-
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA
MAADHIMISHO YA SIKU YA MWALIMU DUNIANI TAREHE 11 OKTOBA,
2006
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh. Margaret Sitta
(Mb);
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Henry Shekifu (Mb);
Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Yahya Msulwa;
Waheshimiwa Viongozi wa chama na Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania;
Walimu wote, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima mliyonipa
ya kunialika
kushiriki nanyi katika sherehe hizi za maadhimisho ya Siku ya
Mwalimu Duniani.
Nawashukuru kwa mapokezi mazuri mliyonipa na burudani murua za
kwaya na
muziki wa Boka Boma Music Band.
Nawapongeza wale wote walioshiriki kuandaa maadhimisho haya
yaliyofana.
Nimefurahishwa sana na niliyoyaona kwenye mabanda ya maonyesho.
Pongezi za
pekee kwa Chama cha Walimu Tanzania kwa kuendelea kuwaunganisha
walimu
nchini, na ninawapongeza walimu wote kwa kuadhimisha siku yenu
leo
hii. Nawaahidi ushirikiano wangu na ule wa wenzangu wote
Serikalini.
-
Ndugu viongozi, ndugu wananchi;
Leo tunawapongeza walimu kwa kuadhimisha siku yao duniani. Hii
ni siku
muhimu kwa walimu. Ni siku ambayo walimu duniani kote hutafakari
mahali walipo
na kule waendako katika kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu. Na
sisi wadau wengine
ni fursa ya kuonyesha shukrani na pongezi zetu, kama Taifa, kwa
walimu wote nchini
kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulijenga na kuliendeleza
Taifa letu.
Nchi yetu ni kubwa na maeneo mengi yanapishana kwa viwango
vya
maendeleo, lakini Mwalimu yuko katika kila kona ya nchi hii.
Walimu ndio huwafunda
na kuwalea raia na viongozi wa kesho wa taifa letu.
Vilevile, walimu ndio wanaotutengenezea viongozi katika fani
mbalimbali za
taaluma na ujuzi. Walimu ndio wanaotujengea nguvu kazi ya
kutumainiwa ya Taifa
letu. Walimu ndio wanaoijenga haiba ya taifa. Nakubaliana nanyi
kabisa kwamba
walimu ndio chimbuko la taifa na utaifa. Miongoni mwa walimu
ndio
wametoka viongozi wengi wa nchi yetu wakiwemo Wabunge na
Mawaziri. Hata Rais
wetu wa kwanza Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Rais
wetu wa pili Mzee Ali Hassan Mwinyi walikuwa walimu.
Ni ukweli uliodhahiri kwamba, aina ya walimu tunaokuwa nao,
inaamua aina
ya Taifa tunalolijenga. Kwahiyo basi, kwa Serikali na jamii yote
kwa jumla, kutambua
na kuheshimu nafasi ya Mwalimu katika ujenzi na maendeleo ya
Taifa letu, ni jambo
muhimu sana.
Ahadi yangu kwenu ni kwamba tutaendelea kuutambua, kuuheshimu
na
kuuenzi mchango wa walimu kwa Taifa letu. Tunatambua kuwa wengi
wenu
mnafanya kazi katika mazingira magumu. Serikali haitachoka
kuzifanyia kazi kero za
walimu na kutafuta njia mbalimbali za kuwasaidia.
-
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Walimu;
Mimi na wenzangu Serikalini tunalipa kipaumbele cha juu suala
zima la Elimu
nchini. Mipango na malengo yetu katika Sekta ya Elimu inaongozwa
na Malengo ya
Milenia ya Elimu, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2005 na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini
Tanzania
(MKUKUTA). Nia yetu ni nini basi?
Moja, ni kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wote.
Mbili, ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa na haki katika
utoaji
elimu;
Tatu, kuona kuwa ubora wa elimu inayotolewa unaongezwa na
kuimarishwa;
Nne, kuhakikisha kuwa rasilimali tunazotenga kwa ajili ya utoaji
elimu
zinatumika kwa ufanisi na kutimiza malengo tunayoyakusudia.
Tano, tunaimarisha asasi za uongozi na uendeshaji wa Sekta ya
elimu;
Sita, tunaongeza ushirikishwaji wa Wadau mbalimbali wa
elimu,
ikiwemo sekta binafsi katika upangaji sera na mipango ya
elimu;
Ndugu zangu, kwa bahati nzuri, haya vilevile ndiyo malengo ya
mipango
mikubwa ya elimu inayotekelezwa hivi sasa, yaani Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya
Msingi (MMEM) 2002 – 2006 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Sekondari (MMES)
2004 – 2009. Serikali inafanya kila juhudi ili kuhakikisha kuwa
mipango hii
inafanikiwa. Lakini bila ushirikiano wa walimu hatuwezi kufika
popote. Nichukue
-
fursa hii kuomba ushirikiano wa walimu wote nchini katika
utekelezaji wa MMEM na
MMES.
Kuendeleza Ubora wa Elimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Malengo ya Milenia ya Elimu kwa watoto wote wenye umri wa kwenda
shule
ifikapo mwaka 2015 yanasisitiza juu ya ubora wa Elimu itolewayo
kwa watoto wote.
Mwalimu ndiyo raslimali muhimu katika kuyafikia malengo yetu
tuliyojiwekea katika
Sekta ya Elimu likiwemo lile la ubora wa elimu. Hivyo basi,
kauli mbiu yenu ya “Kila
Mwanafunzi Anahitaji Mwalimu Bora” ni sahihi. Ni kauli muafaka
kwa kipindi hiki
tulicho nacho.
Ndugu zangu;
Kama nilivyosema hapo mwanzo, Serikali inamtambua Mwalimu na
kuthamini
sana nafasi yake katika kuchangia maendeleo ya elimu na ya nchi
kwa ujumla. Kwa
ajili hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa walimu
wanaandaliwa vizuri,
wanaendelezwa kazini, wanaandaliwa mazingira mazuri ya kufanyia
kazi na kujali
maslahi yao.
RISALA
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Ninawashukuru sana kwa risala yenu nzuri na iliyowasilishwa
vizuri. Nafurahi
kwamba risala imebainisha vyema mafanikio na matatizo
yanayowakabili walimu na
-
kutoa mapendekezo muafaka juu ya hatua za kuchukua. Vilevile
mmetaja maeneo
yanayohitaji mazungumzo na maelewano na Serikali na wadau
wengine ili tuweze
kuyafikia malengo ya kielimu tuliyojiwekea. Napenda
kuwahakikishia kuwa
tumesikia, tumeelewa na tuko tayari kufanya kila tuwezalo
kufanya yale yanayoihusu
Serikali.
Uboreshaji wa Mishahara ya Walimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Natambua haja na umuhimu wa kuboresha maslahi ya walimu, hasa
mishahara
yao. Tumeanza kuchukua hatua. Katika mwaka huu wa fedha,
tumeongeza mishahara
ya walimu, kama ilivyokuwa kwa kada mbalimbali za utumishi
wa
umma. Tutaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wa umma
pamoja na walimu
kadri uchumi wetu unavyokua na hali inavyoruhusu.
Kwa kuzingatia hilo, tarehe 18 Mei, 2006 Serikali iliunda Tume
ya Kuboresha
Mishahara ya Watumishi wa Umma pamoja na walimu. Tume ilianza
kazi rasmi tarehe
01 Julai, 2006 na kazi yake kubwa ni kufanya uchunguzi kuhusu
hali ya Mishahara ya
Watumishi wa Umma ilivyo sasa na kutoa mapendekezo ya namna ya
kuiboresha
zaidi. Tume hiyo imeshakutana na wadau mbalimbali wakiwemo
wawakilishi wa
walimu wa Shule za Msingi, Sekondari, na vyuo vya Ualimu.
Kwa upande wa Walimu, tume hiyo inapitia maeneo yafuatayo kwa
lengo la
kushauri namna ya kuboresha mishahara ya walimu:
Misingi gani itumike kupanga mishahara ya walimu;
Serikali ifanye nini kuboresha mishahara ya walimu;
-
Mwalimu wa Shule ya Msingi, Sekondari na Chuo ana majukumu
gani
anayoyafanya kuanzia asubuhi hadi jioni;
Kazi ya mwalimu inaweza kulinganishwa na ipi nyingine katika
Utumishi wa Umma na kwa nini;
Mambo gani mengine yazingatiwe katika kuboresha mshahara wa
mwalimu.
Tume hii tayari imeanza kupokea maoni na ushauri kuhusu
uboreshaji
wa mishahara ya walimu. Ni matarajio yangu kuwa muda iliyopewa
utatosha kabisha
kuwasilisha mapendekezo muafaka Serikalini. Naomba tuwe na
subira Tume imalize
kazi yake. Nawaahidi kuwa Serikali itaifanyia kazi ipasavyo
taarifa ya Tume hiyo.
Ucheleweshaji wa Mishahara ya Walimu
Mmelielezea kwa uchungu tatizo la ucheleshwaji mishahara ya
walimu.
Naelewa machungu yenu, na nawaunga mkono. Tatizo hili sasa lina
kila dalili ya kuwa
sugu na kuota mizizi lisipokomeshwa. Bila ya shaka mnakumbuka
kwamba Serikali
ilikwishatoa maelekezo kuwa ifikapo tarehe 25 kila mwezi
mishahara ya walimu iwe
imelipwa. Hata hivyo, bado maelekezo haya hayajatekelezwa kwa
ukamilifu. Sababu
mbalimbali zimekuwa zikitolewa lakini bado hazikidhi haja.
Sielewi kwa nini watu
wanajaribu kuhalalisha kutotimiza ipasavyo wajibu wao kwa jambo
linalowezekana.
Wakati mwingine maelezo yanayohalalisha kutojali na uzembe kwa
upande wa
wenzetu tuliowapa dhamana ya kushughulikia mishahara ya walimu.
Bado mimi
naamini tukijipanga vizuri na kutimiza ipasavyo wajibu wetu
tunaweza kulipa
mishahara ya walimu ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi. Ingekuwa
vyema basi Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na
-
HAZINA wakakaa pamoja na kuzungumzia vikwazo na kutafuta njia
bora zaidi ya
kulipa mishahara ya walimu kwa wakati. Katika mazungumzo hayo,
wazingatie suala
la walimu wapya na kuchelewa sana kulipwa mishahara yao.
Ningependa kupata taarifa kuwa baada ya kikao hicho kero hii
itakuwa
imepatiwa ufumbuzi wa kudumu. Usumbufu wanaopata walimu
kufuatilia stahili yao
unapunguza ari na tija yao kazini. Pia hupunguza mapenzi kwa
kazi yao. Ualimu ni
kazi ya heshima. Tusimfikishe mahali Mwalimu anakopa kila mwezi
ili aishi
wakati akingojea mshahara wake.
Upandishaji wa Madaraja kwa Walimu
Ndugu zangu,
Nimesikia pia kuhusu tatizo la ucheleweshaji wa upandishwaji wa
madaraja
kwa walimu, ambalo nalo linachukua sura ya kuwa sugu. Pia lipo
tatizo la
ucheleweshaji wa marekebisho ya mishahara baada ya kupandishwa
madaraja. Wakati
mwingine mtu anapandishwa madaraja mawili au hata zaidi wakati
ambapo hata kwa
daraja la nyuma alilopandishwa mshahara haujarekebishwa.
Kupandishwa daraja
wakati ukifika na kurekebishiwa na kurekebishiwa mshahara kwa
wakati ule ni haki ya
mtumishi. Kutofanya hivyo ni uonevu. Ni matatizo ambayo napata
ugumu
kuelewa. Isitoshe hakuna maelezo ya msingi kwa nini jatatizo
haya yasiishe. Naomba
sasa iwe ilani ya mwisho. Safari ijayo tupate taarifa ya
mabadiliko. Hatuwezi
kuzungumza jambo hilo hilo kila mwaka.
Naomba kuitumia nafasi hii kuwakumbusha wahusika kuzingatia
muongozo wa
Serikali wa mwaka 2005 kuhusu kushughulikia malalamiko ya
watumishi wa umma
kuhusu kupandishwa vyeo na kuyashughulikia mapema
iwezekanavyo.
-
Ni vyema mamlaka zinazohusika na upandishaji wa vyeo vya walimu
zikiwemo Tume
ya Utumishi wa Umma - Idara ya Huduma ya Walimu, Wizara ya Elimu
na Mafunzo
ya Ufundi na halmashauri za Wilaya na Miji kuhakikisha kuwa
zoezi la walimu wote
wenye sifa kupandishwa vyeo stahili linakamilika kabla ya
tathmini ya utendaji wa
kazi kwa njia ya uwazi (OPRAS) kuanza.
Madeni ya Walimu
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Ndugu Walimu;
Mmelielezea pia tatizo la malimbikizo ya madeni ya walimu.
Tunatambua kuwa
hili ni tatizo la siku nyingi na kuna walimu wengi ambao
hawajalipwa kwa muda
mrefu stahili zao mbalimbali hasa fedha za uhamisho, matibabu,
mapunjo ya
mishahara, gharama za masomo na posho za kikazi na likizo.
Ndugu zangu Walimu, mkakati wa kulipa madeni ya walimu tunao
na
mchakato wa kufanikisha azma hiyo unaendelea. Mpaka sasa madeni
ya walimu wa
shule za msingi yaliyowasilishwa ni kiasi cha shilingi Bilioni
9.9. Hatua za uhakiki wa
madeni hayo zinakamilishwa.
Nawasihi wale wanaofanya kazi hii waongeze kasi ili waimalize
mapema
iwezekanavyo na malipo yafanyike ndani ya kipindi hiki cha mwaka
wa fedha 2006/07.
Fedha yake ipo, kinachosubiriwa ni kupatikana kwa taarifa hizo
za uhakiki.
Kwa upande wa walimu wa Sekondari na Vyuo chini ya Wizara ya
Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, madeni yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.1
yaliwasilishwa
Serikalini. Baada ya uhakiki, madeni ya zaidi ya shilingi
milioni 855 yameonekana
-
hayana matatizo (queries) na yatalipwa wakati wowote kuanzia
sasa. HAZINA
imekwishatenga fedha hizo na nimeambiwa wako katika maandalizi
ya mwisho ya
kulipa.
Nyumba za Walimu
Ndugu Walimu,
Nalitambua vyema tatizo kubwa la upungufu wa nyumba za walimu
nchini,
hasa vijijini. Kama mlivyosema katika risala yenu, nyumba
zilizopo zinakidhi asilimia
19.4 tu ya mahitaji. Nakubaliana nanyi kwamba tatizo hili ni
mateso makubwa kwa
walimu. Lakini, napenda kuwahakikishia kuwa hili ni jambo
linalonisononesha na mie
pia. Serikali inalitambua na imeendelea kulichukulia hatua za
kukabiliana
nalo. Mikakati ya muda mfupi wa kati na mrefu ili kupunguza
makali yake imewekwa
na inaendelea kutekelezwa.
Katika utekelezaji wa MMEM, kwa mfano, jumla ya nyumba 12,590
zimejengwa
kati ya mwaka 2002 hadi 2006 katika shule za msingi. Aidha, kwa
mwaka wa fedha
2006/07 nyumba 2,000 zinatarajiwa kujengwa katika shule za
msingi. Kwa upande wa
shule za sekondari, jumla ya nyumba 908 zimejengwa katika mwaka
wa kwanza wa
utekelezaji wa Mpango wa MMES, unaoisha mwaka 2009. Kwa mwaka wa
fedha
2006/07 jumla ya nyumba 1,000 zinatarajiwa kujengwa na fedha za
ukamilishaji wa
majengo hayo tayari zimetumwa mashuleni. Aidha, kama mjuavyo,
katika Mpango wa
MMES, kwa nia hiyo hiyo ya kupunguza tatizo hilo, kila
yanapojengwa madarasa
mawili hujengwa nyumba moja ya mwalimu.
-
Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua umuhimu wa kuongeza kasi
ya ujenzi
wa nyumba za walimu. Tumedhamiria kufanya hivyo ila kasi yetu
inapunguzwa na
uwezo wetu ukilinganisha na mahitaji mengi ya nchi pamoja na
hili la nyumba za
walimu. Tunawahakikishia kuwa tutaendelea kuwekeza kwenye ujenzi
wa nyumba za
walimu. Serikali pia itaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali
wakiwemo wahisani
wa nje, , mashirika ya Serikali na yasiyo ya Kiserikali na watu
binafsi katika ujenzi wa
nyumba za walimu. Kwa ajili hiyo, kwa mfano, Shirika la
Maendeleo ya Jamii (TASAF)
limejenga nyumba za walimu 264 kati ya mwaka 2001 na 2005. Najua
wanaendelea
kufanya hivyo.
Tumeanza mazungumzo na wahisani wetu wakubwa juu ya haja ya kuwa
na
mpango maalumu wa kujenga nyumba za walimu nchini. Wazo hilo
linapokelewa
vizuri ila bado tunasubiri uamuzi wa kiutekelezaji. Kwa nafasi
hii, nawashukuru
wadau wote wanaochangia kwa hali na mali katika kupunguza tatizo
la nyumba za
walimu.
Ubora wa Elimu na Muda wa Mafunzo ya Walimu
Ndugu Walimu,
Nimefurahi sana kuona kwamba suala la utoaji wa elimu bora
shuleni na
uhusiano wake na muda wa mafunzo ya walimu na mafunzo kazini
mnalitambua na
kulipa nafasi yake stahiki. Ni jambo muhimu kwamba sote
tunashiriki kuchuna bongo
zetu na kuchangia katika jitihada za kutafuta njia ya kuboresha
elimu tunayoitoa kwa
watoto wetu. Kwa ufahamu wangu, Elimu Bora ni matokeo ya
majumuisho ya mambo
mengi, mwalimu akiwa muhimili mkuu wa ubora huo.
-
Kimsingi ufanisi kwa upande wa Elimu Bora unamtegemea
mwalimu
anayemudu maudhui ya somo, mahiri katika matumizi ya njia za
kufundisha na
kujifunzia masomo yaliyoko kwenye mtaala. Kadhalika, hutegemea
mwalimu mwenye
utambuzi wa mahitaji ya walengwa, mazingira bora ya kujifunzia
na walimu kuwa
mfano wa kuigwa.
Aidha, natambua pia kwamba mazingira bora ya kufanyia kazi kwa
walimu
yana nafasi ya aina yake katika uwezeshaji wa mwalimu kutumia
taaluma yake na
vipaji vyake alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Uzoefu ndani na nje ya nchi na utafiti wa kielimu unaonesha wazi
kuwa Ubora
wa Mwalimu hutegemea sana mafunzo endelevu baada ya kupata
Mafunzo ya Awali
(tarajali). Tunaweza kuwaweka walimu miaka 2, 3 au hata zaidi
katika mafunzo ya
ualimu, lakini kama hakuna mafunzo ya kufuatilia ni vigumu
kupata aina ya walimu
tunaowataka. Hivyo hatuna budi kuweka mkazo stahiki kwa mafunzo
kazini kwa
walimu wetu.
Ndugu Walimu, naomba tutambue pia kuwa unapokuwa na mipango ya
kuleta
mabadiliko makubwa katika elimu, aghalabu huna budi kutumia njia
mbadala na
wakati mwingine za dharura kupata mahitaji ya msingi au kutatua
matatizo muhimu.
Mpango wa muda mfupi wa kuandaa walimu ni mfano mmojawapo. Huu
ndiyo
ulikuwa msingi wa kuendesha Mafunzo ya Ualimu Ngazi ya Cheti
katika sehemu mbili
(yaani Chuoni na Shuleni) wakati wote wa utekelezaji wa MMEM.
Baada ya mahitaji ya
haraka ya walimu kupungua, hivi sasa Serikali imerudi tena
kwenye kutoa mafunzo ya
Ualimu kwa miaka miwili.
Kwa kutumia njia hii mbadala kwa mwaka mmoja tumeweza kuboresha
uwiano
wa mwalimu kwa mwanafunzi kutoka 1:56 (2004) hadi kufikia 1:52
(2006) kitaifa
-
pamoja na kwamba bado zipo tofauti baina ya mikoa na wilaya.
Kinachotakiwa sasa ni
kuendeleza mafanikio yaliyopatikana. Kazi iliyo mbele yetu ni
kuimarisha mafunzo
kwa walimu wetu hawa ili kunoa ubora wao.
Kazi hiyo tunaendelea nayo. Tumekwishatumia shilingi milioni
880.5
kugharamia walimu wa Sekondari 655 na wakufunzi 370 kujiendeleza
kwenye Vyuo
Vikuu.
Pia, nimejulishwa kuwa walimu 21,519 wa Daraja B na C
wameendelezwa
kitaaluma na walipimwa Mei, 2006. Vilevile, Walimu 26,017
wanaendelea na mafunzo
na watafanya mitihani yao ifikapo Mei, 2007. Nimeambiwa pia kuwa
Walimu 42,000 wa
daraja A wamehudhuria Mafunzo ya Ualimu kazini katika matumizi
ya njia shirikishi.
Kwa hiyo, tunaendelea kufanya juhudi. Nia yetu ni kuhakikisha
kwamba Kila
Mwanafunzi anapata Mwalimu aliye Bora, aliyeandaliwa vyema, kama
ambavyo kauli
mbiu yenu inavyosema.
Kutokana na umuhimu wa kuendeleza walimu kitaaluma na kitaalamu
natoa
wito kwa mamlaka zote zinazohusika na masuala ya walimu
kuhakikisha kuwa fedha
zote zinazotengwa kwa ajili ya mafunzo zinatumika kama
ilivyokusudiwa.
Waratibu wa Elimu ya Sekondari
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT;
Elimu ya Sekondari ni muhimu katika maendeleo ya Elimu nchini na
katika
kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tunashukuru kwamba
Elimu ya Sekondari
inapanuka kwa kasi kubwa nchini. Hii inatupa changamoto ya
kuendelea na jitihada za
-
kuiboresha. Hivyo, katika kuiboresha Elimu hiyo, tumeamua
kusogeza huduma karibu
na walimu. Utaratibu wa kuwa na Waratibu wa Elimu ya Sekondari
katika ngazi ya
wilaya ni hatua ya awali ya kufikia azma hiyo.
Vifaa vya Kufundishia na Kujifunzia
Ndugu zangu, Walimu,
Napenda sasa kuzungumzia suala la upatikanaji wa vifaa vya
kufundishia na
kujifunzia. Elimu bora na Mwalimu Bora huchangiwa sana na
upatikanaji wa nyenzo
na vifaa vya kufundishia. Vilevile, kuwa na mwanafunzi bora
kunategemea upatikanaji
wa vifaa vya kujifunzia pamoja na walimu bora na mazingira
mazuri ya shuleni na
nyumbani.
Tunatambua ukubwa wa matatizo ya upatikanaji wa vifaa vya
kufundishia na
kujifunzia hasa katika kipindi hiki ambapo shule zinaongezeka na
ubora wa elimu ni
agenda yetu muhimu. Tunaendelea na juhudi za kulikabili tatizo
hili. Tumenunua
vitabu vya kiada vya kutosha sasa na kupunguza uwiano wa
mwanafunzi kwa kitabu
kwa shule za msingi kutoka 1:20 mwaka 2000 hadi 1:3 mwaka
huu.
Tutaendelea kutoa Ruzuku ya Uendeshaji kwa shule za msingi kwa
ajili ya
ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Katika mwaka huu
wa fedha,
tumetenga jumla ya shilingi bilioni 44.8 kwa ajili ya vifaa vya
kufundishia na
kujifunzia. Hata shule za Sekondari zisizokuwa za Serikali nazo
tumeamua
kuzichangia. Tumetenga shilingi milioni 250 kwa ajili hiyo.
Serikali itaendelea
kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi
zote ili kufikia lengo la
kutoa elimu bora kwa watoto wetu.
-
TATIZO LA UKIMWI
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT,
Ndugu Walimu,
Nimefarijika sana kuona kuwa, katika risala yenu, mmeongelea
suala la
UKIMWI. UKIMWI bado ni tishio la maisha ya Watanzania wote ikiwa
ni pamoja na
walimu. Ugonjwa huu unatishia kuhatarisha na kudhoofisha juhudi
tunazozifanya za
kupunguza pengo la upungufu wa walimu. Kila mwaka, UKIMWI
unatupokonya
walimu wengi. Hatuna budi kuongeza juhudi za kupambana na
maradhi haya hatari.
Nawaomba walimu muamue kukataa kuambukizwa UKIMWI.
Ugonjwa huu unaepukika, na nitashangaa sana kama yupo mwalimu
asiyejua
njia za kuepuka UKIMWI. Ukweli ni kwamba jamii inawategemea
walimu kuwaandaa
watoto wao wajiepushe na UKIMWI. Siamini kuwa wapo walimu
wasiojua A,B,C za
kujikinga na UKIMWI: Abstain, Be faithful or Use condom. Sio
mambo mapya.
Wasiokuwa na ndoa, wasubiri; wenye ndoa, wawe waaminifu – hata
wenye wapenzi
hivyo hivyo. Na wale watakaoshindwa kabisa wahakikishe
wanapofanya tendo la ndoa
wanafanya hivyo kwa usalama na usalama huo unafahamika. Nawasihi
tuzingatie haya
kwani tatizo hili ni kubwa na linalotishia maangamizi.
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT,
Serikali inao Mpango wa Elimu ya UKIMWI katika Shule za Msingi,
Sekondari,
Vyuo na sehemu za kazi. Kupitia mpango huu, walimu hupata uelewa
wa mambo
mbalimbali kuhusu UKIMWI ikiwa ni pamoja na elimu ya matumizi ya
dawa za
-
kurefusha maisha. Ninaelewa kuwa si walimu wote wanaopata
mafunzo hayo
vyuoni. Hata hivyo, tunawategemea hao wachache kuwaelimisha
wengine
wanaporudi vituoni mwao ili nao wajumuike katika mapambano haya
ya kufa na
kupona.
Kwa kuwa Chama cha Walimu kinawakilisha walimu walio wengi,
ninashauri
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi wakae pamoja na CWT kuona
ni jinsi gani
wanaweza kushirikiana kukabiliana na janga hili.
Pengine niitumie nafasi hii kuwaarifu kuwa mke wangu, ambaye ni
Mwalimu
mwenzenu, ameamua kutumia muda wake wa kuwa likizo bila malipo
kujishughulisha
na juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana.
Nafahamu pia
kwamba anayo nia ya kutumia sehemu ya muda wake kuchangia katika
mapambano
dhidi ya maradhi haya miongoni mwa walimu wenzake. Mimi na yeye
tunatambua
kuwepo kwa wanaharakati wa mapambano haya miongoni mwenu.
Ameamua
kushirikiana nanyi, kufanya kazi nanyi. Nawaomba mumpokee,
mshirikiane naye.
Nadhani anaweza kuwa wa msaada kwa kiasi fulani.
Ndugu zangu,
Katika risala yenu mmeongelea pia masuala mengine ya maslahi na
haki zenu
kama walimu. Yale yote yahusuyo matatizo ya Mfuko wa Bima ya
Afya, Malipo ya
Pensheni, kuundwa kwa chombo cha majadiliano kati ya CWT na
Serikali, nimeyasikia,
Waziri wa Elimu ameyasikia na viongozi wa Chama cha Walimu nao
wameyasikia.
Bahati nzuri sana mnaye Waziri anayejua kwa undani kero na
matakwa ya
Walimu. Yeye ni Mwalimu mwenzenu na kwa miaka kadhaa amekuwa
mwanaharakati
mwenzenu wa kupigania haki za wafanyakazi (sijui baada ya kuwa
Waziri wa Elimu
kama bado ni mwanaharakati).
-
Mnacho Chama imara cha Walimu Tanzania, na, nawahakikishia kuwa
mnayo
Serikali inayosikia, inayosikiliza, inayojali na iliyo tayari
kuchukua hatua. Tunayo
dhamira ya dhati ya kuboresha elimu kwa kuongeza walimu,
kuboresha hali ya shule,
maslahi ya walimu, pamoja na mazingira yao ya kufanyia kazi.
Tuendelee kuzungumza
na kushauriana.
Nimefurahi kwamba mmesema kwenye risala yenu pia kuhusu
utekelezaji wa
kuundwa kwa chombo cha majadiliano kati ya Serikali na Chama cha
Walimu
Tanzania. Ni kweli Tanzania imeridhia mkataba wa Shirika la Kazi
Duniani ILO No. 98
unaohusu haki za wafanyakazi kujadiliana na waajiri kuhusu
maslahi na mazingira
bora ya kazi. Sheria ya majadiliano ya Watumishi wa Umma
ilipitishwa na Bunge
mwaka 2003 na ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali mwaka
2004.
Sheria hiyo inatumika ila haijaeleza wazi ni nani mwenye mamlaka
ya kuunda
chombo/baraza la majadiliano (joint staff council). Kufuatia
hali hiyo ziliandaliwa
kanuni ambazo zinatoa mwongozo kuhudu uundaji wa chombo cha
majadiliano, na
kanuni hizo zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali mwaka 2005.
Kwa umuhimu wa
suala hilo, naiagiza Menejimenti ya Utumishi wa Umma kukamilisha
kanuni hizo ili
zianze kutumika.
Hata hivyo mie na nyie hatuna haja ya kungoja kanuni ndio
tujadiliane masuala
ya maslahi ya Taifa letu. Tuendeleeni.
Ndugu Makamu wa Rais wa CWT, Ndugu Walimu,
-
Nimesema mengi. Naomba nimalizie kwa kuwapongeza tena walimu
wote
nchini kwa kazi nzuri mnayoifanya. Natambua mazingira magumu
mnayofanyia kazi
ila napenda kuwahakikishia dhamira yetu ya kuchukua hatua
kuyaboresha. Nawasihi
walimu wa ngazi zote nchini kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu
taaluma yenu na
kuendelea kuwa kioo cha maadili mema kwa watoto tuliowakabidhi
kufundisha na
kwa Watanzania kwa ujumla. Hatma ya taifa hili ipo mikononi mwa
Walimu.
Nawashukuru tena kwa kunikaribisha kushiriki nanyi katika kilele
cha Sherehe
za Siku ya Mwalimu Duniani kwa mwaka huu wa 2006.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!