote wa Hizbu na wa ZPPP watampigia kura mjumbe huyo na hivyo hivyo
kwa mgombea wa ZPPP. Fikra hii ilifanyika kwa kuzidi kutilia nguvu
umoja na vile kila siku idhihirivyo kuwa misingi na matakwa ya
ZNP/ZPPP juu ya maslahi ya nchi yakilingana. Ndugu zetu ASP wao
daima muelekeo wao (kama tulivyoona na tutavyozidi kuoona) ulikuwa
kinyume na hivyo, maslahi yao binafsi ndio yaliokuwa mbele.
20
AfroShirazi Iliandaa Machafuko Siku ya Uchaguzi Waongozi wa
Chama cha AfroShirazi walipoona ushirikiano wa Hizbu na ZPPP katika
uchaguzi, walijua kuwa hawatoweza kushinda, kwa hivyo waliandaa
kufanya machafuko katika vituo vya uchaguzi. Walianza kwa
kuwasukuma sukuma wanachama wa Hizbu na wa ZPPP khasa mabibi na
vizee. Waliendelea katika mipango yao hiyo ya fujo kwa kuwatowa
wanachama wa ZPPP/ZNP katika mistari waliyokuwa wamejipanga kwendea
kwenye masanduku ya kutilia kura. Ilipokuwa wanachama wa Hizbu na
ZPPP hawakukubali kutolewa katika mistari, hapo tena wanachama wa
AfroShirazi walianza kuwapiga wanachama wa ZNP/ZPPP kwa magumi,
mateke na mwisho walianza kutumia silaha kama visu, mapanga na
mawe. Michafuko hiyo ilianza katika vituo vya uchaguzi na baadae
iliendelea majumbani, mitaani na viamboni. Waongozi wa Hizbu na
ZPPP, walipoona wenziwao wao wanauliwa na kujeruhiwa,
waliwatangazia wao wote waondoke katika vituo vya upigaji kura na
waliwazuia waliyokuwa bado hawajafika katika vituo vya upigaji
kura, wasende mpaka watapoambiwa na chama chao ZNP/ZPPP kuwa wende
ndio wende. Michafuko hiyo ilimalizikia kwa kuuawa MaHizbu na
MaZPPP 68 na mamia kujeruhiwa vibaya vibaya. Wengi wao walibakia na
vilema vya muda na wengine vya milele. Michafuko hiyo ilianza tokea
saa 12 za asubuhi kabla hata kufunguliwa hivyo vituo. Na tokea
wakati huo, askari wa polisi walikuwa wamesha kuwepo katika vituo
vyote vya mjini na mashamba lakini walijifanya kama hawayaoni yenye
kutokea. Serikali ya kikoloni walipoona mambo yamezidi watu
wanauliwa na kujeruhiwa kwa wingi, ndipo walipoagizia kikosi cha
askari wa kuzuwia fujo (GSU) kutoka Kenya. Askari hao walifika
Zanzibar kiasi cha saa saba za mchana. Baada ya kuingia mitaani
waliweza kutuliza michafuko na kurejesha hali ya kawaida. Lakini
wakati huo waliyokuwa wameuliwa, wamesha uliwa na waliyokuwa
wamejeruhiwa, wameshajeruhiwa. Juu ya fujo hilo lililoandaliwa na
AfroShirazi katika uchaguzi huo kwa kufikiria kuwa kwa kufanya
hivyo watapata ushindi, wanachama wa ZPPP na Hizbu walisema, Mungu
Mmoja kheri tufe lakini hatutowacha kwenda kuzitia kura zetu. Baada
ya kuhisabiwa kura, AfroShirazi walijikuta na viti vyao vilevile 10
walivyovipata katika uchaguzi wa Januari 1961. ZNP/ZPPP walijipatia
viti 13. Katika sehemu ya Zanzibar kulikofanywa ukatili mkubwa sana
siku hiyo ya uchaguzi wa taarikh moja Juni 1961, hapakutokea kuliko
Bambi. Huko Mwalimu mmoja wa skuli, anayeitwa Bwana Ali Muhsin
Mshirazi (bwana huyu pia alishiriki katika mauwaji ya Januari 12,
1964) alishirikiana na makatili wenzake kwa kuwachukua vijana
wadogo, ambao wengi wao walikuwa ni miongoni mwa wanafuzi wake na
kuwatia ndani ya tanuri la kuchomea mbata kwa kuwadanganya ati kuwa
"anawahifadhi na ghasia ziliopo katika mji". Baada ya kuwatia humo,
waliiondoa ngazi waliyo wateremshia kisha waliwamiminia geloni kwa
mageloni ya petroli kisha wakawawasha moto. Vijana hao waliachwa
wakiteketea mpaka kuwa majivu. Tanuri hilo ndilo lililokuwa kaburi
lao. Jee nini kosa la vijana hao? Na wawe wana makosa ya aina
yoyote, jee ulimwenguni huu tuishio iko kanuni ya adhabu ya aina
hiyo? Kwa Kiislamu haifai kuadhibu kwa moto hata kwa mnyama mwenye
kudhuru. Seuze binaadamu, tena watoto wadogo! Malipo ya Mwenyezi
yanaanza tangu hapa duniani, natunayaona, kesho ndio hesabu na
malipo ya milele. Kwa bahati, mmoja kati ya vijana hao ambaye siku
yake ilikuwa bado Mwenye Enzi Mungu hajamuandikia, aliweza kupenya
wakati walipokuwa wenzake wana teremshwa ndani ya tanuri mmoja
mmoja. Kijana huyo, ndiye baadae aliyeweza kuzifikisha khabari hizo
katika mikono ya polisi na kuweza kukamatwa mikatili hiyo. Jambo la
kustaajabisha na kusikitisha ni kuwa mahakama iliyokuwa ikiendeshwa
na Naibu Jaji Mkuu mkoloni, Muingereza haikuweza kupata hata
mshitakiwa mmoja kati ya wote waliyopelekwa mbele yake kwa
mashitaka ya kuuwa, kuwa ni mukhalifu. Hakutokea hata muuwaji mmoja
aliyepewa adabu ya kuuliwa au hata ya kufungwa gerezani kifungo
kikubwa. Wote waliachiliwa huru. Katika kesi ya mwalimu (Ali Muhsin
Mshirazi) na mikatili wenzake, ushahidi aliyoutoa kijana yule mdogo
mbele ya mahakama, kila aliyekuwepo na kumsikia kijana huyo jinsi
alivyotoa ushahidi wake dhidi ya mikatili hiyo, aliona mikatili
hiyo itapewa adabu inayo wasitahikia. Hakimu wa kesi hiyo alipokuwa
anatoa hukumu yake alisema kuwa, "Ushahidi nilioupata kutokana na
kijana huyu ni ushahidi mzuri, na 21
nampa sifa kwa kutokana na umri wake na alivyoweza kutoa
ushahidi wake na alivyoweza kuikabili mahakama kwa ushujaa. Lakini,
nasikitika ushahidi wake haukuweza kupata kusaidiwa na mtu mwengine
ambaye mwenye umri mkubwa. Kwa kuwa huyu ni kijana mdogo, nashindwa
kuamini ushahidi wake peke yake. Kwa hivyo basi, sina budi na
kuwaachilia huru washitakiwa hawa"!! Yote haya tuliokuwa
tukitendewa na wakoloni, bado utamsikia Mwalimu Nyerere akidanganya
na akikejeli kwa kusema kuwa Chama cha HizbulWattan kikipendelewa
na wakoloni! Nyimbo hii ya kijanja na ya kejeli pia ikiimbwa na
waongozi wa hii serikali inayojiita ya 'mapinduzi'. Haikuimbwa na
hao tu, bali hata wale ndugu zetu tuliyokuwa pamoja kwa muda hapo
mwanzoni walikuwa shangweni kwa kujitafutia maslahi ya nafsi zao.
Maneno haya ni istihzai ya dhahiri, kwani ingelikuwa wakoloni
wameipendelea Hizbu bali sio kuipendelea, lakini lau wangelifanya
insafu na uaminifu tu basi hata hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'
yasingeweza kutokea. MUUNGANO WA ZNP/ZPPP, WAUNDA SERIKALI
Waswahili wanasema, "Wanja wa Manga, si Dawa ya Chongo". Fujo lote
walilolifanya AfroShirazi kwa kutarajia kupata ushindi, hawakupata
ushindi. ZNP/ZPPP, waliunda Serikali kwa kupata viti 13 kwa viti 10
vya AfroShirazi. Serikali hii ikiitwa, "Responsible Government"
yaani "Serikali ya Madaraka" kufikilia Uhuru. Sheikh Mohammed
Shamte Hamad ndiye aliyekuwa Waziri Kiongozi (Chief Minister) wa
Serikali hiyo. KUTOKUFAULU MAZUNGUMZO YA MWANZO YA KATIBA YA UHURU
Baada ya miezi 10 mpaka 11 tokea Serikali ya Muungano wa ZPPP/ZNP
"Serikali Ya Madaraka" kuwa katika madaraka, Serikali ya Kiingereza
ilikubali baada ya kushikiliwa na serikali hiyo ya madaraka kufanya
mkutano wa mazungumzo ya uhuru. Mkutano huo wa Katiba ya Uhuru
ulifanywa katika miezi ya Machi na April 1962 huko Lancaster House,
London. Pande zote mbili yaani upande wa Serikali na upande wa
Upinzani walihudhuria kwenye mkutano huo. Kwa bakhti mbaya mkutano
huo haukuendelea kwa siku nyingi illa ulivunjika bila ya
kukubaliana kwa kuwekwa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa
AfroShirazi walikataa kuzungumzwa chochote kilicho khusika na
kutolewa taarikh ya Uhuru mpaka kwanza pafanywe uchaguzi mwengine.
Baada ya matokeo ya uchaguzi huo, ndio yafuatie mazungumzo ya
kutolewa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa upande wa Serikali
waliwanasihi mwisho wa uwezo wao waongozi wa upande wa Upinzani
yaani AfroShirazi waache kuleta vizingiti vitavyo sababisha
kuchelewa kwa Uhuru wa Zanzibar. Bali waongozi wa AfroShirazi
walin'gan'gania uzi wao huo huo wa kupinga kuzungumzwa chochote
kitachofikilia kutolewa kwa taarikh ya Serikali ya Ndani kabla ya
kufanywa uchaguzi mwengine. Waongozi wa upande wa Serikali,
walipoona waongozi wa upande wa Upinzani hawataki kubadili msimamo
wao, walijaribu kuzungumza nao nje ya mkutano. Katika mazungumzo
hayo, upande wa Serikali waliutaka upande wa Upinzani wakubali
kufanyika serikali ya pamoja, yaani "Government of National Unity"
(hii ni mara ya pili ASP kupewa shauri na wenzao ZNP/ZPPP kufanya
serikali ya pamoja.) Katika serikali hiyo ya pamoja, upande wa
Serikali watawapa ASP wizara tatu kati ya wizara nane na pia
watawapa uwezo wa kutumia "veto" kwa jambo lolote litalotokea nao
wakaliona si maslahi kwa upande wao. Yaani ASP watakuwa na madaraka
sawa sawa na ZNP/ZPPP katika uendeshaji wa hiyo serikali ya pamoja.
Waongozi wa AfroShirazi baada ya kuyasikia hayo, walitaka muda wa
kuyazungumza na kuyazingatiya wakiwa peke yao, na waliahidi kutoa
uamuzi wao siku ya pili kabla ya kuhudhuria kwenye kikao cha
mkutano wa Katiba. Kwa dalili zote, walionesha kuwa wamevutika na
mashauri hayo, na ilikuwa kuna tamaa kuwa watawafik. Upande wa
Serikali walingojea kwa hamu na matumainio (pia na wasi wasi) kuwa
shauri waliyoitoa itakubaliwa au sana watataka wazidishiwe wizara
moja badala ya tatu ziwe nne, yaani wawe wao ASP na wizara nne na
ZNP/ZPPP wizara nne. Wakati ulipofika siku ya pili, waongozi wa ASP
wakiongozwa na Sheikh Karume walifika kwa Mawaziri. Walikataa hata
kukaa kitako, Karume alisema, "Tumeyazingatia mashauri yenu.
Mazuri! Lakini sisi hatutaki kushirikiana na nyinyi!" Wakazunguka
wakatoka. Kutokana na msimamo huo wa ukorofi uliopangwa, waliyokuwa
wakiutumia AfroShirazi, Mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri wa
Makoloni, aliufunga mkutano bila ya kuzungumzwa lolote kukhusu
maendeleo ya Katiba. Aliwashukuru wajumbe wote kwa kuhudhuria na
aliwataka warejee nyumbani mpaka 22
watapoweza kuwafikiana baina yao, wakati huo Serikali ya
Kiingereza itakuwa tayari kufungua tena mazungumzo ya maendeleo ya
Katiba. Wajumbe wote wa upande wa Serikali (isipokuwa Sheikh Ali
Muhsin) na wa upande wa Upizani, walirejea Zanzibar bila ya
kuwaletea wananchi Uhuru wa nchi yao waliwokuwa wakiungojea kwa
hamu kubwa. Wananchi wa Zanzibar kwa jumla walivunjika moyo na
matokeo haya. Baada ya kufuzu hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' ya
Januari 12, 1964, Katibu Mkuu wa AfroShirazi, Sheikh Thabit Kombo
alisema wakati akikhutubia mkutano wa hadhara mbele ya Makao Makuu
ya AfroShirazi, hapo Mapipa ya Ngozi, Kisiwandui: "Tunamshukuru
Mwalimu Nyerere kwa kutuvua mtego waliyotaka kutunasa Mahizbu
wakati wa mkutano wa mwanzo wa Katiba, huko Uingereza. Mahizbu
walitaka kutufanyia ujanja wa kutaka tuungane pamoja katika
kuendesha serikali na kwa kutaka kutimiza ujanja wao, walikiri
kutupa wizara tatu katika serikali yao. Lakini mzee Karume kabla ya
kusema lolote, alizungumza na Mwalimu kwa simu kumtaka shauri yake
juu ya jambo hilo. Mwalimu alimwambia mzee Karume asikubali kufuata
shauri hiyo ya Hizbu kwani huo ni ujanja tu wakutaka kusiwepo na
upinzani. Mkitaka shauri yangu kataeni. Ndipo mzee alipokataa",
alisema Thabit Kombo. Mara nyingi utamsikia Mwalimu akisema kuwa
yeye hakukhusika na lolote katika mizozo ya kisiasa ya Zanzibar.
Hatujui Mwalimu anataka akhusike namna gani zaidi ya hivyo
alivyokhusika (alivyo jikhusisha). Yeye Mwalimu ndiye aliyekiasisi
Chama cha AfroShirazi na ni yeye aliyekuwa, "master mind" katika
kuyaandaa hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'. Wavamizi wal