MAMBO YA ZAKA, UTOAJI, SADAKA, FUGU LA KUMI NA PESA
Lengo la makala hii siyo kuweka sheria yo yote! Lengo langu siyo
kukuambia wala kukuagiza utoe kiasi hiki au kiasi kile katika
utoaji wako! Kama umeokoka itakuwa tabia yako kutoa, na baada ya
kusoma makala hiyo, ni matumaini yangu kuwa utoaji wako utaongezeka
tu na utatoa kwa furaha ya moyo. Najua wapo wengi wanaifuata
desturi ya kutoa fungu la kumi pasipo nia mbaya, ndio maana sehemu
kadhaa za makala hiyo hayawahusu watu kama hao moja kwa moja (hasa
sehemu za mwisho). Kama unaifuata desturi ya kutoa fungu la kumi
kwa moyo safi mbele ya Mungu kwa sababu umefundishwa na wengine
ufanye hivyo, ni tuamaini langu utapata uelewa zaidi na bora kwa
kusoma makala hii. Pia inawezekana kabisa, wapo wachungaji
wanaofuata mambo hayo kutokana na mafundisho na mfumo wa madhehebu
yao bila nia mbaya, hapo pia ni tuamaini langu watapata kitu kwa
kusoma makala hii. Naomba utambue muktadha wa kila sehemu ya makala
hiyo bila kufikiri kwamba lazima kila sehemu inahusu wewe! Sitaki
kuwakosea watu ovyo ovyo!
Mzigo na lengo la makala hii ni lifuatalo: kuondoa kila nafasi,
kila hoja na kila hila ambazo viongozi mbalmabli wanazozitumia ili
kukulazimisha - kwa kukutisha na kwa kupotosha neno la Mungu –
kutoa pesa kanisani kadiri ya maagizo yao. Lengo la makala ni kuwa
tunalotoa, tutalitoa kwa moyo mnyofu sawasawa na neno la Mungu.
Naomba ukumbuke hayo unaposoma makala hiyo.
Upo mchanganyiko mwingi, na mafundisho ya uwongo kuhusu somo
hili la utoaji ni mengi.
Tatizo hapa si kwamba maandiko ya Biblia hayapo wazi, la hapana;
tatizo kubwa ni pale watu huifundisha mistari ya neno la Mungu nje
ya kile Biblia yenyewe inenavyo na inavurugwa ili kuwashinikiza na
kuwatisha waumini ili watoe. Msukumo wa yote hayo mara zote ni
uchoyo uliopo kwa upande wa wachungaji na viongozi wa madhehebu.
Matokeo ya kufanya hivyo ni kwamba waumini wananyonywa na kutumiwa
vibaya na hao ambao walipaswa kuwatumikia vizuri na kuwaongoza watu
katika maarifa ya Kristo na wokovu wake.
Sasa nataka wote tutazame juu ya kile kilichofundishwa na
kutendwa na KANISA LA AGANO JIPYA. Tunapoendelea kufanya hivyo,
tafadhali tukumbuke kuwa mitume walioliandikia kanisa katika Agano
Jipya walijua wazi na kwa uhakika kabisa kile kilichokuwa kinasemwa
na sheria ya Musa (juu ya fungu la kumi), na kwa kweli wao wenyewe
mitume wamelelewa na kukuzwa na sheria hizo. Kwa hiyo katika
kuwaandikia hao waumini juu ya mambo ya utoaji kwa Mungu, wangeweza
kabisa kupata fursa ya kufanya mrejesho na nukuu wa sheria ya Musa
- au hata kutoka katika sehemu yoyote ya nyaraka za Agano la Kale -
iwapo sehemu yoyote ya Agano lile ingewahusisha waumini wa
kikristo.
Kile ninachokiandika hapa kisimwongoze yeyote yule kutoa kwa
uhafifu au kidogo kuliko kile wanachokitoa sasa, lakini pengine hii
isaidie kukuchochea wewe uweze kumtolea Mungu zaidi na kumtolea kwa
moyo wa furaha.
UTOAJI KATIKA MAKANISA YA AGANO JIPYA.
Neno la Mungu liko wazi! Tusome tu! Kila mtu anaweza kuelewa
mambo yale yaliyofundishwa na mitume makanisani katika Agano Jipya.
Kwa hiyo, sasa tuyaangalia mistari yote ambayo moja kwa moja
inahusu jambo hili la utoaji - kwa kuwa hata Biblia yenyewe
haijakaa kimya juu ya jambo hili kubwa la kumtolea Mungu katika
kizazi hiki cha Agano Jipya.
Mstari wa kwanza ambao tutauangalia unapatikana katika kitabu
cha Matendo ya Mitume 11:29,
“…njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia
katika siku za Klaudio. Na wale wanafunzi, kila mtu kulingana na
uwezo wake alio nao, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao
waliokaa Uyahudi.”
Hapa sasa tunakiona kigezo kimojawapo kilichohamasisha kiwango
ambacho waumini walikitoa ili kuwasaidia waumini wengine ambao
walikuwa wakiteseka kwa kupungukiwa na mahitaji yao ya lazima -
waumini walitoa kila mmoja kulingana na uwezo wake alio nao (hiyo
ni tafsiri ya Kigiriki. Union Version ya Kiswahili inasema, “kwa
kadiri ya alivyofanikiwa”. Tutakutana na maneno hayo baadaye).
Kulingana na lugha hii iliyotumika hapa, basi ni wazi kuwa watu
walitoa pesa zao kwa viwango tofauti kabisa. Na inawezekana baadhi
yao walitoa viwango vya fedha zaidi kuliko hata asilimia kumi ya
mapato yao. Katika mazingira ya jinsi hii kiwango walichokitoa watu
hawa hakikuzingatia mfumo wa kikumi unaofundishwa leo makanisani na
wahubiri walio wengi wao. Badala yake utoaji ule ulizingatia uwezo
wao wa kutoa.
Lakini pia tunagundua kuwa waumini wale walizikusanya pesa hizo
kwa niaba ya Wakristo wenzao waliokuwa wanateseka kwa upungufu wa
mahitaji ya lazima. Tutakuja kuona kuwa matoleo mengi maalum
yalikuwa yakitolewa na kufanyika na kanisa lile la kwanza kwa
nyakati hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia waumini masikini
waishio katikati yao - hasa wale waliokuwa wamepungukiwa na
mahitaji yao ya lazima katika maisha yao.
Hebu basi tuangalie tena mstari mwingine muhimu wa neno la Mungu
ambao unahusika moja kwa moja na somo letu ambao unaonyesha kwa
uwazi kabisa kuwa utoaji haukuzingatia kanuni yoyote ile ya
asilimia katika Agano Jipya.
“Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu. Kama
nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. Siku ya
kwanza ya kila juma (yaani, jumapili), kila mtu kwenu na aweke
akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake…” (1 Wakor.16:1,2).
Kutokana na mistari hiyo hapo juu sasa tunaweza kupambanua mambo
muhimu matatu. Jambo la kwanza ni kuwa wazo au desturi ya kutenga
pesa jumapili ilifanyika kwa lengo la kuwasaidia Wakristo waliokuwa
wakiteseka kwa ajili ya kukosa mahitaji muhimu na ya lazima.
Jambo la pili ni kwamba, haijatamkwa popote pale hapa wala
mahala pengine popote pale kwenye Agano Jipya lote kwamba eti, pesa
zilizokuwa zikikusanywa siku ya jumapili zilikuwa ni mali ya
mchungaji - ya kwamba eti hiyo ilikuwa ni haki yake.
Na jambo la tatu ni kwamba kiwango cha pesa walichokuwa
wanakitoa waumini wale hakikuzingatia mifumo ya asilimia kumi
(kikumi) kama inavyodaiwa na kusukumwa leo makanisani, lakini
badala yake walitoa kadiri ya kufanikiwa kwake mtu yule atoaye pesa
hizo. (Huu hapa ni ukweli unaofanana na yale tuliyoyaona hapo juu
ambapo watu walitoa kulingana na uwezo alionao mtu yule.) Maelekezo
hayo yanamaanisha nini? Kwa baadhi, kwa mfano, ingemaanisha kuwa
Mungu amewafanikisha zaidi kiasi kwamba hata wasingehitaji nusu ya
mapato yao kwa wiki ile au mwezi ule, hivyo wangeweza kutoa nusu ya
mapato yao. Usinielewe vibaya! Hii sio sheria. Hapa naelezea tu
lile neno kuwa ‘kwa kadiri ya kufanikiwa kwake’ inavyomaanisha
katika baadhi ya mazingira mengine.
Mstari mwingine ambao nao tutauangalia ni mmoja ya mstari iliyo
wazi juu ya kanuni ya utoaji katika Agano Jipya. Mstari huo inaweka
kwa ufasaha wa hali ya juu kabisa juu ya misingi inayotupasa
kuifuata katika jambo hili la utoaji.
“Kila mtu ATOE KAMA ANAVYOKUSUDIA MOYONI MWAKE, SI KWA UCHOYO au
kwa KULAZIMISHWA, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo
mkunjufu.” (2 Wakor.9:7).
Hapa tena tunaona ya kuwa kutoa hakukuzingatia mfumo wa
asilimia, lakini ilikuwa ni kutoa kulingana na nini kila mtu
aliamua ndani ya moyo wake mwenyewe. Hii bila shaka inaweza
kutushangaza, lakini hayo ndiyo mafundisho ya mitume. Hata hivyo
kwa fundisho hilo bado mitume hawatupatii sisi fursa ya kuwa
wanyimivu au wavivu katika kumtolea MUNGU. Mambo yote yaliyoandikwa
hapo juu yanapaswa kututia moyo katika mwelekeo wa kinyume. Anasema
kile unachokiamua moyoni mwako kinapaswa kiwe ni kitu
kinachompendeza Mungu - na inampendeza Mungu kuwa tutoe kwa furaha
na wala si kwa uchoyo. Mioyo yetu inapaswa iwe imefunguliwa na
mitepetevu. Mtume Paulo anaendeleza hii kwa undani zaidi katika
ukweli unaofunua kuwa mambo mengi yanayofanyika makanisani leo yapo
kinyume na neno la Mungu - ni kwamba hatupaswi kabisa kutoa kwa
kulazimishwa na kusukumwa.
Na hapa sasa ndipo tunafikia katika ukweli wa umuhimu wa hali ya
juu katika somo hili la utoaji. Tafakari sana:
Hapa inasema kuwa ni kosa iwapo utakuwa unatoa kwa kuwa
umelazimishwa. Ni makosa kutoa iwapo unajisikia kuwa unalazimishwa
kutoa na mtu mmwingine! Iwapo itatokea kiongozi anakutishia kwa
laana kwa sababu eti hutoi, basi pia ni makosa. Kutoa kwa sababu
unataka kutoa ili uikwepe laana, ni makosa. Ni makosa kutoa kwa
kuinyenyekea sheria - hii inawakilisha utoaji usio wa lazima
utokanao na hofu kwa sababu ya shinikizo na wala si kwa uhuru
utokanao na upendo. Mambo haya yote ni kumtolea Mungu kwa sukumwa
na mambo ya hofu, kulazimishwa pamoja na mafundisho maovu na
matendo ya uovu.
Nasema tena, ikiwa wewe utatoa kwa sababu umefanywa na mtu
ujisikie ni lazima kutoa, ndipo utakuwa hutoi kwa moyo wa furaha.
Ikiwa mtu fulani atakusukuma wewe kutoa kwa sababu ya sheria
iliyopo katika Agano la Kale, kwa kufanya hivyo watu hao wanafanya
kinyume kabisa na neno la Mungu kama lilivyotangazwa na mtume
Paulo. Ikiwa mtu fulani atakutishia wewe kwa laana katika Agano la
Kale ili kukulazimisha wewe kutoa, ndipo sasa watu hao watakuwa
wanatenda dhambi dhidi yako, pia wanamtenda dhambi Kristo.
Na wachungaji wengi pamoja na viongozi wengi wanakosea sana, na
wanafanya dhambi dhidi ya washirika wao kwa kuwaambia, “Utalaaniwa
kama usipotoa zaka au fungu la kumi”. Fundisho la jinsi hiyo
limejaa uwongo mtupu! Mitume wenyewe hawakufundisha hivyo. Bwana
Yesu mwenyewe wala naye hakufundisha hivyo. Hakuna mahali popote
katika Agano Jipya ambapo utakuta mitume wanawasukuma watu au
kuwatisha waumini katika kutoa kwa kunukuu Malaki 3:8 -10!
Kadhalika hakuna mstari wowote wanaounukuu kutoka katika Agano la
Kale ili kuwasukuma waumini wao katika kutoa. Mitume walijua vizuri
sana kile ambacho Agano la Kale kinafundisha juu ya utoaji kikumi
pamoja na zaka, (sio tu kulingana na kile kinachosemwa na sheria
lakini walijua kuhusu Abrahamu na Yakobo pia). Lakini pamoja na
kuyajua kwao hayo yote hatuoni mahali popote ambapo mitume
wanawatisha waumini kwa kuitumia mistari hiyo ya Agano la Kale
kwamba ETI watalaaniwa iwapo watakuwa hawatoi; wala hakuna popote
ambapo waliitwa ni waasi, kwa kutokutoa kwao kulingana na shinikizo
la matakwa ya mchungaji; wala hakuna mahali popote ambapo
wanatishiwa kufukuzwa kanisani eti, kwa sababu hawakutoa kulingana
na matarajio ya viongozi wao wa kanisa. Mistari ya neno la Mungu
katika Agano la Kale inatumiwa vibaya; na kisha watu wa Mungu
wanachezewa na kutumiwa vibaya na wachungaji pamoja na viongozi wao
wanaotafuta kuwanyonya washirika wao pesa zao kwa kujitafutia faida
yao wenyewe au kwa faida ya madhehebu yao. Wanachokifanya
wachungaji hao ni upinzani wa moja kwa moja wa neno la Mungu
tulilolinukuu hapo juu. Wachungaji na viongozi wa jinsi hii
wanajiweka wenyewe chini ya hukumu ya Mungu kwa kuwatendea dhambi
watu wake Mungu, kwa kuitumia vibaya misitari ya neno la Mungu kwa
faida zao.
Kama nilivyokwisha kusema, 2 Wakorintho ile sura ya 9, pamoja na
sura ya 8, ni sura za umuhimu kwetu kwa vile imejaza mafundisho ya
lazima yahusuyo kutoa. Katika ile sura ya 8 na ule mstari wa 7,
Mtume Paulo anawaambia Wakoritho, “Lakini kama mlivyo na wingi wa
mambo yote…basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia.” Paulo
anawatuia moyo ndugu waumini wa huko Korintho waige / wafuate mfano
wa waumini wa huko Makadonia katika kukusanya pesa kwa ajili
waumini masikini. Lakini sasa sikiliza kile akisemacho katika
mstari unaofuatia hapo (v.8),
“Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu
unyofu wa upendo wenu”
Mitume wa Bwana kwa MAKSUDI KABISA walijiepusha kuweka sheria
katika jambo hili la utoaji. Tutambue pia, Paulo aliita utoaji huu
‘neema’. Anawatia moyo wapate ‘wingi wa neema hii’! Sasa je? Vipi
unavyoweza kulazimisha ‘neema’? Katika kuelekeza kwao, hawatumii
maneno kama vile “kama usipotoa basi utalaaniwa na Mungu kutokana
na Malaki 3:9!”, au, “Kama usipotoa basi utatengwa na kanisa!”
Mitume wanakataa kuwaamuru waamuni kutoa. Hawawaambii kwamba ni
lazima kufuata ‘sheria’ fulani. Hataki kuwaagiza kuifuata sheria
iliyoandikwa kwenye mawe au kutoka katika kitabu - bali anawataka
wafuate upendo wa Mungu ambao umemwagwa kwa wingi ndani ya mioyo
yao kwa Roho Mtakatifu. (1 Yoh. 3:17). Anachokifanya ni kuwaonyesha
kuwa kile ambacho upendo wake Mungu ndani ya mioyo ya waumini wa
Mekodania ilivyowaongoza waumini hao kutenda! Na mitume nao
wanatamani kuona matunda hayo hayo ya upendo kutoka kwa wale
waumini wa huko Korintho!
Anaelezea ukweli huo pia kwa waumini walioko huko Filipi
wanaotuma pesa ili kumsaidia. Akiongelea kuhusu zawadi alizozipokea
kutoka kwa hao waumini wa huko Filipi, anasema, “Si kwamba
nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa
mengi, katika hesabu yenu.” Paulo anafurahia si tu kwa sababu
amepokea zawadi, lakini zaidi ya yote anafurahia kile
kinachowakilisha zawadi hiyo, ambacho ni tunda la upendo ndani ya
maisha ya waumini wale ambayo Mungu mwenyewe anayahesabia ni ya
thamani. Paulo anafurahishwa zaidi kuona kuwa waumini hao wanapaswa
kubarikiwa zaidi yake yeye mwenyewe. Na je, mwelekeo huu ni
mwelekeo wa wachungaji na viongozi wa siku hizi za leo? Na kama
tunataka kukua kiroho na kuwa na matunda katika maisha yetu, basi
ni wazi kabisa kuwa kutoa kwa moyo ulio huru ni ishara ya kukua
huko na tunda hilo.
Kwa hiyo kulingana na Agano Jipya, mambo ya ukweli uliokuwa
unaelekeza utoaji wao, ulikuwa kama ifuatavyo. Wakristo walitoa
“kadiri ya kufanikiwa kwao”, na “kulingana na uwezo wake alio nao”,
au hata “atoe kama anavyokusudia moyoni mwake.” (1 Wakor.16:2;
Matendo 11:29; 2 Wakor.9:7).
Agano Jipya halitoi maelekezo yoyote mengine kwa Wakristo
yanayohusiana na kiwango ambacho muumini anapaswa kukitoa katika
utoaji wao - mbali na mistari hiyo hakuna mistari mingine yoyote
inayowamuru kuhusu kikumi (asilimia kumi ya mapato yake).
Lakini si jambo zuri kupunguza kile unachokitoa kwa sababu ya
mambo haya, kwani Mungu anaona mioyo yetu na “humpenda yeye atoaye
kwa moyo mkunjufu”. Kwa sababu hiyo, mtume Paulo anatupatia onyo
moja linaloonekana ndani ya Agano Jipya, ambalo si kama ni onyo
lakini linaonekana ni kama ukiri wake wa kweli kwamba tunapaswa
kuchochea mioyo yetu katika utoaji. Jambo hilo ni hili,
“Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye
kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.” (2 Wakor.9:6).
Lakini tafadhali angalia vizuri sehemu hiyo; Paulo hatishi wala
hatengenezi sheria ili kuwasukuma waumini katika utoaji. Badala
yake YEYE anafunua ukweli wa kiroho ambao utatufanya sisi kufikiri
kuhusu hali ya mioyo yetu katika jambo hili. Ninaamini kuwa mstari
huu wa neno la Mungu unaonyesha kuwa iwapo mtu mmoja atachagua
kutoa ‘kidogo’ au ‘kwa uchache” (yaani, kichache kile alichotoa
kinalinganishwa na ukweli wa vile alivyo navyo), ndipo na wao
watavuna kwa uchache, si tu katika hali ya vitu, lakini ya kiroho,
kwani kile unachotoa kinawakilisha au kudhihirisha pia hali ya moyo
wako. Lakini hatuwi watu wa kiroho kwa kuyatazama na kuyafuata
mambo ya nje, kwa kufuata sheria. Matendo yetu ya nje yawe ni
mng’aro wa hali ya moyo. Utoaji wetu lazima utokane na mioyo yetu
kwamba umeguswa na kubadilishwa kwa upendo wa Mungu. Hii ndiyo
sababu hakuna hata mtume mmoja katika mafundisho yao anaweka sheria
katika mambo ya utoaji.
Makusudi yote ya Agano Jipya ni kwamba ili tuweze kuzaliwa mara
ya pili, na kupata upendo wake Mungu uliomwagwa ndani ya mioyo yetu
kwa Roho Mtakatifu - na kwa Roho wake Sheria za Mungu zimeandikwa
ndani ya mioyo yetu (Hebr 8:10). Kama vile ilivyo maisha yetu sasa
yaongozwe kwa nguvu ya Roho wa Kristo ndani yetu, na wala si kwa
kujaribu kutii sheria zilizoandikwa kwenye mawe, hivyo basi utoaji
wetu uongozwe na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu, sio kwa
kulazimishwa na sheria ya nje. Sisi ni watu tuliozaliwa mara ya
pili! Katika Kristo sisi tumefanyika kuwa ni viumbe vipya, mambo ya
kale yamepita na mambo yote yamekuwa mapya - na mambo yote ni ya
Mungu. Ni Agano Jipya ambalo ndani yake Mungu ametupatia moyo mpya
na Roho mpya (Ezek. 36:26) na maisha mapya, ambayo ni maisha yake
Kristo, ambayo ni maisha ya milele! Sasa tutarudije tena kwenye
mambo ya kale? Tutaishije tena kwa mambo ya kale (kutegemea Agano
la Kale).
Kama tumezaliwa toka juu kweli kweli, itakuwa tabia yetu
kuwasaidia watu wa Mungu – hasa washirika maskini - watumishi wa
Mungu na kazi ya Mungu. Tunapaswa kuongozwa na upendo na Roho ya
Mungu ndani ya mioyo yetu kadhalika katika utoaji wetu. Simaanishi
kuwa unapaswa kusubiri Roho akuambie cha kufanya kila wakati, bali
mioyo yetu iwe imebadilishwa haswa kwa Roho wa Mungu hadi kwamba
tunafurahia kusaidia watu wa Mungu na kazi ya Mungu.
Huwezi kutengeneza sheria kwa upendo! (Warumi 13:10).
Unaweza kufundisha, kuonya na kusihi, lakini kama utafanya
sheria ili watu waweze kuziishia hizo ndipo basi utakuwa unalipinga
Agano Jipya ambalo Kristo Yesu alimwaga damu yake na utakuwa
unarejea kwenye ukale. Hiyo sasa itawaongoza watu katika kutoa kwa
ulazima ambapo ni kinyume cha mambo yote tuliyoyasoma hadi sasa
katika Agano Jipya. Mengi ya yale aliyoyaandika Paulo kwa waumini
wa huko Galatia imeungana na pambano hili la vita kinyume na wale
wanaotaka kuwarudisha watu katika kutunza sheria mbalimbali za
Agano la Kale.
Katika Matendo sura ya 15, pale mitume wanapoyaandikia makanisa
kuwaonya kuhusiana na wale wanaodai kuwa washirika lazima waitunze
sehemu ya sheria ya Musa, hapo hapo mitume bado hawalitaji suala la
kikumi hata mara moja, kana kwamba ni jambo la lazima kwa mshirika
kutoa kikumi hicho wanapotoa maamuzi yao katika jambo kama hili.
Zaidi ya hiyo, jambo hilo halikuwa tu ni maamuzi yao, bali yalikuwa
ni maamuzi yaliyofanywa kwa maelekezo ya Roho Mtakatifu
(Mtd.15:28)
Hakuna mahala popote katika Agano Jipya ambapo panaagiza mambo
kama hayo au hata kushauri tu kwamba Wakristo wafuate mambo ya
kisheria katika mfumo wa kutoa kikumi. Wala hakuna mahala popote
katika Agano Jipa ambapo panaelezea kiasi gani cha mapato ya
mshirika au muumini anayopaswa kuyatenga ili kumtolea Mungu.
Mitume walisikiliza mafudisho ya Yesu, pia walijua yaliyoandikwa
katika Torati, lakini hawakufundisha juu ya ‘fungu la kumi’ au juu
ya ‘sheria ya utoaji’, wala hawakuwatisha waumini kwa laana! Kama
wao hawakutumia cheo wala mamlaka yao kama mitume wa Bwana Yesu
kuwatisha na kuwakamia watu wa Mungu lazima watoe zaka au fungu la
kumi vinginevyo watawalaaniwa na Mungu, je, wahubiri / wachungaji
hawa wanapata wapi na kutoka kwa nani mwongozo huu wa kutisha watu
wa Mungu kiasi hiki? Hawapati mamlaka wala ruhusa kutoka Biblia
wala kutoka kwa Mungu Mwenyewe bali wanajiinua juu ya neno la
Mungu, na wanawatenda dhambi washirika!
ANANIA NA SAFIRA
Lakini sasa niseme neno kidogo juu ya Anania na Safira. Watu
hawa hawakufa eti, kwa sababu walikataa kutoa kikumi (kama watu
wengi wavyoweza kufikiri), bali walikufa sababu walidanganya.
Waumini wengi tu walikuwa wakiuza ardhi na nyumba zao, na walileta
pesa zote kwa mitume. Wanapozileta pesa hizo kwa mitume hazikuwa
kama kikumi au nusu ya ya mapato ya mali zao, bali wao kwa hiari
yao walikuwa wakileta asilimia kwa mia ya mauzo yote ya ardhi na
nyumba zao! Anania na Safira waliuza ardhi yao kisha WAKAJIFANYA
ILI WAONEKANE kuwa wanaleta pesa zote za mauzo ya mali zao kwa
mitume. Sasa ilikuwa ni kwa sababu ya udanganyifu (uongo wao huo)
ndicho kilicho wasababishia kufa.
Ebu tusome mtume Petro alichosema kwa Anania, 'Anania mbona
shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu.
Ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla
hujauza hicho kiwanja SI KILIKUWA MALI YAKO? Hata baada ya kuuza
fedha ulizopata SI ZILIKUWA KWENYE UWEZA WAKO?” (Mtd 5:1-5). Kwanza
kabisa mtume Petro anamwambia Anania kuwa amemdanganya Roho
Mtakatifu, ndipo anamweleza kuwa hakukuwa na haja ya kudanganya
(kusema uongo), kwani uwanja uliouza ulikuwa ni mali yake.
Hawakuhitajika kuuza kiwanja hicho! Lakini hata baada ya kukiuza
bado pesa hizo zilikuwa ni mali yao; hawakulazimika kuzileta pesa
hizo kwa Petro. Unaona, haikuwepo sheria yoyote kuhusu jambo hili,
bali waumini walitoa vitu vyao kwa hiari na kutokana na pendo.
Anania na Safira walitenda dhambi kwa sababu wao WALITAKA KUIGIZA
WATU WENGINE lakini jumbe mioyoni mwao walikuwa na uchoyo, hivyo
walidanganya kuhusu kiasi halisi walichotoa. Uchoyo huu ndani ya
mioyo yao na udanganyifu (uongo) ndiyo ilikuwa dhambi yao. Mtume
Petro aliweka wazi kabisa kuwa hawakuwa chini ya sheria yoyote
katika kuuza ardhi yao na kisha kuleta pesa hizo kwake! Yote
yalikuwa jambo la hiari tu!
Kama wangekuwa hawajauza ardhi yao wasingeweza kuhukumiwa;
lakini pia kama wangeuza ardhi yao kisha wakasema kuwa wameuza
ardhi yao na wameleta nusu tu ya mauzo yao na kuyaleta kwa mitume
hapo pia wasingeweza kuhukumiwa.
Lakini sasa walidanganya; walitafuta waonekane kama wengine wao.
Ilikuwa ni kwa sababu ya udangaanaayifu huu na uwongo huu ndipo
walihukumiwa. Wachungaji au viongozi wanaotumia mistari hii ya neno
la Mungu ili kuwatishia watu katika kutoa wanalichafua neno la
Mungu kisha wanawatendea dhambi watu wa Mungu.
KUTOA PASIPO KUHESABU GHARAMA
Tunaona kwa waumini katika Agano Jipya pengine utoaji hauna
mipaka!
“Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu
vyote shirika, WAKIUZA MALI ZAO, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na
kuwagawia watu wote kama KILA MTU ALIVYOKUWA NA HAJA.” (Matendo
2:44,45).
“…wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, WAKALETA
THAMANI YA VITU VILIVYOUZWA, wakaiweka miguuni kwa wale mitume,
kila mtu akagawiwa KADIRI YA MAHITAJI YAKE.” (Matendo 4:34,35).
Unaona? Wengi wa waumini wa Yerusalemu waliuza mashamba na
nyumba zao, nao walileta thamani kamili ya vitu walivyouza -
walitoa 100%, siyo fungu la kumi. Jambo kama hilo halikutokea kabla
yake. Kulitokea nini hata kusababisha watu wa Mungu kutoa kwa jinsi
hiyo pasipo sheria yoyote iliyotolewa kwao? Kilichotokea hapo ni
lile Agano Jipya. Siku ile ya Pentecoste wanafunzi walibatizwa
katika Roho Mtakatifu, na wakauza mali zao kwa hiari yao kabisa kwa
sababu ya pendo la Mungu ambalo lilikuwa limemiminwa ndani ya mioyo
yao na Roho Mtakatifu. (Hii haimaanishi kuwa tunapokuwa tumekwisha
batizwa katika Roho Mtakatifu basi tunapaswa sasa kuuza nyumba
zetu. Hii sio sheria ya kuifuata, bali ni maelekezo kuonyesha kuwa
nini kinatokea wakati watu wanapokuwa wamejazwa na Roho wa Mungu.
Katika Matendo ya Mitume hatusomi popote juu ya kutokewa na mambo
kama hayo baadaye tena katika miji mingine ambako Injili ilikuwa
ikihubiriwa. Hebu niongeze hapa kuwa ninaamini kuwa watakatifu
waliokuwepo Yerusalem kwa ujumla waliuza nyumba na ardhi ilikuwa ni
zidio la yale wanayoyahitaji katika matumizi yao ya kila siku.)
Pendo halifanyi kazi yake kutokana na sheria za Agano la
Kale.
Pendo halitambui wala halina mipaka! Hilo ndilo Agano Jipya!
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa
Mwanawe pekee…” (Yoh.3:16).
Bwana apewe sifa! Kwa hiyo imeandikwa ‘Pendo ndilo utimilifu wa
sharia.’ (Warumi 13:10). Kutoa ni hiari, ni tendo la hiari la
upendo na kuabudu ambalo linavuka utii wa sheria ya nje. Halitokani
na madaraka au wajibu. Halihesabu. Ni tendo la mwitikio la mara
moja la yeye anayempenda Mungu na anayetaka kuona jina lake Mungu
likitukuzwa hapa duniani na watu wake wakibarikiwa.
Kazi au matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu ni kwamba
tutoe kwa hiari kwa sababu ya upendo wa Mungu mioyoni mwetu. Onyo
ni mmoja tu katika Agano Jipya, yaani, “Ye yote apandaye kwa
uchache pia atavuna kwa uchache…”. Katika Agano Jipya tunafundishwa
kwamba, “Kusudi (au mwisho) la maagizo (sheria) haya ni upendo,
utokao katika moyo safi,…” (1 Tim.1:5). Kama Wakristo tunapaswa
kutoa kutokana na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu kwa hiari,
kwa furaha, siyo kwa sababu ni lazima nishike maagizo yaliyopo nje
yangu au kuepuka laana! Kama upendo wa Mungu upo ndani ya moyo
wangu utoaji ni jambo la kawaida kwangu! Lakini hiyo haimaanishi
kwamba hatuwezi kuwahamazisha watu kwa mafundisho watoe kadiri ya
upendo wa Mungu, kama vile tunavyofanya juu ya mambo mengine, na
kama vile Paulo anavyofanya. Lakini kama ukitaka kuwafundisha
waumini lazima watoe zaka au fungu la kumi sawasawa na Torati
(Toarati inazingatia vitabu vitano vya kwanza ya Agano la Kale),
lazima utuonyeshe angalau hata mstari mmoja katika Agano Jipya
ambapo waumini wanafundishwa na Mitume kufanya hivyo! Lakini
haupo!
Kama tumezaliwa toka juu kweli kweli, kama tumebatizwa na Roho
Mtakatifu, itakuwa TABIA YETU kuwasaidia watu wa Mungu, watumishi
wa Mungu na kazi ya Mungu!
Hata hivyo, hata kwa wale walioishi bado chini ya sheria ya
Musa, pendo kwa Mungu na kwa kazi Yake mioyoni mwao halikutambua
mipaka! Tunasoma,
“Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi
mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia
mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili,
kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin,
nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia
katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa
navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” (Marko 12:41-44).
Kwa mujibu wa maneno ya Yesu, thamani ya sadaka mbele ya Mungu
inategemea SIYO na thamani yake kwake anayeipokea, BALI na thamani
yake kwake anayetoa ile sadaka! “Huyu mjane maskini ametia zaidi
kuliko wote.”
Tumeiangalia mistari ya neno la Mungu ambayo imetujulisha kuwa
waumini walimtolea Mungu kulingana na uwezo waliokuwa nao,
kulingana na jinsi Mungu alivyowabarikia, na pia kulingana na kila
mmoja wao alivyoamua kataika moyo wake. Hivyo basi kutokana na
mistari hiyo tunatambua kuwa hakuna asilimia yoyote ya matoleo
iliyotajwa. Na waumini wangeweza kumtolea Mungu zaidi hata ya hicho
kikumi. Lakini tena, hizo sio kanuni iliyowekwa na Agano Jipya -
hayo ni maelekezo yanayoonyesha nini kilitokea na ni miongozo
ambayo Wakristo wanaagizwa katika mambo yahusuyo kutoa.
-------------------------------
Sheria ilitolewa na Musa lakini kweli na neema imekuja kupitia
Kristo Yesu. Katika Agano Jipya, kama nilivyosema, mambo
yamebadilika! Sisi si mali yetu wenyewe, tumenunuliwa kwa gharama
yenye thamani kubwa (1Wakor. 6:19,20). Kwa hiyo, hatupaswi kuishi
maisha yetu wenyewe isipokuwa tuishi maisha kwake Yeye aliyetufilia
(2 Wakor.5:15). Kutokana na hayo tunatambua kwamba sio tu sisi
wenyewe, bali vyote tulivyo navyo na tunavyo vimiliki ni vya Bwana.
Yesu mwenyewe aliwafundisha watu katika Luka 12:32,
“Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko
isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia
mwivi, wala nondo haharibu.”
Yesu Kristo anadai maisha yetu yote - jinsi tulivyo na vyote
tulivyo navyo. Tumeona matokeo ya kujazwa na ujio Roho Mtakatifu
katika Matendo ya Mitume, ile sura ya 2 na ya 4, mahali ambapo
baadhi ya waumini waliuza nyumba zao na mali zao ili kuwasaidia
waumini walio masikini. Mambo ya asilimia kumi au kikumi ilikuwa
haipo. (Narudia tena, haitupasi kuuza nyumba zetu ili kwamba
tujikute hatuna mahala pa kuishi na tunaishia kurandaranda mitaani
pamoja na familia zetu!)
Lakini pia kuna mifano mingine inayoonyesha utoaji wenye uwingi
mkubwa katika Agano Jipya kama tulivyokwisha kuonyesha hapo juu,
kuwa upendo hautambui/hauna mipaka, wala upendo hauzuiliwi na
sheria kama tunavyoweza kurudi kusoma katika 2 Wakorintho,
“…maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa
furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa
ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya
uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana
pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la
kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini
tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa
mapenzi ya Mungu. (2 Wakor.8:2-5).
Hii ni mistari mizuri ajabu! Waumini hao walikuwa ni maskini na
walikuwa wakipitia njia ya ugumu na mateso kwa maisha yao. Hata
hivyo, pasipokujali ugumu wa maisha yao wao wenyewe, waumini hao
walikuwa na moyo uliotamani kutoa na kutoa kwa utoshelevu mkubwa
kabisa! Kwa hiyo kwanza, walijitoa wao wenyewe kwa Bwana na bila
shaka wakikiri kuwa wao wenyewe na vyote walivyokuwa navyo ni mali
yake Bwana. Kutokana na upendo huu wa Mungu walikuwa walihiari
kumtolea Mungu zaidi na kuzidi. Hivyo ndivyo upendo wa Mungu katika
mioyo yetu unavyoweza kutuongoza!
Unapojisomea mistari hii, je, unapata hisia kuwa watakatifu hao
walitoa pesa zao ili kwamba waje kupata pesa zaidi baadaye? Je,
unafikiri kuwa labda mioyoni mwao walifikiri kuwa, “tukipanda kwa
uhaba basi tutavuna haba - basi ebu tutoe pesa ili tuweze
kubarikiwa kwa kupata pesa nyingi zaidi? Hapana! Mawazo kama hayo
hayakuwemo katika mioyo yao kabisa, kwa sababu huo ungekuwa ni
uchoyo na kubadilisha utoaji kuwa ni mfumo wa kibiashara. Na kwa
sababu ya upendo wake Mungu ndani ya mioyo yao walikuwa wanashauku
kubwa ya kuwasaidia ndugu waliokuwa waahitaji - pasipo hata
kufikiria chochote kile au hata bila aya kujitafutia faida yoyote
ile. Walijitoa katika utoaji wao. Tufuate mfano wao! Yeye apandaye
kwa uhaba anavuna kwa uhaba. Huo ni ukweli wa kiroho ambao unapaswa
kuyachonga maisha yetu. Lakini hiyo sio sababu inayompelekea mtu
kutoa. Usijaribu kutoa ili kuja kupokea, huo ni uchoyo na sio
upendo; hiyo ni biashara na sio kujitoa. Nitagusia jambo hili muda
mchache unaofuatia.
Nilionyesha hapo juu kuwa kulikuwa na aina nyingi sana za utoaji
katika Agano la Kale. Na hii ni kweli kwa mujibu wa mistari ya neno
la Mungu. Kulingana na mistari ifuatayo inaonyesha kuwa kulikuwa na
kikumi kwa Walawi (Hesabu 18:21,24); kulikuwa pia na kikumi kwa
ajili ya karamu na sherehe (Kumb. 14:22-27). Na kisha kulikuwepo na
kikumi kwa ajili ya Walawi na watu masikini kila mwaka wa tatu
(Kumb.14:28-29). Matoleo hayo yote yangepaswa kupanda zaidi hata ya
kikumi ya kile kilichotolewa. Zaidi ya hayo, tunao pia mfano wa
matoleo ya hiari, ambayo wana wa Israel waliyatoa kwa hiari yao na
kwa utoshelevu mkubwa. Basi tunasoma katika kitabu cha Kutoka kuwa
wito ulipotolewa kwa wana wa Israeli ili kuchangia ujenzi wa hekalu
la Mungu,
“Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye
roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa
Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, … Wana wa Israeli wakaleta
sadaka za kumpa Bwana kwa hiari; wote, waume kwa wake, ambao mioyo
yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, … nao wakasema na
Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo
vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana
aliagiza ifanywe.” (Kutoka 35:21; 35:29; 36:5).
Ni jambo la kushangaza kwamba waandishi wengi wanalinganisha
utoaji wa sheria katika mlima wa Sinai na siku ile ya Pentekoste,
na kama tunavyosoma katika kitabu cha Matendo 2, hapa pia
tunakutana na furaha ya utoaji wenye utoshelevu usio na mipaka,
hata kwamba mwisho wa utoaji wao kulipatikana matoleo mengi
zaidi.
Naitaja mifano hii si kwa ajili ya kutengenea sheria kwa ajili
yetu. Hapana, bali ni kutaka kuonyesha kuwa hata nyakati za Agano
la Kale utoaji haukuwekewa mipaka kwa asilimia kumi tu; hakukuwepo
na utoaji wa kulazimu tu, bali kulikuwepo pia na utoaji wa hiari
kama huo nilioutaja hapo juu. Kadhalika huo utoaji wa hiari
Waisrael waliweza kuleta wakati wowote (Walawi 1:3). Nayataja mambo
haya ili kuonyesha kuwa hata katika nyakati za Agano la Kale
kulikuwepo na wazo la kutoa pasipo mipaka. Je, hiyo haipaswi kuwa
ni kweli kwetu sisi katika Agano hili Jipya ambapo upendo wake
Mungu umemiminwa katika mioyo yetu kwa Roho Mtakatifu?
Mtu yeyote asemaye kuwa makala haya yatapunguza kipato cha
kanisa, au kitawafanya watu wasitoe au kupunguza kile wanachokitoa
kwa sababu mimi ninaonyesha wazi kuwa utoaji hauna sheria, wala
mipaka kuhusiana na mifumo ya utoaji katika Agano Jipya, basi mtu
huyo hajaelewa chochote katika yote niliyoyaandika katika makala
hii.
NENO ‘KIKUMI’ AU ‘ZAKA’ KATIKA AGANO JIPYA
Ni muhimu pia kugundua kuwa neno ‘ZAKA’ (‘kikumi’ - asilimia
kumi) haijatajwa kwa mujibu wa kanisa lake Mungu. Imetamkwa katika
muktadha 3 katika Agano Jipya - mara mbili kuhusika na mafarisayo
(Luka 18:12; 11:42); na mara moja tu katika kitabu cha Waebrania 7,
ambapo inaelekeza mahala ambapo Ibrahimu alimtolea Melkizedeki na
kile kilichokuwa kinatolewa na kabila la Walawi (Nitaongea juu ya
jambo hili baadaye kidogo kadiri tunavyoendelea na makala hii).
Lakini hii ndiyo kumbukumbu za mwandishi kwa nyakati zilizopita
kuonyesha kuwa Melkizedeki (Yesu) alikuwa ni mkuu kuliko Ibrahimu.
Mistari hiyo hapo haimfundishi Mkristo chochote kile kuhusu kutoa
kikumi leo!
Hebu pia iwekwe wazi kuwa katika nyaraka za mitume kwa makanisa,
sio tu kwamba hakuna popote panapotajwa juu ya kikumi, lakini zaidi
ya hilo hakuna pia popote pale panapotaja utofauti wa matoleo kama
vile kikumi, zaka na dhabihu, au matoleo ya mwaka mpya, tunda la
kwanza na mambo mengine mengine mengi yanayokuzwa na wahubiri na
‘manabii’ wa leo katika makanisa. Watu wengine wanapenda kuleta
mawazo ya Agano la Kale yahusuyo kutoa katika kanisa la Kristo leo.
Pia wanapenda kuelezea namna mbalimbali ya matoleo na utofauti wa
aina zake na kisha kuyawekea kanuni katika kanisa.
Mambu hayo yote ujue kuwa yapo kinyume kabisa na fundisho la
Agano Jipya, ni kinyume pia na fundisho la Mitume wa Yesu, na zaidi
ya yote ni kinyume na maelekezo ya Roho Mtakatifu ndani ya mioyo ya
wote wanaolazimishwa kutoa kwa jinsi hii. Mitume hawakuweka jambo
kama hilo katika mafundisho yao, na jambo lingine linalolingana na
hayo tunasoma juu ya watu wafanyao mambo ya aina hiyo katika 1
Timotheo 1:6,7:
“Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili; wapenda
kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo
yale wayanenayo kwa uthabiti.”
Iwapo kama inakupendeza wewe kuufanya huu utofauti, na kisha
ukaongozwa na mfumo wa aina hiyo ya utoaji, basi fanya hivyo wewe
mwenyewe kwa usiri wa nafsi yako tu, lakini usiwapeleke watu wa
Mungu katika vifungo vya utoaji wa jinsi hiyo kwa kuwafanyia sheria
wengine! Pia, kama wewe unapenda kuishi katika mifumo ya Agano la
Kale huo ni uchaguzi wako, lakini katika Agano Jipya Wakristo wao
hutoa tu kwa Mungu wao na wakati mwingine hutoa hata asilimia
miamoja. Na matoleo yao yote yanakusudiwa kuwa ni “harufu ya
manukato, sadaka yenye kibali impendezayo Mungu.” (Wafilipi
4:18).
TATIZO LA FUNGU LA KUMI LENYEWE
Tatizo moja kubwa au hatari yakufuata sheria katika mambo
yahusuyo kutoa fungu la kumi ni kwamba, unapokuwa umekwisha kulitoa
fungu la kumi hilo, utaweza kuamini kuwa umefanya kilicho sawa,
kile kinachohitajika. Unafikiri kwamba jukumu lako la kutoa sasa
limekwisha kwa wiki ile au kwa mwezi ule! Hapo ndipo hasa ni mahala
au ni fikra ambayo sheria inakuingiza uwazie, kwa sababu wewe sasa
unafanya utoaji ule kana kwamba ni jukumu ulilopewa ulifanye au
kazi fulani ili kutimiliza sheria. Utoaji sasa unageuka kuwa ndio
jukumu la kidini badala ya kuwa ni tendo la uhuru na upendo tu! Kwa
hiyo hatari kubwa hapo ni kwamba utakuwa unajisikia ni mwenye haki,
au upo sawa mbele za Mungu kwa sababu tayari unajiona kuwa
umekwisha timiza (unalofikiri ni) ‘wajibu’ wako wa kutoa fungu la
kumi wiki au mwezi ule! Tukumbuke onyo la Bwana Yesu tusianguke
katika fikra za Mafarisayo ambaye alisema moyoni mwake, “Ee Mungu,
nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi,
wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara
mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” (Luka
18:12).
Ni vilevile kama ilivyotokea kwa waumini wa kanisa la Galatia,
ambao wao waliamini kuwa wanapaswa kutimiza aina fulani fulani za
sherehe za Agano la Kale kushika sabato, kutahiriwa ili kwamba wawe
na haki mbele za Mungu! Mtume Paulo anawaonya kwa nguvu sana dhidi
ya ya mawazo kama hayo. Tatizo lingine kubwa na hatari zake ni kuwa
kama wewe unaamini katika mambo ya kutoa hilo fungu la kumi, basi
itaweza kukuwekea mipaka juu ya upendo wa Mungu na katika utendaji
kazi wa Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako, kuhusiana na jambo hili
la kutoa zaidi ya kikumi kila mwezi. Hakuna mahala popote katika
Agano Jipya panapoelezea kuwa Waakristo tutakuwa tumetimiza wajibu
wetu pale tutakapokuwa tumetoa kikumi kanisani kila mwezi.
MSAADA KWA WACHUNGAJI
Hebu sasa, tuone maandiko katika Agano Jipya yanasemaje kuhusu
utoaji au msaada wa wachungaji na watumishi wengineo. Ipo sehemu
moja tu katika Agano Jipya inayojishughulisha na jambo kama hili
mjoa kwa moja, yaani, 1 Timotheo 5:17,18:
“Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu;
hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko
lasema, ‘Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka’. Na tena, ‘Mtenda
kazi astahili ujira wake.’” (Kwa lugha ya Kigiriki neno ‘wazee’ na
sawa na ‘wachungaji’.)
Maana ya maneno hayo hapo ni wazi kabisa; ikiwa mchungaji hana
kazi nyingine (yaani, hana mapato mengine) kwa sababu mtu huyu
anafuata mwito wake kwa kuwalisha washirika na neno la Mungu, basi
ni jambo la haki na ni la upendo washirika watambue kujitoa kwa
mchungaji wao huyo mzuri kwa ajili ya kanisa la Bwana na hivyo
kumsaidia na riziki zake, sawasawa na mahitaji yake. Ni jambo la
maana sana kwa somo hili tutambue lugha ya mtume. Hapo hataji
‘fungu la kumi’ wala hafundishi kwamba makusanyo yote ya jumapili
lazima yawe mali ya mchungi kama vile ilivyofanyika kwa walawi na
makuhani walivyopata fungu la kumi sawasawa na sheria ya Kumbukumbu
sura 18 na Hesabu 20:20,21. Hapana, hafundishi hivyo! Paulo
ananukulu maneno ya Yesu (Luka 10:7) na sheria ya Torati la Musa
juu ya ng’ombe (Kumbu.25:4), kwamba yule ng’ombe anayefanya kazi
kwa ajili yako lazima umhurumie na kumruhusu kula. Kwa hiyo, Paulo
anasema tunapaswa tutambue kazi nzuri ya mchungaji kwa ajili yako
na kumhurumia na kumheshimu kwa ajili ya kazi hiyo aliyoifanya kwa
ajili ya watu wa Mungu. Lakini utoaji huo haupaswi kutumika ili
kumtajirisha mchungaji au mtume au mtumishi yoyote; au utoaji huo
usimfanye mchungaji aonekane kuwa ni tajiri kuliko makutano
anayoyahudumia.
Na pia jambo la kuzingatia hapa ni kwamba utoaji huo uwe ni wa
hiari kutoka moyoni mwa mtu, yaani, tunaona kutokana na maneno ya
Paulo yeye haweki sheria wala hatoi mfumo wa rasmi wa kuwasaidia
wachungaji, ila anawakumbusha waumini juu ya daraka lao ya haki na
ya upendo. Nilisema utoaji hautokani na sheria fulani ila uwe ni wa
hiari na siyo ‘kwa kulazimishwa’, lakini tena hayo hayamaanishi
tuwe wavivu katika jambo hili. Katika mambo yote haki na upendo
ndio unaopaswa kutuongoza sisi, na sio sheria na hii ndiyo sababu
inayowafanya mitume wasite kuweka kanuni – badala yake
wanatukumbusha, anatusihi, anatutia moyo kufuata mambo ya haki.
Mafundisho hayo ya Paulo (1 Tim.5) tunayapatia pia 1
Wathesalonike 5:12,13:
“Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa
ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni;
mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao.”
Sehemu hii mtume Paulo hataji chochote juu ya msaada kwa ajili
ya watumishi wa Mungu lakini naamini kuwa lile neno ‘muwatambue’ na
‘mkawastahi sana’ pamoja na lile alilolisema katika 1 Timotheo 5
linatuongoza tuweze kufahamu hivyo.
Nimesema kuwa tunapaswa kuongozwa na upendo, huruma na haki
katika utoaji wetu. Hivyo basi ebu nitoe mifano michache ili
kukionyesha kile ninachomaanisha hapa. Kwa mfano, nawafahamu baadhi
ya wachungaji katika vijiji fulani ambako washirika wao ni
masikini, na makusanyo ya sadaka zao za jumapili zinaweza kufikia
kati ya sh. 2000 hadi 5000. Kiwango hiki cha pesa sio kikubwa sana.
Ingewezekana katika hali kama hiyo, basi washirika wangesema kuwa
Mchungaji, “Shiling elfu tano si kiasi kikubwa sana, tafadhali
chukua hizi shilingi elfu tano kwa ajili ya matumizi ya familia
yako pale nyumbani.” Kwa hiyo katika hali kama hii washirika hao
wangechagua kumpa mchungaji wao makusanyo hayo yote ya sadaka ya
siku hiyo ya jumapili. Hili sasa ni jambo la huruma na upendo na
haki pia. Amina!
Nilipokuwa nahudumu kama mchungaji mshiriki katika kanisa,
hakuna makusanyo yoyote ya sadaka za jumapili nilizokuwa napewa
mimi, wala hata kwa wale wachungaji wenzangu wawili tuliokuwa
tukihudumu pamoja. Makusanyo hayo ya pesa yalikuwa yanatumika kwa
ajili ya kulipia gharama za uendeshaji wa kanisa hili kama vile
umeme n.k. Lakini nyingi ya pesa hizo zilikuwa zinatolewa kusaidia
kazi ya Mungu kwa baadhi ya maeneo katika nchi ile pia hata nje ya
nchi ile. Lakini ilikuwa inatokea iwapo mshirika yeyote alipenda
kunipa mimi, au hata yoyote kati ya wachungaji wenzangu tuliokuwa
tukitumika pamoja, basi kulikuwa na sanduku limewekwa kanisani humo
ambamo mtu huyo angeweka pesa hizo ndani ya kijisanduku kile.
Wangeweka pesa hizo katika bahasha na juu ya bahasha ile
wangeandika jina la mchungaji yule wanayependa kumsaidia. Lakini
hauweki jina lako wewe unayetoa pesa hizo juu bahasha yako, kwa
kuwa tunaamini kuwa si sawa kwa mchungaji kuelewa ni nani
anayempatia pesa hizo. Huo ulikuwa ni wakati wangu mzuri kabisa
katika maisha yangu kwa sababu nilikuwa ninamtegemea Mungu - naye
alikuwa mwaminifu kwangu. Sikuwa na pesa nyingi katika familia
yangu, lakini nilipata amani na furaha kubwa katika moyo wangu kwa
sababu niliamini Mungu ameniita mimi kwa jambo hili na moyoni
mwangu nilipata utoshelevu kumwekea yeye Mungu matumaini yangu. Hii
(yaani, viongozi wa kanisa kusaidiwa na utoaji wa hiari na
kujitolea wa washirika wale) inaonekana ilikuwa ni hali ya kanisa
la Agano Jipya pia kama tulivyouona Mtume Paulo alivyo kuwa
akiwasihi kama nilivyo nukuu hapo juu.
Au, washirika wa makanisa makubwa ya mijini wanaweza kuamua
kumsaidia mchungaji wao kwa kutenga pesa kiasi ya sadaka
zinazokusanywa siku ya jumapili ili zimfae kwa mahitaji yake pamoja
na familia yake. Hicho ndicho kinachofanyika kwa makanisa mengi
ulimwenguni kote. Kwa upande mmoja hii inamfanya mchungaji awe na
uhakika wa kipato kusaidia familia yake katika mahitaji ya lazima,
lakini kwa upande mwingine inaweza kuonekana kana kwamba mchungaji
huyo anaifanya huduma hiyo ni ajira. Wengi wanaona uhakika huu wa
kipaato ni mzuri na ni jambo la haki, lakini mimi sina uhakika kama
tunaweza kuifanya huduma ya kichungaji ionekane kama vile ni kazi
zingine za ajira - kama afisa mifugo, kilimo, menega, n.k. Ila hilo
ni wazo langu tu.
Hata hivyo, Biblia haitoi haki au ruhusa ya mtu fulani
kuyachukua makusanyo yote yanayofanyika jumapili eti yawe ni yake.
Hapana! Inapotokea mtumishi yoyote anadai pesa za sadaka jumapili
kuwa ni haki yake kuzichukua, basi mtu huyo anafanya biashara zake
mahala hapo, anafanya biashara na kuwanyonya watu wa Mungu. Hii ni
dhambi kubwa sana. Hakuna fundisho lolote katika makanisa ya Agano
Jjipya linaloelekeza hivyo wala hatuoni mfano wowote wa aina hiyo.
Punde tu nitakwenda kuonyesha jinsi baadhi ya wachungaji na
makanisa wanavyowatendea vibaya na kuwaharibu washirika wao katika
jambo hili la utoaji.
MSAADA KWA WENGINE WAFUNDISHAO NA KUHUBIRI INJILI
Sasa nataka kurudi na kuangalia juu ya mistari inayoelezea juu
ya kuwasaidia wale waliomo katika huduma. Msaada huu hauhusu
wachungaji wa kanisa tu bali pia na kwa wengineo. Tunaona kuwa
mtume Paulo anafundisha kuwa utoaji unaotelewa na washirika unaweza
kumhusu mtumishi wa Bwana yeyote yule anayejitaabisha kwa ajili ya
watu wa Mungu na kazi yake. Na ukweli huu tunauona katika mistari
mingine ya neno la Mungu. Mtume Paulo aliwashukuru waumini wa
Filipi kwa msaada wao. Yeye anaandika.
“Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha
tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri
hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa
nina mahitaji…Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki
yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa
katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa
lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na
kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike
mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba
nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa
mengi, katika hesabu yenu.” (Wafilipi 4:10-17).
Mtume Paulo anawaeleza Wafilipi kuwa walifanya vema kumsaidia
katika shida zake. Kwa ukweli kutokana na mstari huu tunauona
ukweli kuwa ni jambo la upendo na la haki kuwa tunapaswa kuwasaidia
wale wanaoteseka na kupungukiwa kwa sababu ya ile kazi ya Mungu
wanayoifanya kwa niaba yetu. Na mtume Paulo anafurahia kwa sababu
anayaona matoleo wanayompelekea au zawadi zile kama ishara ya kukua
kwao katika upendo katika Kristo. Na huwezi kulazimisha kukua kwao.
Kukua ni matokeo ya uchaguzi tunaoufanya sisi wenyewe kwa hiari
mbele ya Mungu! Kutokana na mistari hiyo hapo juu, tunaona Wafilipi
walichagua wenyewe kwa hiari yao kumsaidia Paulo kwa ajili ya kazi
yake kwa ajili yao na kwa ajili ya Injili. Na utoaji huo ulitokana
na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yao - wala hamna aliyewalazimisha
kufanya hivyo! Pia lilikuwa ni kanisa la Filipi tu ndilo
lililomsaidia Paulo kwa jinsi hiyo. Lakini Paulo mwenyewe
hakulalaminika, badala yake Paulo anaeleza kuwa yeye hakutamani
kile kipawa, bali alifurahi kwa ajili yao kwa sababu kipawa kile ni
dalili ya pendo la Mungu mioyoni mwao na Paulo anafurahia kuyaona
matunda haya ndani yao.
“Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele;
nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu,
harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.”
(mstari 18).
Wakorintho wa kwanza sura ya 9 ni sura nyingine tena ya Biblia
ambayo ni muhimu sana katika mafunzo yetu haya. Katika eneo hili
mtume Paulo anaeleza kwa ukamilifu kabisa ule ukweli anaougusa
anapowaandikia Wafilipi 4. Paulo hakuomba msaada wala fedha
anapowandikia Wakorintho. Yeye anasema alifanya kazi kwa mikono
yake ili apate kuihubiri Injili kwa uhuru zaidi kwao. (Soma Matendo
20:34; 1 Wakor.4:12; 1 Wathess.2:9; 2 Wathess.3:8). Wengi wa
Wakorintho hawakuelewa na jambo hili! Lakini alikazia kuwaeleza
kuwa yeye kama mtume alitegemea kuwa angeweza kupata msaada wa
fedha kutoka kwao kama ilivyo kwa mitume wengine kama Petro ambao
walipata msaada huo (1Wakor 9:1-18). Anawaelezea kwa ufasaha na
uwazi kabisa juu ya msingi ya haki ambayo ingemfanya aweze kupata
msaada wao kwa kutoa mifano mingi,
“Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake
mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake?
Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?”
(m.7).
Kwa kutoa mifano hiyo, hapo anaweka mambo uwazi zaidi kwamba
wale walioingia katika kazi ya Mungu wanapaswa kupata msaada wa
msingi wa mahitaji yao kwa kazi ile waifanyayo. Kwa maneno mengine,
yeye ahubiriye kwa muda wote kikamilifu anapaswa kupokea msaada ili
kukidhi mahitaji yake ya maisha ya kila siku kutoka kwa wale
anaowatumikia. Na baada ya hapo ananukulu kutoka katika Agano la
Kale. Je, hapo ananukuu kuhusu sheria ya fungu la kumi kwa ajili ya
makuhani? Hapana! Anataja ng'ombe tena; ananukulu, “kwa maana
katika torati ya Musa imeandikwa usimfunge kinywa ng'ombe apurapo
nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini
ananena hayo kwa ajili yetu. Naam yaliandikwa kwa ajili yetu.”
(m.9,10). Anaendelea kusema, “Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu
vya rohoni, je! ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?”
(m.11). Ndipo anathibitisha hayo yote kwa kusema, “Hamjui ya kuwa
wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na
wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya
madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio
Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.” (m.13,14).
Katika mfano huo wa mwisho, mtume Paulo anaelezea tu ukweli ule
ule kwa kutumia mfano mwingine kupitia katika Agano la Kale. Huo
mfano wa mwisho Paulo hanukulu mstari moja kwa moja kutoka katika
Agano la Kale lakini anadhihirisha ukweli kwamba kama vile wale
wazifanyao kazi za hekaluni walikula katika vitu vya hekalu
(tunasoma hayo katika Kumbu.18:3), vivyo hivyo wale waihubirio
Injili wanavyopata riziki kwa hiyo Injili. Hebu sasa tugundue
kupitia mstari huo hapo kuwa mtume Paulo hatamki au hataji chochote
kile kuhusu kutoa kikumi! Angeweza kufanya hivyo kwa urahisi tu kwa
kulinganisha kuwa kama vile Walawi na Makuhani walivyopokea kikumi
toka kwa Wasraeli, basi vivyo hivyo na wachungaji na wahubiri
wanahusika na kupokea kikumi toka kwa waumini wao! Mtume Paulo
angeweza kuagiza hapo juu neno hilo kwa uwazi kabisa! Lakini
hakufanya hivyo. Hakufanya hivyo kwa sababu jambo kama hilo (yaani,
kuwapa wachungaji fungu la kumi kila wiki/mwezi) halipo kwa
matumizi ya Agano Jipya, na wala halimo katika mpango wa Mungu kwa
watu wake katika Agano Jipya. Badala yake, mtume anachagua
kututolea mfano ambao unatukumbusha kwamba makuhani katika Agano la
Kale sawasawa na agizo la Mungu waliweza kula sehemu ya dhabihu
zilizotolewa na Waisraeli, lakini agizo hili halihusu jambo la
kikumi – lilkuwa agizo tofauti kabisa! Labda pia ni la maana kwamba
hapo anaepuka kutumia neno ‘makuhani’ - anasema ‘wale wazifanyao
kazi za hekaluni’. Labda alifanya hivi kwa kusudi kwa sababu katika
Agano Jipya sisi sote ni makuhani (1Petro 2:5,9).
Nafikiri watumishi wa Mungu mahala pote katika ulimwengu huu wa
Biblia wangekaa kimya na kuwaza au hata kutafakari kwa nini jambo
kubwa kama hili katika maisha yetu kwa Agano Jipya lipo kimya,
ambalo jambo hilo hilo lileta heshima kwa makuhani, kwa Ibrahmu
baba yetu mbele ya Melkizedeki. Leo Mungu mwenyewe awe kimya,
Biblia iwe kimya, Yesu awe kimya, mitume wawe kimya na wala Agano
lenyewe tunalo litumikia sisi, yaani, Agano Jipya lisiseme chochote
juu yake? Ni kwa sababu ya mfumo wa Mungu wa pendo lake kwa wakazi
wanaolitumikia Agano Jipya ametuondolea kongwa la utumwa, kongwa la
Sheria, na makali ya maumivu yalaiyokuwemo ndani ya amatoleo hayo
ya kusukumwa. Atupatia njia nyingine “apenda wanaomtolea kwa moyo
wa hiari.”
Mifano hiyo yote inathibitisha ukweli mmoja ambao tayari
tumekwisha kugundua, ya kwamba ni jambo la haki na la huruma kwa
wao wapatao faida za kiroho kupitia huduma ya wale walioacha kazi
ili kumtumikia Mungu waweze kusaidiwa riziki zao na mahitaji yao.
Lakini kwa upande wa mitume na wahubiri hatuna mfano hata mmoja
katika maandiko ambao wanawalazimisha washirika waape pesa, wala
hakuna mfano hata mmoja unaowalazimisha waumini kutoa pesa kwa
mitume, au wachungaji kama wafanyavyo mitume na wachungaji wa leo.
Aina ya mtu mmoja aliwalazimisha washirika kutoa pesa - yaani,
“mitume wa uongo watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa
mitume wa Kristo. Wala si ajabu maana shetani mwenyewe hujigeuza,
awe mfano wa malaika a nuru.” (2 Wakor.11:13,14). Lakini kwa kiasi
Wakorintho walifurahia mitume wa uongo kama hao kwani Paulo anasema
juu yao, “Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza,
akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.” (m.20).
Lakini ingawa mtume Paulo angaliweza kutazamia waumini wa huko
Korintho kumsaidia na riziki zake aliikataa haki yake hiyo, na
akafanya yote kwa ajili ya faida ya watu aliowapenda. Hapa
anatangaza, “Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo
yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo…. Lakini mimi
sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo
kwangu mimi.” (1 Wakor.9:12,15). Huyo ni mtu wa Mungu twaona hapo
hafanyi kitu, hatendi kitu, haandiki kitu ili watu wampe pesa!
Anajitoa kwa ajili ya watu wa Mungu na kazi ya Mungu bila kutafuta
faida yake mwenyewe. Sikiliza maneno yake ya ajabu na yenye neema
na ya upendo kwa watu. “Maana sivitafuti vitu vyenu bali nawatafuta
ninyi…” (2 Wakor. 12:4). Sikiliza ushuhuda wake “Sikutamani fedha
wala dhahabu wala mavazi ya mtu.” (Mtd 20:30).
Waumini kadhaa wa huko Korintho hawakutambua huduma ya Paulo (1
Wakor.9:1-3; 2 Wakor.10:7-10). Walikuwa wakisema wao kwa wao kuwa,
"Paulo akiwapo mwilini ni dhaifu na maneno yake si kitu." Pamoja na
maneno hayo, Paulo hakushurutisha wampe pesa kama mtume wakati
akihubiri Injili miongoni mwao! Kwa hiyo wengine waliopo huko
Koritho walifikiri kuwa Paulo si mtu muhimu kwa sababu wao
walimtazama katika sura ya nje - walihukumu hukumu ya macho tu,
“Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu.” Wao waliamini kuwa kama
mtu ni mtume basi angewashurutisha kupewa pesa kwa ajili ya huduma
yake. Mawazo yao hayakuwa ya kiroho, hivyo Paulo aliwauliza swali
hili, “Je! Nilifanya dhambi kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa
sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?” (2 WaKor 11:7).
Mtume Paulo anauliza swali hapo kuwa je, alifanya dhambi kwa
kutokuwalazimisha kumpatia pesa!? Hapana, kwa vyovyote hajawatendea
dhambi yoyote, bali alikuwa anajaribu kuwaonyesha jinsi ambavyo
wanakosea katika kufikiri kwao. Na hata siku hizi waumini wengi
wanayo mawazo kama hayo ya kukosea kuhusu huduma, wanapenda kuona
kama mtu akijiinua na kudai kuwa yeye ni mtume, nabii au muhubiri
mkuu, na kama akija na fahari na kuanza kuwasukuma watu ili kutoa
pesa “kwa ajili ya kazi ya Mungu” (kama wanavyodai), ndivyo ilivyo
kuwa nyakati za Paulo. Kama tulivyosoma, hata yeye mwenyewe mtume
Paulo anawaambia, "mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani,
akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza akiwapiga usoni.” (2
Wakor.11:20). Lakini mtume Paulo anasemaje juu wa mitume wa aina
hii? Yeye anasema, “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo,
watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa
Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano
wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao
wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki.” (2 Wakor.11:13-15).
Hili ni neno kubwa na zito kwa wale wote ambao nia zao ni
kutengeneza faida kubwa kwa kuwatumia wale wanaowahudumia.
Iko wazi hapa kuwa kutokana na yote hayo tuliyoyaona na
kuyajadili, hii haimanishi kuwa eti, kwa kuwa Paulo yeye hakuomba
sadaka hizo na wakati mwingine yeye alikataa kupokea msaada wa
fedha, basi wale watendao kazi za kiroho za kumtumikia Mungu na
watu Wake, kwamba wasipewe msaada kukidhi mahitaji yao ya lazima!
Kinyume chake sasa, Biblia inatutia moyo kuwasaidia wale waatendao
kazi kubwa kwa niaba yetu kulingana na mahitaji yao wanayoweza kuwa
nayo. Na hii sasa ni kwa ajili ya upande wa washirika, kutokana na
upendo na haki basi wanapaswa kuwasaidia wao wanaowahudumia katika
Bwana. Na kwa upande wa wachunaji na wahubiri wanapaswa kuwahdumia
watu wa Mungu kutokana na wito wao, na upendo wa Mungu na Roho ya
Kristo. Tuwe tunaoishi sawasawa na pendo la Mungu lililomiminwa
ndani ya mioyo yetu na Roho Mtakatifu. Au tunaishi sawasawa na
sheria ya Torati iliyoandikwa katika vibao vya mawe? Yatupasa
tuelewe tofauti ya mambo haya mawili kama tukipenda kuishi kama
Wakristo.
DESTURI YA WAKRISTO/MAKANISA KUWASAIDIA WAUMINI MASIKINI.
Kama nilivyosema, mzigo na desturi wa Wakristo na makanisa
katika Agano Jipya ulikuwa kutoa pesa kwa kwa ajili ya washirika
MASKINI. Karibu mistari yote ya neno la Mungu iliyomo katika Agano
Jipya inayoelezea juu ya taratibu za ukusanyaji wa pesa inaelezea
na kufananishwa na ukusanyaji kwa ajili ya washirika walio masikini
- Matendo 4:33-35, 6:11:29, 11:29; War.12:13; 15:25,26; Wagal.2:10;
1 Wakor.16:1-3; 2 Wakor.8:1-7; 1 Tim. 5:3,5; Waebr.6:10; Yakobo
1:27; 1 Yoh.3:17. Ina maana, sehemu kubwa ya sadaka (utoaji) za
waumini zilitumiwa kuwasaidia washirika maskini. Kama tulivyoona,
mistari mingine inahusu msaada kwa ajili ya watumishi wa Mungu.
Ile desturi yetu ya kuchanga pesa jumapili (siku ya kwanza ya
juma), je, jambo hili linatokana na nini? Na waumini walitoa pesa
zao kwa ajili ya nini katika Agano Jipya? Ebu na tuisome ile
desturi iliyoanzishwa na mtume Paulo aliyoianzisha,
“Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile
nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya
kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya
kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;
nami nitakapofika nitawatuma kwa nyaraka wale mtakaowachagua,
wachukue hisani yenu mpaka Yerusalemu.” (1 Wakor.16:1-3).
Huko Yerusalemu walikuwepo waumini maskini wengi kwa hiyo Paulo
aliwasihi na kuwatia moyo waumini wale huko waliokuwa na uwezo
kuwasaidia ndugu zao maskini waliopo Yerusalemu. Na hapo Paulo
anatoa mipango juu ya namna changizo hilo litakavyofanyika. Basi
sasa, kutokana na maneno ya Paulo ni wazi tu kwamba jambo hili la
kuchanga pesa kwa ajili ya ndugu maskini ilikuwa jambo la kawaida
kati ya makanisani ya Agano Jipya. Kwa Warumi aliwaandikia
ifuatavyo,
“Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu maana
imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili
ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini.” (Warumi
15:25,26).
Kwa matendo yake pamoja na mafundisho yake mtume Paulo
aliwaonyesha waumini ni baraka kutoa kwa ajili ya wadhaifu na
maskini bila kutazamia kupata kitu! “Katika kila jambo nililofanya,
nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii
imetupasa kuwasaidia WADHAIFU, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu
mwenyewe jinsi alivyosema, ‘ni baraka zaidi, kutoa kuliko kupokea.’
” (Matendo 20:35).
“Changieni katika mahitaji ya watakatifu…” (Warumi 12:13). Kutoa
pesa kwa ajili ya ndugu maskini ilikuwa jambo la muhimu sana
makanisani wakati wa mitume! Petro alipozungumza na Paulo juu ya
Injili alimwambia, “Walichotuomba ni kwamba tuendelee KUWAKUMBUKA
MASKINI, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.”
(Wagalatia 2:10).
Mtume Paulo anawafariji Wakorintho wakue katika utoaji wao kama
vile wafanyavyo katika mambo mengine katika maisha yao ya kiKristo,
“Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani,
katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo
wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya
kutoa.” (2 Wakor.8:7).
Kutokana na haya yote basi tunaona wazi kuwa: 1. Waumini
walianzisha desturi ya kuchangishana pesa kwa ajili ya ndugu zao
maskini. 2. Walitoa kwa kadiri ya kufanikiwa kwa kila mtu! Maneno
ya mtume Paulo hapo ni wazi kabisa kuwa yeye haweki sheria juu ya
kipimo cha utoaji; yeye anaagiza juu ya namna ya kuchanga tu! Mtume
Paulo hawakamii waumini wa huko na wazo kulaaniwa wasipotoa!
Kama tukiangalia mistari yote iliyopo hapo juu ihusuyo
mafundisho juu ya utoaji, ni wazi kabisa kuwa mzigo wa kwanza
waliokuwa nao waumini ni kuwasaidia waumini (ndugu zao) maskini.
Kuanzia katika Matendo ya Mitume hadi waraka wa Yohana, ilikuwa ni
desturi ya makanisa kuwahurumia ndugu zao maskini.
Hayo yanahusu hususan wajane na yatima katika makanisa, na
makanisa ya Agano Jipya walikuwa na mfumo kuwasaidia wajane –
Matendo 6:1-6; 1 Tim.5:3,5,9,10; Yakobo 1:27.
SABABU YA KUTOA.
Tunatoa kwa sababu Yesu Kristo alitoa maisha yake kwa ajili yetu
na ametuokoa! Tulinunuliwa kwa thamani kubwa sana na sisi si mali
yetu bali Yake sasa. Tunatoa kwa sababu hiyo ni tabia ya Mungu,
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa
Mwanawe pekee…”. Na sisi tumefundishwa kufanya vivyo hivyo alivyo
Mungu alivyofanya - “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye
aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai
wetu kwa ajili ya hao ndugu.” Na tunafanya hivyo hasa kwa ajili ya
waumini maskini, “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha
akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo
wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” (1 Yoh.3:16,17). Tunafanya hivyo
“kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na
Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” (War.5:5). Utoaji wetu ni sehemu
ya upendo wetu kwa Mungu, na kwa watu Wake, na kwa kazi Yake
duniani; ni sehemu ya kuabudu kwetu kwa Bwana!
Ni jambo la kuhuzunisha sana tena sana kumwona mchungaji au
kiongozi fulani ajifanye kama bwana juu ya watu wa Mungu na ‘kupiga
mjeledi’ kwa mafundisho makali yake akisema, “Toe zaka, toe zaka,
au utalaaniwa!” – kana kwamba washirika ni watumishi wake! Kiongozi
wa namna hiyo anaharibu au kupotosha sura ya Mungu, yaani, tabia ya
Mungu machoni pa wasikilizaji, na anaharibu (angalau kwa kiasi)
uhusiano kati ya washirika na Mungu. Yampasa mchungaji awe mtumishi
wa washirika ni siyo kujiinua kama bwana! “Lakini Yesu akawaita,
akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na
wakubwa wao huwatumikisha. LAKINI HAITAKUWA HIVYO KWENU; bali mtu
ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu
ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama
vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa
nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Hiyo ni tabia ya mchungaji kweli
kweli. Yampasa mchungaji au kiongozi awakilishe ‘sura’ au ‘mfano’
au ‘chapa’, yaani, tabia ya Yesu Kristo mbele ya watu, machoni
pao.
Shida mmoja ni hiyo, viongonzi na wanchungaji wengi kwa lengo
lao la kupata faida (pesa) kwa ajili yao wenyewe, au kwa ajili ya
madhehebu yao, kila jumapili, walibuni mafundisho makali ili
kuwalazimisha washirika kuleta pesa kwao kila wiki! Kwa upande moja
wanawatisha washirika kwamba watalaaniwa na Mungu kama wasitoe
fungu la kumi (wananukulu hasa Agano la Kale kujaribu kuthibitisha
udanganyifu huo), au kwa upande wengine wanawatia moyo kupa pesa
kwa kuahidi watapata mengi kwa kurudishwa. (Kwa kawaida wananukulu
Malachi 3:10 na Luka 6:38). Mafundisho haya mawili yote ni
udanganyifu na dhambi dhidi watu wa Mungu ambao Yesu alikufa kwa
ajili yao! Kwa yale ya kwanza yanajaribu kuwalazimisha washirika
watoe kutokana na ‘hofu’ na ‘sheria’ badala ya upendo. Kwa yale ya
pili yanachochea uchoyo mioyoni mwa waumini. Wachungaji na viongozi
wengine wanafundisha, ‘Unaona, kama ukitoa elfu moja, kumbe,
utapata laki moja! Panda mbegu!’ Hiyo ni dhambi. Hiyo ni biashara!
Wanaharibu imani ya watu wa Mungu!
Sitoi ili nipate!
Inaandikwa “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na
kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu
watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho,
ndicho mtakachopimiwa.” (Luka 6:38).
Hiyo ni uthibitisho wa uaminifu na wema wa Mungu, sio sababu
kutoa! Baraka hizi za Mungu ni matokeo ya kutoa kwako – siyo sababu
ya kutoa! Ukitoa kwa uchoyo wa kupata, unaharibu thamani ya utoaji
wako mbele ya Mungu na pamoja na hayo kwa hakika utakosa baraka
zile Bwana Yesu alizozitaja kwenye Luka 6!
Yesu alizidi kufundisha, “Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni
mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo
thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu.”
(Luka 6:35). Kwa mujibu wa Biblia, tunabarikiwa zaidi kupitia
kutoa, kuliko kupitia kupokea! “Ni baraka zaidi kutoa kuliko
kupokea.” (Matendo 20:35).
Uwe mwangalifu sana! Usidhanie kuwa unaweza kununua au kulipa
kwa ajili ya baraka za Mungu! Ikiwa kuna mtu anayejiita mwenyewe
kuwa ni mtumishi wa Kristo Yesu, na anataka pesa zako ili akuombee,
mtu huyo ni mdanganyifu na hamtumikii Kristo kabisa. Ikiwa
umefundishwa kuwa unapaswa kutoa pesa katika matoleo yako iwapo
utakuwa umebarikiwa na Mungu katika mkutano, ndipo utakuwa
umefundishwa vibaya - mtumishi wa aina hiyo sio tu kuwa
anamwakilisha vibaya Mungu, bali anakosa. Ebu sikiliza mstari huu,
ili ukweli huu uingie katika moyo wako,
“Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya
kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali… moyo wako si mnyofu mbele
za Mungu.” (Matendo 8:21,29)
Wazo ya kwamba tunapaswa kulipia ili kupokea baraka za Mungu, au
wazo ya kwamba tunadaiwa na Mungu pale tunapokuwa tumebarikiwa, ni
fundisho la uovu. Wazo hili limeimarishwa kwa kiasi kutokana na
tamaa za watumishi ambao wanajitumikia wenyewe. Watumishi
wanaozurura kule na kule wakitafuta mbinu za kuwaibia waumini mali
zao na pesa zao kwa kisingizio kuwa Mungu anazitaka pesa hizo ili
wao waweze kubarikiwa. Huo ni uongo wa mchana kweupe. Usinielewe
vibaya! Sisi, kama watu wa Mungu, kwa hakika tutayaleta matoleo
yetu, lakini tunatoa pesa kwa sababu ya upendo wetu kwa watu wa
Mungu ambao wanasumbuka kwa kukosa mahitaji ya lazima, na kwa ajili
ya upendo wetu kwa ajili ya kazi ya Mungu; kadhalika na kuwapa watu
wengine kwa moyo wa huruma na upendo. Lakini hatutoi kwa moyo wa
uchoyo wala ‘kununua’ baraka za Mungu. Ndiyo, Mungu anaweza
kutugusa mioyo yetu kwenye mikutano na kutuelekeza kutoa kwenye
eneo maalumu lihusulo kazi yake Mungu. Lakini hiyo ni mwitikio wa
kile ambacho Mungu anakifanya ndani ya moyo wako kwa wakati huo,
ambalo ni jambo la tofauti kabisa na lile la kufanya kitu kwa
ulazima au sheria.
Zaidi ya yote, Yesu Kristo alifundisha, “bali wewe utoapo sadaka
hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume.”
(Mathayo 6:3). Utoaji wetu unapaswa uwe kwa wepesi utokanao katika
upendo wetu kwa ajili ya Mungu na watu wake na wengine pia. Utoaji
wetu usiwe ni mbinu ya kutengeneza faida fulani katika maisha yetu,
kama ifanywavyo au kuamuliwa na watumishi wengi kuwa “Panda mbegu”.
Mafundisho ya jinsi hii ya kupanda mbegu na mawazo ya aina hiyo ni
ya uovu mtupu.
Napenda kumaliza sehemu hiyo kwa kunukuu maneno ya Dr. Frank
Philip Seth (anayetoka Dar Es Salaam), ambaye huweka mambo hayo kwa
ufasaha mzuri,
“Mafundisho mengi kuhusu UTOAJI wa SADAKA yamekuwa na shida ya
kuelemea upande fulani, hivyo kupelekea watu kushindwa kufanya
yawapasayo na kuishi kwa hofu, bila kupata baraka zinazostahili
katika utoaji wao.
Lengo la msingi kabisa ni KUMCHA Mungu. Mambo mengine yatafuata
hapo, kwenye kusudi/lengo la utoaji wako, ila anza na Mungu. Kama
lengo sio kumpendeza Mungu, au kutoa kwa kumcha Mungu, fikiri tena
kwa habari ya utaoji wako. KANUNI ya msingi ya utoaji wowote ni
kutoa kwa MOYO wa kupenda. Ukitoa kwa sababu ya KULAZIMISHWA,
angalia tena kusudi la huo utoaji. Jifunze kutoa kwa UKARIMU kwa
maana utavuna kwa ukarimu pia.
Sasa najua watu wamefundishwa kutazama baraka, kama ndio
kichocheo cha kutoa zaka na sadaka zao. Kumbuka baraka ni matokeo -
kichocheo cha kutoa na lengo la MSINGI ni kumcha Bwana Mungu wako.
Ukitoa kwa sababu unamwogopa au unamwonea aibu mchungaji wako, hiyo
ni shauri yako, ila leo nakupa shauri, toa zaka na sadaka zako kwa
sababu unataka KUMCHA Mungu na kumpendeza. Fuata maagizo yake, na
ujue kiasi, mahali na muda wa kutoa …sadaka zako. Bila kusahau
kwamba Bwana alisema sadaka ni SIRI; “mkono wako wa kushoto usijue
nini mkono wa kulia unafanya”.
Nisikilize kwa makini. Sisemi kuwekewa mikono au kuombewa baraka
ni vibaya, ila HAKUNA namna mtu atatoa sadaka zake kwa MOYO MBOVU
kama wa Kaini, halafu akawekewa mikono, ikamsaidia kupokea baraka,
hakuna! Kwa upande wa pili, hakuna mtu atatoa sadaka zake “kwa
SIRI”, bila kuwekewa mikono na mtumishi yeyote, ila ametoa sadaka
zake kwa MOYO MZURI kama wa Abeli, asipokee baraka zake kwa kipimo
cha kujaa, kusukwa-sukwa, na kufurika. Thamani ya sadaka yako ni
MOYO wa shukrani, uelekevu na ibada mbele za Mungu wako. Usisahau
hata siku moja, baraka za Mungu hazinunuliwi kwa sadaka, ila kwa
“moyo wa uelekevu” mbele za Mungu wako.
Sasa, nataka uone kwa undani kidogo habari ya sadaka…, ili
usijivune sana utoapo. Kwanza, imekupasa kujua kwamba Mungu hana
shida na hiyo pesa yako, ila HALI ya moyo wako utoapo hizo sadaka
zako. Angalia tena hapa, “Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo
waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta?...BWANA anataka nini
kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa
unyenyekevu na Mungu wako.” (Mika 6:6-8). Bwana Yesu akiona shida
iliyoko kati ya taratibu za KIDINI, akasema maneno haya, ambayo
nabii Mika alisema pia, “Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye
mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya,
Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia”
(Mathayo 12:6,7). Yesu anasema, kuna mmoja aliye mkuu zaidi kuliko
hekalu lako, naye ni Mungu; na anachotaka kwako sio SADAKA ila
REHEMA. Sasa usisahau kwamba Rehema ni “hali ya moyo inayompelekea
mtu kutenda au kuenenda kwa namna fulani”; sasa ukiwa na MOYO wa
REHEMA, kisha ukatoa sadaka zako, umefanya jambo jema sana.
Ukisukumwa kutoa ILI ubarikiwe, jua umepoteza lengo la MSINGI la
utoaji wako;…chunguza moyo wako na uhusiano wako na Mungu.”
(Dr.F.P.Seth: “Zaka ya Fungu la Kumi”).
Kumbuka, ‘Mungu huuangalia moyo’. Thamani ya utoaji inazingatiwa
na hali ya moyo wako.
JE, PESA ZIKUSANYWAZO JUMAPILI KAMA SADAKA ZINAMHUSU NANI?
Pesa zangu nizitoe kwa nani na kwa ajili gani? Hili ni swali
muhimu sana na ni la msingi. Ikiwa wewe ni Mkristo, basi bila shaka
utakuwa unahudhuria ibada mara kwa mara. Kwa hiyo, ni haki
kulisaidia kanisa kwa ajili ya gharama zinazotumika hapo. Kwa mfano
gharama kwa ajili ya kulipia umeme au mafuta zinazotumika kanisani
hapo n.k. Lakini pia ni haki kumsaidia mtumishi anayetumika hapo
kanisani kwa moyo wa uaminifu; kumsaidia ili apate kukutana na
mahitaji yake ya muhimu na ya lazima, na sio kumfanya awe
tajiri.
Lakini ni uhakika ulio wazi kabisa kuwa halipo fundisho lolote
katika Agano Jipya linalosema kuwa makusanyo yote ya sadaka, au
hata sehemu yoyote ya pesa hizo kwamba eti, zinamhusu mchungaji au
kiongozi wa kanisa. Lakini tafadhali usinielewe vibaya! Kama
nilivyokwisha kuonyesha katika mistari niliyoitaja hap juu, nami
nitaendelea kuitaja hapo chini - ni wazi kuwa Wakristo wanapaswa
kuwasaidia wale wanaowatumikia kwa kazi. Lakini ni makosa kwa
wachungaji na viongozi wengine wao kujifanya kana kwamba ni
wakurugenzi huko makanisani na kuwekeza mifumo kwa washirika wao
ambayo ipo kinyume kabisa na neno la Mungu. Zaidi ya hayo yote,
waumini katika Agano Jipya walijua wazi kuwa wanamtolea nani na
nini wakitoacho. Mifumo ya utoaji ambayo waumini wanatoa pesa kisha
wao hawaambiwi kuwa pesa hizo zinaenda wapi ni makosa makubwa na ni
kinyume cha haki mbele za Mungu. Hata katika mifumo tu ya dunia
watu hutambua jambo hili - makampuni, mashirika au hata serikali,
wao huchapisha mahesabu yao yanayoonyesha ni kiasi gani cha pesa
kilichotumika.
Sasa je, kanisa linapaswa kutenda kinyume na haki na kutokuwa na
uwazi kuliko hata wafanyavyo wasioamini? Je, viongozi wanasumbuliwa
na jinsi wanavyozitumia pesa hizo kiasi kwamba sasa wanajitafutia
njia za kuwaficha ukweli wa taarifa ya makusanyo ya pesa hizo wale
wanaozitoa pesa hizo? Hii ni inaingizwa ni makosa na ni mchezo usio
na haki hata kidogo.
Kama tulivyoona, waumini walitoa pesa kuwasaidia waumini maskini
na watumishi wa Mungu mbalimbali. Lakini lipo fundisho la uongo
lisemalo kwamba lazima ulete sadaka (utoaji) zako ZOTE kanisani
ambapo unaabudu (kwa ajili ya huduma). Hiyo ni ubuni wa kibinadamu
kabisa! Fundisho hili halitokani na Biblia. Kama hili ni kweli,
hatuwezi kuufuata mfano wa Msamaria mwema, na mithali hiyo ya Yesu
haina maana sasa! Aidha, Yesu alitufundisha, “Akuombaye, mpe; naye
atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.” (Mt.5:42). Fundisho hili
halina msingi katika neno la Mungu. Fundisho hili linafanya kanisa
liwe kama biashara na msukumo wa fundisho hili inaonekana kuwa ni
uchoyo tu. Tunajua kwamba waumini huko Jerusalemu mwanzoni
waliileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa
mitume, lakini hiyo ilikuwa tendo la pekee kabisa na haliwakilishi
utaratibu ambao waumini na makanisa waliufuata baadaye, kama tayari
tumeshaona! Ulikuwa mfano mmoja wa utoaji tu!
Watu wanajaribu kuhalisisha fundisho hili kwa kudai Malaki 3:10
inathibitisha wazo hili lao! Mara moja tunatambua dai lao halina
msingi katika Agano Jipya kwani wanakimbilia Agano la Kale ili
kujaribu kuthibitisha wazo lao! Kama tulivyoona, kwa ujumla ni
jambo la kawaida kuleta sadaka zetu kanisani – hiyo ni wazi, hamna
hoja – lakni ni wapi Yesu au mitume wafundishapo kwamba lazima
ulete sadaka zako zote kanisani unapoabudu? Hamna fundisho hili
katika Biblia. Njia mmoja ni kupotosha maana ya Malaki 3:10, na wao
wanafanya hivyo. Mstari huo unatufundisha mambo yale tayari
tuliyoyajifunza katika makala hiyo, yaani, kama sehemu ya kuabudu
kwetu kwa Mungu tunapaswa kuwasaidia watumishi wa Mungu na
washirika maskini kupitia sadaka zetu kutokana na upendo wa Mungu
ndani ya mioyo yetu. Hiyo tu.
‘Zaka’ iliyotajwa katika Malaki 3:10 haihusu ‘walawi’ tu (wao
waliohudumia hekaluni)! Ilihusu ‘mgeni’, ‘wajane’ na ‘yatima’ pia!
Tena hapo napenda kunukuu kutoka mafundisho ya Dr.F.P.Seth
yanayohusu sehemu hiyo na sehemu ifuatayo,
“Pamoja na sababu BINAFSI za utoaji, ambazo msingi wake uko
katika KUMCHA Mungu na KUMWABUDU, kuna mambo ya msingi ya kuangalia
hapa. Kwanza, imekupasa kujua kwamba mfumo wa sadaka uliwekwa ili
kuwepo na CHAKULA katika nyumba ya Mungu, au katikati ya watu wa
Mungu. Angalia hapa, “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo
chakula katika nyumba yangu”. Hili neno “ghalani” limekuwa na
tafsiri kwamba (ghala ni ‘kanisani’ ambapo mtu anaabudu). Lakini
nakwambia leo, hili neno “ghalani” ni zaidi ya kanisani kwako
(Malaki 3:10). Sasa tafsiri ya Chakula ni Chakula, yaani hiki
chakula cha kujenga mwili na sio cha roho (Neno). Hata kama itakuwa
sadaka ya pesa, lengo ni kiwemo “chakula” na sio tafsiri ya “Neno”
au “mahubiri”.
Watu wengi wamejaribu kubadili hili neno “chakula”, na kusema ni
“mahubiri”… Neno la Mungu ni chakula, ila hapa kwenye Malaki,
hasemi habari ya mahubiri (Neno), anasema habari ya chakula cha
mwilini kabisa (ugali, mchele, nyama, nk.). Lengo la Mungu kusema
watu “walete chakula (zaka)” ni hili hapa, “Kila mwaka wa tatu,
mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo,
uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala
urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na
mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba”.
(Kumb. 14:28,29). Hapo hakuna kitu kama mahubiri, ni chakula kabisa
cha damu na nyama. Je! Masikini, wajane, na yatima wako wapi wakila
na kushiba katikati yetu?
Angalia tena, Mungu aliweka mfumo wa kutoa sadaka kwa ajili ya
watu wasio na KIPATO au URITHI katika jamii husika. Ndipo tunaona
Walawi … wanatajwa hapa, WAKICHANGANYWA na mgeni, yatima, wajane,
nk., yaani watu wenye UHITAJI katika jamii. Hawa wote hawakuwa na
chakula cha kutosha, kwa sababu hawakuwa na urithi (Mlawi na mgeni)
AU mtu waliyemtegemea amekufa (yatima na mjane), na kupitia ZAKA,
wanapaswa wale na kushiba. Sasa ukiangalia “ghala” kwenye kitabu
cha Kumbukumbu la Torati, utaona unaagizwa “uliweke ndani ya
malango yako”. Sasa sisemi kupeleka kanisani kwako ni makosa, ila
SIO lazima ufanye hivyo… Ukitaka kuona shida katika mafundisho ya
utoaji, jiulize maswali yafuatayo, Je! Mtumishi fulani akipewa ZAKA
au SADAKA na kondoo asiye wa kundi lake, anakataa na kumwagiza huyo
kondoo apeleke kwa mchungaji wake? Kama anapokea kutoka kwa kondoo
wasio wa kundi lake, kwa nini anazuia kondoo wake wasiongozwe na
Mungu wao kutoa sadaka zao mahali pengine? Jiulize tena swali, Je!
Mungu akisema “kuanzia sasa, wanadamu wote wasitoe tena sadaka za
fedha na vitu”, Je! Hao watumishi wataendelea na huduma kwa moyo
ule ule? Jibu mwenyewe maswali haya kwa nafsi yako, wala usimtazame
mwingine.
Umewahi kufikiri watumishi wanasema “leteni zaka yote na sadaka
zenu kwa sababu mnakula kiroho hapa kanisani”, na ghafla! Mungu
anabadilisha utaratibu na kusema, “wapeni watumishi wangu vitu vya
rohoni tu, yaani faraja na maombi, ila msiwape pesa na vitu”.
Fikiria mwenyewe ni huduma ngapi zingesimama. Halafu ujiulize kwa
nini zimesimama? Je! Hawana chakula au hawana faida? Ndipo
utagundua tofauti kati ya mchungaji wa halisi na mchungaji wa
mshahara.
Hebu piga picha uone jinsi wajane, yatima na masikini
WANAJIKAMUA kupeleka zaka zao kanisani kwa sababu “wametishiwa
maisha” kwamba watalaaniwa wasipofanya hivyo. Kweli imewapasa watu
WOTE kutoa zaka na sadaka zao, ila kwa KUMCHA Bwana, na kwa MOYO wa
KUPENDA kutoa, sio kwa HOFU na VITISHO. Kama mtumishi angechagua
vyema, angewalazimisha watu kwa ukali ZAIDI wasitende dhambi,
kuliko kuwalazimisha watu kutoa zaka na sadaka zao wakiwa dhambini;
mtumishi wa namna hii angekuwa upande wa Bwana na sio wake
mwenyewe.
Soma maandiko na uongozwe na Roho Mtakatifu kujua mambo haya,
kwa maana iko baraka katika KUWATUNZA wajane (hasa), masikini,
yatima na wahitaji wengine, bila kuwasahau watumishi wa Mungu aliye
hai, ili kazi ya huduma iendelee na mwili wa Kristo ujengwe.”
(Dr.F.P.Seth: “Zaka ya Fungu la Kumi”).
Nilinukuu haya siyo ili tufuate sheria ya Agano la Kale, lakini
Dr. Seth aliweka wazi kutokana na Malaki 3, na mstari 10 mwenyewe,
kuwa hata Agano la Kale linathibitisha mambo tuliyoyaona kwenye
Agano Jipya na niliyoyaandika hapo, yaani, sadaka ya watu
zilitumiwa kwa ajili ya watu maskini na kwa ajili ya watumishi wa
Mungu. Zaidi ya hayo, wale wanaotumia Malachi 3:10 ili kufundisha
kuwa lazima ulete utoaji wako wote kanisani mwako, wanakosa sana!
Ni jambo la uchoyo tu.
Aidha, Kwa ujumla, siyo shughuli ya mwingine ajue utoalo - siyo
shughuli ya ndugu yako, wala kanisa lako, wala mchungaji wako ajue
utoalo! Haimhusu mtu yeyote yule kujua ni kiasi gani umeweka ndani
ya kapu la sadaka au umeweka kwa ajili ya nini, jambo hili ni kati
yako wewe na Mungu, basi. Wale, wanaokulazimisha kuwajulisha
viongozi wa kanisa kiasi unalotoa wanafanya dhambi, “Bali wewe
utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono
wako wa kuume.” (Mathayo 6:3).
------------------------------
‘Nyumba ya Mungu’, Ukuhani na ‘Madhabahu’.
Wengine wanafundisha lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka au
kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa
sababu madhabahu yapo pale pale tu. Hiyo ni kosa kubwa sana. Kwa
ajili ya upungufu wa nafasi, nitanukuu kwa kiasi kidogo kutoka
makala yangu iitwayo “‘Nyumba’ ya Mungu na ‘Madhabahu’ ni nini?”
Lakini unaweza kusoma makala nzima kupita link hiyo:
https://somabiblia.com/nyumba-ya-mungu-ni-nini/ Kwa hiyo, haya kwa
ufupi:
“Kama kuna mtu yeyote atasema kuwa jengo au chumba ambacho
Wakristo hukutanika siku za jumapili kuwa hiyo ni 'nyumba ya Mungu'
au akisema ‘Karibuni kwenye nyumba ya Mungu,’ basi watu hao
watakuwa wanaupotosha ukweli mkuu wa Agano Jipya. Ni makosa na
watakuwa wanawafundisha watu wa Mungu kimakosa - wanawafanya
wafikiri kuwa ukweli huu wenye nguvu za kiroho unahusu tu mambo ya
nje. Kama vile matofali na chokaa. Sisi (watu wa Mungu) tu kanisa.
Sisi ni hekalu la Mungu kiroho (Waefeso 1:22,23; 2:21,22). Mahali
pale wanapokutanika watu wa Mungu hapo ndipo kanisa la Mungu lilipo
– hata kama mahali hapo ni chini ya mti! Nyumba ya Mungu ni kanisa,
na kanisa ni watu wa Mungu (1 Timotheo 3:15).
Hakuna tena mwendelezo wa kuhani wala ukuhani kati yetu sisi na
Mungu - kwa sababu sisi tumefanywa kuwa ukuhani mtakatifu, ukuhani
wa kifalme (1 Petro 2:5-9), na Yesu ndiye kuhani wetu mkuu
(Waebr4:14). Na yeye pekee ndiye mpatanishi kati ya mwanadamu na
Mungu. (1 Timotheo 2:5). Kwa hapa duniani sisi ambao ni watu wa
Mungu, tu hekalu la Mungu. Kupitia Yesu Kristo tunayo nafasi ya
kuingia katika uwepo wa Mungu, katika patakatifu pa patakatifu
mbinguni (Waebr. 4:16,10:19).
Kama mtu yeyote yule kudai kuwa bado ipo madhabahu hapa duniani
ambayo inawapasa Wakristo kuiendea, huo ni udanganyifu kwa ujumla
wake. Kusema au kudai kuwa kuna aina fulani ya madhabahu ya kidunia
inayoonekana ambapo Wakristo wanakutana pamoja huko ni kulikataa
Agano Jipya. Ye yote asemaye lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka
au kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa
sababu madhabahu yapo pale pale tu, anakosa sana. Anajaribu kufanya
kanisa liwe kama biashara! Hamna mafundisho hayo katika kanisa la
Bwana, katika Agano Jipya. Usinelewe vibaya, kwa ujumla ni jambo la
kawaida kuleta pesa ya sadaka yetu ‘kanisani’, hata hivyo hamna
fundisho kuwa lazima utoe pesa yako yote kwa kanisa. Wazo hili
inakaribia ushirikina. Upendo wa Mungu mioyoni mwenu utatuongoza
kutoa pesa yetu kwa ajili ya mahitaji aina ya mbalimbali.”
Ufupisho
Tumeuona utoaji wa waumini mara nyingi katika kanisa la kwanza
katika Agano jipya ukilenga katika kuwasaidia waumini ambao ni
masikini. Sio kuwafanya wawe wavivu, la, bali ni kwa sababu wao ni
masikini halisia. Biblia inalionyesha jambo hili kwa uwazi sana, na
utoaji wa kuwasaidia watumishi wengine wanaoteseka ni msisitizo wa
wazi ulioainishwa katika Agano Jipya – na katika Agano la Kale pia.
Kama kanisa lako linahusika na utaratibu kama huu, basi hata wewe
unaweza kusaidia kwa kuchangia kwa ajili ya mambo kama haya. Lakini
hamna mafundisho kuwa utoaji wako wote ni lazima uende kwenye
kanisa lako lile tu unalosali? Kwa hakika kabisa sio hivyo! Kama
unawajua Wakristo maskini – hasa yatima na wajane - au hata
mtumishi mwaminifu anateseka mahala fulani katika huduma kwa
mahitaji ya lazima, kwa vyovyote unaweza kuwasaidia watu hao; au
kuisaidia huduma ambayo inahusika na kusaidia watu masikini katika
kuwapatia chakula, nguo, Bibilia n.k. Sababu kuu inayoyafanya
makanisa haya yadai kuwa matoleo yako yote ni lazima uyatoe
hapohapo unapoabudu tu au ni lazima matoleo hayo yapitie kwao, ni
hii hapa - wakuu wa hapo wanazitamani pesa zako! Je, ipo sababu
nyingine! Je, Msamaria mwema awezaje kumsaidia mtu anayeteseka
iwapo ataambiwa, “Oh, samahani sana ndugu, siwezi kukupa msaada huu
kwa sababu matoleo yangu kwanza lazima nitoe kanisani kwangu
ninakoabudu au yapitie kwa kiongozi wangu kanisani.” Je, Msamaria
huyo atakuwa ameokoa hali ya ndugu ambaye anamwona anateska kwa
kupungukiwa na mahitaji ya lazima? Lakini uovu huu ndio
unaofundishwa makanisani, na wengi wanaridhia fundisho hilo!
UTARATIBU WA KUTOA
Tunachokionyesha ndani ya makala hii, ni kwamba kukuelezea kuwa
haikuwepo sheria kwa Wakristo kwa ajili ya utoaji katika kanisa la
Agano Jipya, na wala hakukuelekezwa ni kiasi gani tunapaswa
kukitoa. Kwa hiyo, hata sasa na mimi sitengenezi sheria yoyote kwa
ajili yako hapa, lakini hebu niseme hivi: Mtu anaweza kusoma makala
hii niliyoiandika na akaamini, na bado yeye akapenda kupanga kutoa
mara kwa mara na sio kuwa mvivu katika kutoa kwake - hataki
kutokujali jambo la utoaji - kwa hiyo mtu kama huyo anaweza kupanga
kiwango fulani kila wiki au kila mwezi, kama msingi wake kila wiki
au mwezi, lakini pia akatoa mara nyingine kadiri mahitaji
yanavyozidi kujitokeza au kadiri Mungu anavyomfanikisha. Hakuna
tatizo lolote katika jambo kama hili. Hii inatokana na kuitunza
kanuni tuliyoisoma, ambayo ni kwamba kila mmoja alitoa kadiri
alivyoamua moyoni mwake, kulingana na uwezo wake na kadiri Mungu
alivyomfanikisha. Lakini hii inahusiana na mahusiano ya muumini
yule na Mungu katika maisha yake binafsi. Haihusiki na kanuni
yoyote ambayo mtu yoyote anaweza kuitengeneza ili kuwalazimisha
watu kutoa kanisani. Ule utoaji ni uamuzi wa mtu mwenyewe na kama
nilivyokwisha kusema kuwa makala hii imeandikwa ile kurekebisha
matumizi mabaya ya utoaji (upotoshwaji wa utoaji makanisani)
yanayofanywa kwa upande wa viongozi na wachungaji wengi. Hapa
sitengenezi sheria mpya, bali naonyesha kupitia mistari ya neno la
Mungu misingi inayowafanya watu watoe.
Labda utashangaa juu ya maneno hayo, lakini kama nilivyosema,
lengo langu siyo kukuambia wala kukuagiza utoe kiasi hiki au kiasi
kile katika utoaji wako, ila kuondoa kila nafasi, kila hoja na kila
hila ambazo viongozi mbalmabli wanazozitumia ili kukulazimisha -
kwa kukutisha na kwa kupotosha neno la Mungu – kutoa pesa kanisani
kadiri ya maagizo yao; badala yake, tutoe kwa moyo mnyofu sawasawa
na neno la Mungu.
MISTARI INAYOITUMIWA NA WATU KUUNGA MKONO UTOAJI WA KIKUMI.
MALAKI 3
Wachungaji na watumishi, pamoja na viongozi wanaowatisha watu
kwa laana, au wanaojaribu kuwashawishi watu waweze kutoa pesa kwa
kuwaahidi kuwa Mungu atawarudishia pesa hizo mara mia zaidi, watu
hao wanapinga mafundisho ya Kristo Yesu mwenyewe. Kuna eneo moja tu
katika Agano la Kale mahala ambapo panakemea kuhusiana na utoaji wa
kikumi (Malaki 3:8-10). Kukemea huko kulikuja moja kwa moja kutoka
kwa Mungu kupitia mtumishi wake Malaki. Kama unasoma kitabu hiki na
muktadha wake utaona kuwa Mungu anawakemea Waisraeli kutokana na
ibada zao za sanamu, na kwa kumpa Mungu mgongo wao. Alama moja ya
uasi wao ilikuwa walizidharau matoleo ya Mungu, na kwamba
anachokitafuta Mungu hapo ni kuwataka Waisraeli waache dhambi zao
na kumrudia Bwana, ndipo watakapomheshimu Yeye kwa kutoa kilicho
cha haki - na hiyo ingekuwa ni ishara kuwa Israel wamerejesha mioyo
yao kwake Mungu. Kimsingi hapo Mungu anaelezea hali ya mioyo yao.
Ebu sikiliza kile ambacho Mungu anakisema kwa IsraelI katika Malaki
1:10,
“Sina furaha kwenu, asema Bwana wa majeshi, wala sitakubali
dhabihu yo yote mikononi mwenu.”
Unaona hapo kuwa matoleo au sadaka zetu tunazomtolea Mungu
hazina maana yoyote mbele zake Mungu mpaka pale mioyo yetu iwe
imemrudia yeye au ipo sawa mbele yake. Unaweza kusoma kitu hicho
hicho katika Malaki 2:12-13. Mungu anasisitiza jambo hilo kwenye
Agano la Kale lote kama ilivyo katika Isaya 1:11. “Huu wingi wa
sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana.” Na tena,
kupitia Amosi Mungu anasistiza kwamba zaka na sadaka hazina maana
wakati tunapofuata dhambi, “Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali,
mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu
kila siku ya tatu.” (Amosi 4:4). Tukiifuata dhambi kama Waisraeli
walivyofanya wakati wa Amosi, hata zaka yetu ni dhambi – kwa sababu
ni jambo la unafiki na udanganyifu.
Sadaka ya Abeli ilikubaliwa na Mungu, lakini sadaka ya Kaaini
ilikataliwa, na hiyo ilitoka na hali ya moyo wake. Katika kitabu
cha Malaki nabii yule anaelezea juu ya hali ya moyo wa Israel, na
Mungu anawaambia watu wake kuleta sadaka ya kweli, hii ni kutoka
moyoni ambako kuna amwabudu Yeye kwamba iwe ni ishara kwamba
wamemrudia Yeye kutoka kwenye dhambi yao na kuabudu kwao sanamu
zao.
Hivyo basi wachungaji na watumishi wengi mara nyingi huwaonya na
kuwakemea waumini wao ili kuwafanya waogope na waanze kutoa, jambo
ambalo Agano Jipya linafundisha wazi kuwa utoaji usiwe ni wa
kulazimishwa. Watu hawa wanaangalia mambo kwa nje katika kutoa,
badala ya kuangalia hali ya moyo ndiyo inayoleta thamani katika
kutoa kwao. Lakini kwa vyovyote watu hao hufanya hivyo kwa sababu
hawafurahishwi na hali ya kiroho ya wasikilizaji wao, bali wao
hufanya kila njia ili kuvuna pesa nyingi kadiri wanavyoweza kutoka
kwa waumini wao. Huu ni ukatili mkubwa wa kiroho wanaotendewa
watoto wa Mungu katika kanisa la leo. Bila shaka, tuliyoyasoma
katika Agano la Kale hapo juu kuhusu Israel yanatuonyesha kwa wazi
kuwa lengo la Mungu ni mioyo ya uasi ya watu Wake ibadilishwe
kwanza, na utoaji safi ikafuata kama matokeo ya mabadaliko hayo! Ni
jambo tupu na la udanganyifu kukosa katika utaratibu huu, yaani,
kuwalazimisha watu wa Mungu watoe pesa na kumbe, kwa ghafla sasa
watu hao ni watu wa kiroho kwa ajili ya utoaji huo! Lakini
wachungaji wengi wanafanya vivyo hivyo.
Kumbuka, ‘Mungu huuangalia moyo’. Thamani ya utoaji inazingatiwa
na hali ya moyo wako.
-------------------------------
Baadhi ya watu hufikiri kuwa Waebrania 7 inatufundisha sisi
kwamba tunapaswa kutoa vikumi. Katika sura hiyo mwandishi
anatuonyesha kuwa Ibrahimu alitoa kikumi chake kwa Melkizedeki, kwa
namna moja hata kabila la Lawi lilitoa kikumi kwa Ibrahimu. Hata
hivyo ukiangalia kwa umakini sura hiyo, hakuna fundisho lolote
linaloonyesha kuwa Wakristo wanapaswa kutoa kikumi. Eneo hilo
mwandishi anawaonyesha wasomaji wake wa kiyahudi (wakati ule)
kwamba waelewe kuwa Yesu Kristo ni mkubwa kuliko Ibrahimu. Hiyo tu!
Ibrahimu alitoa kikumi chake kwa yeye ambaye alikuwa hana mwanzo
wala mwisho wa siku zake! Katika ujumla wake kitabu chote cha
Waebrania kiliandikwa ili kuonyesha kuwa Yesu, Mwana wa Mungu, ni
mkubwa kuliko malaika, mkubwa kuliko Musa, mkubwa kuliko Ibrahimu
na ni mkuu kuliko ukuhani wa Walawi.
Zaidi ya hayo yote, hakuna popote katika Agano Jipya ambapo
panafundisha kuwa wachungaji wanafananishwa na makuhani wa Agano la
Kale na kwa hiyo watu wa Mungu watoe kikumi cha mapato yao kwa
mchungani wao! Kuna mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na wanadamu
naye ni YESU KRISTO (1Tim 2:5). Hatunaye kuhani yeyote hapa duniani
ambaye anaweza kusimama kama mpatanishi wetu kwa Mungu isipokuwa
Yesu Kristo pekee basi! Je, hawajasoma katika Biblia yao kuwa sisi
watakatifu wa Mungu ya kwamba sasa wote ni makuhani! Sisi ni
“ukuhani mtakatifu, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, mzao mteule
watu wa miliki yake Mungu”. (1Petro 2:5,9). Inapaswa ieleweke wazi
kuwa heshima hii ya kikuhani haiwaendei wachungaji tu na viongozi
fulani fulani wa dini zao. Hapana. Heshima hii Mungu ameiwekeza kwa
kila amwaminiye Yesu! Na huu ndio wema wa Mungu wetu leo katika
Agano Jipya.
Iwapo baadhi watapinga kuwa utoaji wa kikumi alioufanya Ibrahimu
ulifanyika kabla ya ujio wa sheria ya Mus