HOTUBA YA MH. JANUARY Y MAKAMBA YA KUTANGAZA NIA YA KUOMBA
RIDHAA YA CHAMA CHA MAPINDUZI KUMTEUA KUGOMBEA URAIS KATIKA
UCHAGUZI MKUU 2015
Kama ilivyo ada, tunaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
baraka zake na kibali chake cha kutukunanisha siku hii ya leo.
Nawashukuru wote mliofika hapa na nyote mnaonisikiliza kupitia
luninga na redio. Nawashukuru pia wana-CCM na Watanzania
waliokusanyika katika mikoa mbalimbali ambao wataunganishwa nasi
moja moja wakati wa kipindi cha maswali na majibu.Nimeonelea
nitumie siku na fursa hii kuwajulisha kwamba, baada ya tafakuri ya
kina ya changamoto za sasa nchi yetu na mahitaji ya uongozi wa aina
mpya, nimeamua kuomba nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kwa ajili hiyo, keshokutwa, nitasafiri kwenda Dodoma kuchukua
fomu ya kuomba ridhaa ya wana-CCM ili niweze kuteuliwa na Chama
chetu kuwa mgombea kwa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu.Nafanya hivyo nikitambua ukubwa na utakatifu wa dhamana
ninayoiomba.
Naiomba nafasi hii nikiwa nimejiridhisha bila shaka yoyote
kwamba ninao uwezo, ukomavu, uzalendo, uadilifu, uzoefu, hekima,
busara, maarifa na ubunifu wa kuishika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Naiomba nafasi hii nikielewa kiu ya Watanzania ya kupata uongozi
mpya, wa zama za sasa, unaotoa matumiani mapya, yatakayozaa
Tanzania mpya. Naiomba nafasi hii nikiwa naelewa misingi
iliyoijenga nchi yetu misingi ya haki, umoja, amani, mshikamano na
upendo miongoni mwa Watanzania na haja ya kuilinda misingi
hiyo.Nchi yetu iko katika njia panda. Katika miaka 10 ijayo,
Tanzania inaweza kuchukua njia mojawapo kati ya hizi mbili: inaweza
kupiga hatua kubwa ya maendeleo na hali ya maisha ya wananchi wote
kuboreka.
Lakini vilevile, ipo hatari ya taifa letu kupasuka kutokana na
dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii,
kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa dola, dalili za ufa katika
Muungano, umaskini na tofauti kubwa ya kipato baina ya
wananchi.Aina ya uongozi tutakaouchagua mwaka huu ndio utaamua
mustakabali wa nchi yetu. Baada ya miaka 50 ya uongozi wa kizazi
kilichopita, sasa ni wakati wa nchi yetu kuongozwa na viongozi wa
aina mpya, wenye mtazamo mpya, fikra mpya, maarifa mapya na
majawabu mapya. Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, Nimesimama hapa
kuwahakikishia kwamba nimefanya tafakuri ya kina na za muda
mrefukuhusu mwelekeo wa nchi yetu. Na niko tayari kutengeneza na
kuongoza timu madhubuti ya Watanzania wazalendo na waadilifu
watakaounda Serikaliitakayojenga kesho njema. Nimesimama hapa
kuwakaribisha wana-CCM wenzanguna Watanzania wote kwenye kampeni
hii. Tunayo dhamira na uwezo wa kushinda na kuongoza mabadiliko
makubwa ambayo Watanzania wanayatarajia.Kwa mambo niliyoyaona na
kujifunza kuanzia kufanya kazi na Rais Kikwete Ikulu, kwenye
uongozi wa Chama, Bungeni na Serikalini, nimepata matayarisho ya
kutosha ya kuiongoza nchi yetu.
Naiomba nafasi hii nikiwa naijua vyema sana nchi yetu, nikiwa
nayajua kwa kina matatizo ya Watanzania katika kila kona ya nchi
yetu, na nikiwa nimejiridhisha kwamba ninao ubunifu na maarifa ya
kutosha ya kutafuta majawabu mapya kwa ajili ya kuinua hali za
maisha za Watanzania.
Siko mbele yenu kuwasimulia kuhusu matatizo ya nchi yetu ambayo
sote tunayajua. Niko mbele yenu kuelezea namna tukavyotatua
matatizo ya nchi yetu. Katika kuomba nafasi hii nimefikiria na
nitaelezea baadhi ya majawabu mapya ambayo yananitofuatisha mimi na
wengine wanaoomba nafasi hii.
Natambua kwamba nikiteuliwa na Chama changu, nitakabidhiwa Ilani
ya Uchaguzi itakayoelekeza mambo ya kufanywa na Serikali ijayo.
Nitainadi Ilani hiyo na kuitekeleza kwa nguvu zangu zote. Hata
hivyo, kama wasemavyo waswahili, ziada njema haigombi. Kuwepo kwa
Ilani hakuzuii kuwa na mambo ya ziada ya msingikwa ajili ya
maendeleo ya taifa letu. Kwa msingi huo, nianze kwa kusema kwamba
Serikali nitakayounda itaendeshwa na falsafa ya uwezeshaji mpana wa
wananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwa miaka mingi sasa,
Watanzania wamepewa ahadi nyingi na viongozi wa siasa. Badala ya
kuwaahidi wananchi kwamba tutawafanyia kila kitu, Serikali
nitakayoiunda itawajengea uwezo na nguvu ya maamuzi kuhusu maisha
yao. Serikali yangu itajikita katika kuwajengea nguvu ya kiuchumi
ya kuendesha maisha yao, na kuamua waishi wapi, wapeleke watoto
shule wapi, waanzishe biashara gani, wajenge nyumba za aina gani,
wakatibiwe wapi. Tutawajengea uwezo wa kuwa na sauti katika maamuzi
ya Serikali yao.Tutaondokana na dhana ya wananchi kubaki watazamaji
tu katika masuala ya nchi yao. Sitaunda Serikali ya waporaji na
wabinafsi. Nitaunda Serikali yenye utu nainayowasikiliza na
kuwajali watu. Serikali inayotimiza wajibu wake bila chembe ya
uzembe wala ulegevu. Nitaunda Serikali yenye Mawaziri wasiozidi 18
ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka kuhusu uwezo
na uadilifu wake. Serikali yetu itakuwa na vipaumbele vikubwa
vitano:
Kwanza ni kukuza kipato cha watu. Msingi wa maendeleo ya nchi
yetu sio mapato ya Serikali, bali ukubwa na uhakika wa kipato cha
Watanzania. Kama nilivyosema awali, nitataka Watanzania tuwe na
nguvu na uwezo wa kiuchumi wa kuendesha maisha yetu.Kwahiyo, kwa
wale wenye shughuli za kufanya iwe ni kilimo, uvuvi, ufugaji au
biashara tutaweka mazingira ya kisera, kisheria na kikodi ili
shughuli hizo zipanuke, zishamiri, ziwe na faida kwao na
ziwanufaishe katika maisha yao.Falsafa yetu ni kwamba mtu yoyote
anayetoa jasho kutengeneza maisha yake na ya familia yake, ni
lazima anufaike na juhudi na jasho lake. Kwa wale wasio na shughuli
za kipato, tutafanya jitihada zote ili wawe na shughuli za kiuchumi
za kufanya. Tutatengeneza fursa za kiuchumi ili mtu yoyote kama
hana shughuli ya kufanya basi awe ameamua mwenyewe. Maendeleo ya
nchi yatapatikana kwa nguvu ya uchumi ya wananchi, sio kwa hisani
ya wafadhili. Kipaumbele cha pili kitakuwa ni kupatikana kwa huduma
bora za jamii na kiuchumi. Kazi kubwa imefanywa na viongozi
waliotangulia, lakini bado Watanzania wengi wanahitaji kupata
huduma ya uhakika ya maji, afya, elimu bora, barabara za uhakika,
umeme, huduma za fedha na mawasiliano. Tutabuni mbinu mpya za
kumaliza matatizo haya. Kipaumbele cha tatu ni utawala bora, wa
haki na wa sheria. Msingi wa amani ya nchi yetu ni haki. Wananchi
wengi hawana uhakika wa kupata haki zao waendapo polisi au
mahakamani. Serikali yangu italibadilisha hili. Tutazijenga upya
taasisi ya usimamizi wa utawala na haki za watu, zikiwemo mahakama
na jeshi la polisi. Hatutakubali Mtanzania yoyote aonewe na watu au
mamlaka za umma. Lakini pia tutataka kila mtu afuate sheria za
nchi, hata ziwe ndogo kiasi gani. Tutakabiliana na tatizo la
ubadhirifu wa mali ya umma kwa nguvu zote. Nampongeza Rais
Kikwetekwa kufanya jambo la kimapinduzi la kuelekeza Ripoti za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ziwekwe
hadharani na kujadiliwa.Serikali yangu itaenda mbele zaidi na
kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG ikitolewa, viongozi ambao taasisi
zao zimekutwa na makosa wanakaa pembeni siku hiyo hiyo na hatua za
kisheria, za kipolisi, za kimahakama zinaanza siku
inayofuatia.Kipaumbele cha nne ni usimamizi wa uchumi.Serikali
yangu taimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa uchumi ikiwemo
Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato.
Nitazipa mamlaka na rasilimali-watu ili ziweze kudhibiti mfumuko wa
bei, kuporomoka kwa thamani ya shilingi, nakisi ya bajeti, kupungua
kwa hifadhi ya fedha za kigeni, kukua kwa deni la taifa na
kusimamia uwekezaji wa kimkakati wa sekta binafsi. Kama ambavyo
tuna Baraza la Usalama wa Taifa sasa, nitaunda Baraza la Uchumi la
Taifa litakalojumuisha wataalam kutoka katika taasisi za umma za
usimamizi wa uchumi, wagwiji wa uchumi kwenye nchi yetu, pamoja na
wawakilishi wa sekta binafsi. Baraza hili litakuwa na jukumu la
kuhakikisha kwamba uchumi wetu unawekewa mikakati ya muda mrefu na
wakati wote hali ya uchumi wetu inaratibiwa kwa weledi na
changamoto zinazojitokeza zinarekebishwa haraka. Kipaumbele cha
tano ni amani, umoja na usalama wa mali na maisha ya Watanzania.
Amani na umoja wa nchi yetu ni tunu na urithi tulioachiwa na
waasisi wa nchi yetu. Marais wote waliopitawamefanya kazi kubwa ya
kuzilinda tunu hizi. Serikali yangu haitakubali urithi huu upotee.
Tutafanya jitihada zote ili kujenga maridhiano mapya na upendo
miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Nitawahusisha
viongozi wa dini zote katika hili. Nitaanzisha Jukwaa la Rais na
Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jumuiya ya Wakristo Tanzania
(CCT) na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) litakalokutana kila
miezi miwili kujadili na kupanga mikakati ya kuendeleza amani,
umoja, upendo na maadili ya jamii. Pia tutachukua hatua mpya za
kuimarisha Muungano wetu na kuupatia uhalali mpya na wa ziada
miongoni mwa Watanzania. Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba sasa nifafanue majawabu mapya ambayo Serikali yangu
itayatekeleza kwa changamoto mahsusi:
Naomba nianze na suala la ajira. Kwasasa, wapo zaidi ya
Watanzania milioni 23 kwenye soko la ajira leo hii. Kila mwaka
wanaongezeka vijana zaidi ya laki tisakwenye soko la ajira. Hawa ni
watu wengi sana. Viongozi wengi wa siasa wameliita tatizo la ajira
kuwa ni bomu. Lakini kulielezea tatizo sio kulitatua. Serikali
yangu itafanya nini?
Watanzania wengi wanajishughulisha na biashara ndogo na za kati.
Karibu zotezinaajiri mtu mmoja au wawilina nyingi
zinasuasua.Watalaamu wanatuambia, asilimia 20 tu ya biashara na
kampuni ndogo nchini zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa mwaka, ajira
400,000 za kudumu zitazalishwa kwa mwaka. Je asilimia 80 za
biashara hizi zikiongeza watu wawili wawili tu kwa mwaka? Tutakuwa
tumepunguza sana kama sio kumaliza tatizo la ajira.Kwahiyo, jawabu
letu la kwanza litakuwa ni maendeleo ya biashara ndogo na za kati.
Zilizopo zifanye vizuri na kuongeza waajiriwa na wale wanaotaka
kuanzisha biashara, iwe rahisi kufanya hivyo. Ziko namna kadhaa za
kufanya hivi. Kwa mfano, katika nchi yetu, Serikali bado ndio
mnunuzi mkuu. KIla siku, Serikali yetu inanunua bidhaa nyingi -
kuanzia kuni, karatasi, matofali, mabati, vyakula na huduma
nyingine nyingi. Katika kuzijengea uwezo kampuni ndogo na za kati,
Serikali yangu itaweka Sheria ya kuwezesha asilimia 30 ya thamani
ya manunuzi ya umma kupewa makampuni madogo na ya kati
yatakayokidhi vigezo rahisi yanayomilikiwa na vijana na wanawake.
Jambo hili litawezesha biashara nyingi ndogo kujenga uwezo,
kupanuka na kuajiri watu wengi zaidi.Lakini, ili hili litokee,
lazima tuwe na taasisi madhubuti ambayo itashughulika na ustawi wa
biashara na makampuni madogo na ya kati. Kwahiyo, nitaanzisha
Mamlaka mahsusi ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati. Pamoja
na mambo mengine, Mamlaka hii itapewa majukumu ya kuwezesha,
kurahisisha na kusimamia biashara ndogo kuanzishwa kwa urahisi,
kuendeshwa bila bughudha, na kupata fursa ya kukua.Ndugu
Wananchi,
Viwanda bado ni tegemeo kubwa la ajira. Kwa viwanda vikubwa
vilivyopo sasa, tutaweka motisha ya kikodi kwa yoyote ambaye
ataweza kuongeza ajira mpya angalau500 au zaidi za kudumu kwa
mwaka. Haipaswi kumgharimu kikodi mtu mwenye biashara kuongeza
wafanyakazi. Kwa waajiri ambao nibiashara au kampuni mpya ndogo na
za kati, yaani SMEs, Serikali yangu itatoa motisha ya kupunguziwa
kodi hizi kwa kila kazi mpya tano au zaidi kwa mwaka. Ukweli hapa
ni kwamba kunawiri kwa uchumi hakutokani na kodi inayokusanywa na
Serikali bali kunatokana na kipato na uwezo wa manunuzi walionao
wananchi na kipato cha wafanyabiashara kuweza kukuza biashara zao
na kutoa ajira nyingi zaidi.
Vilevile, katika kukabiliana na tatizo hili la ajira,tutawezesha
sekta binafsi kujenga na kufufua viwanda vya nguo, katani na
korosho nchini. Huko nyuma tulishawahi kuwa na viwanda vingi vya
aina hii, vikichangia asilimia 25 ya pato la Taifa na kuajiri
asilimia 25 ya wafanyakazi wote nchini. Kwa sasa, ni asilimia 30 tu
ya pamba yetu ndio inayotumika nchini. Pamba tunayo ya kutosha
kukidhi mahitaji ya viwanda vikubwa zaidi ya hamsini. Ndani ya
miaka mitano ijayo tutahakikisha tunajenga na kufufua viwanda 11
vya nguo vitakavyotoa ajira mpya zaidi 100,000 viwandani tu, huku
asilimia zaidi ya 80 ya wafanyakazi hawa wakiwa ni wanawake. Lengo
ni sekta nzima ya pamba kuajiri walau asilimia 10 ya nguvu kazi
(kazi milioni 2.5). Katika kuwezesha hili, Serikali nitakayoiongoza
itachukua hatua za muda mfupi za kikodi na kiushuru ili kuwezesha
viwanda hivi kukabiliana na ushindani wa kanga, vitenge, mitumba na
vitambaa kutoka nje ya nchi.
Ndugu wananchi,
Shughuli za ujenzi wa nyumba na miundombinu huongeza chachu
katika uchumi na kuongeza ajira nyingi sana. Tuna mahitaji makubwa
ya nyumba na tuna mahitaji makubwa ya ajira. Nitahakikisha
tunatengeneza mazingira mazuri ya uanzishwaji na uimarishaji wa
makampuni madogo na ya kati yanayojihusisha na biashara katika
sekta ya nyumba. Tutahakikisha kwamba, ndani ya miaka kumi ya
uongozi wangu, sekta ya ujenzi inachangia zaidi ya asilimia 25 ya
Pato la Taifa na kuajiri zaidi za watanzania milioni 5. Hii
itawezekana kwa kupunguza gharama za ujenzi. Na hili litawezekana
kwa uwekezaji kwenye viwanda vya vifaa ya ujenzi, kama vile viwanda
vya nondo, mabati, simenti, vigae na vioo.Hii itaenda pamoja
naujenzi wa miundombinu mikubwa, hasa ya usafirishaji. Tutaweka
jitihada za makusudi kuongeza kasi na ukubwa wa miradi ya
miundombinu nchini ambayo itaajiri watanzania wengi zaidi na
kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye mzunguko wa uchumi.
Tutahakikisha kwamba wakandarasiwa miradi hii ni makampuni ya ndani
yatakayohifadhi na kuwekeza fedha hizo hapa ndani. Lengo langu ni
kuwezesha wakandarasi wa ndani kiufundi, kiutawala na kifedha na
kuwawezesha kupata walau asilimia 80 ya miradi yote ya miundombinu
inayojengwa kwa fedha za umma ndani ya miaka kumi ijayo.
Shughuli za sanaa na michezo zikisimamiwa vizuri zina uwezo wa
kuajiri asilimia kubwa ya watanzania. Mapema kabisa kwenye serikali
yetu tutarasimisha shughuli za sanaa ikiwemo sinema, muziki na kazi
zote za ubunifu. Tutatunga Sheria kali zaidi kulinda hakimiliki.
Kupitia Mfuko wa Sanaa wa Taifa tutakaouunda upya, tutatoaruzuku na
mikopo ya masharti nafuu kwa wazalishaji, waendeshaji na wasanii
wenyewe kwenye kuendeleza ubunifu na kuzalisha, kutangaza na kuuza
kazi mpya kwa njia za kisasa. Tukiweza kuongeza maradufu uwekezaji
kwenye tasnia ya sanaa na ubunifu hapa nchini, tutatengeneza ajira
mpya zaidi ya milioni mbili. Sita, kwa vijana wasomi na wanataaluma
ambao hawatakuwa wamebahatika kupata ajira katika sekta rasmi,
tutawawekea utaratibu wajiunge na kuanzisha makampuni na biashara
za kitaaluma wahandisi, wanasheria, wasomi katika fani za siasa na
utawala, na wengineo na tutawapa mikopo maalum ya kufanya
hivyo.
Kwa upande wa wamachinga, naelewa kwamba wanazunguka kutwa nzima
wakiuza bidhaa ambazo hawazimiliki na huishia kupata pesa ya kula
tu au nauli au hawapati kitu kabisa. Viongozi nitakaowateua
kuongoza Mamlaka mpya ya Biashara Ndogo na Za Kati katika mwaka wao
wa kwanza watapimwa kwa uwezo wao wa kuhakikisha wamachinga wana
sehemu salama na zenye wateja za kufanyia shughuli zao na hawaishii
kuwa fremu tu barabarani kwa mali za watu wengine. Jambo jingine
kubwa tutakalofanya ni kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji
hapa nchini katika miaka mitano kwa ajili ya wanavijiji kukopeshana
kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Mfuko huu utaendeshwa na
Kamati maalum zitakazoundwa na wanavijiji wenyewe na wao ndio
watakaomua nani akopeshwe na arudishe baada ya muda gani. Mzunguko
wa shilingi milioni 50 kwenye shughuli za uzalishaji mali kijijini
utatoa chachu ya maendeleo ya watu. Fedha zinazohitajika hazifiki
bilioni 700 katika miaka mitano. Kwa sasa tunakusanya zaidi ya
bilioni 800 kwa mwezi. Fedha hizi tutazipata na nitaelezea ni.
Utaratibu wa aina hii umebadilisha maisha ya wananchi wa vijijini
huko nchini Thailand.
Kilimo bado ndio nguzo ya ajira kwa Watanzania wengi. Mambo
mengi yamezungumzwa kuhusu mapinduzi ya kilimokwa miaka mingi. Kila
zao linalolimwa nchini iwe ni pamba, korosho, chai, kahawa,
tumbaku, mkonge, au mboga na matunda lina changamoto zake mahsusi.
Serikali yangu itabadilisha namna ya kushughulikia maendeleo ya
kilimo kwa kuweka mkakati ya zao moja moja tofauti na ilivyo sasa
ambapo kuna mikakati ya jumla ya kilimo. Tutabadilisha utaratibu wa
sasa wa upatikanaji wa pembejeo ambapo pesa nyingi zinapotea kwa
watu wa kati huku wakulima wakiwa hawapati pembejeo za kutosha, kwa
wakati na kwa bei wanayoimudu. Tutaweka mkazo kwenye kurekebisha
mfumo wa ununuzi wa mazao ambao kwasasa unamkandamiza mkulima.
Tutaanzisha Soko Kuu la Kitaifa la Mazao, yaani Commodities
Exchange, litakalowezesha wakulima kuwa na nguvu ya kujua na kuamua
bei na wakati wa kuuza mazao yao.Kwenye uvuvi na ufugaji, mipango
iliyopo inatosheleza. Tutakachokifanya na kuitekeleza kwa haraka na
uhakika. Kwa maeneo ya uvuvi, tutaanzisha mifuko ya kuwawezesha
wavuvi kukopeshwa nyavu, boti na mashine na majokofu ili waweze
kwenda mbali majini na kuhifadhi samaki kwa muda mrefu ili wapate
soko zuri na bei nzuri. Hatutaacha wafugaji wakose malisho ya
mifugo yao. Kila mfugaji atamilikishwa eneo ya malisho na kupewa
hati. Hii itasaidia kumaliza migogoro kati yao na wakulima.Ndugu
wananchi,
Jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala la elimu.
Ni lazima kukiri kwamba, pamoja na changamoto zilizopo, mafanikio
makubwa yamepatikana kwenye Serikali ya Rais Kikwete kwenye nyanja
ya elimu, hasa kwenye udahili wa wanafunzi kwa ngazi zote. Pamoja
na mafanikio haya, changamoto za elimu zipo lukuki na ndugu zangu
Watanzania mnazijua. Sasa nini kifanyike kuboresha elimu? Katika
serikali yetu, tutatekeleza yafuatayo.
Kwanza, Serikali yangu itaondoa shaka na kumaliza kabisa mjadala
kuhusu dira ya elimu yetu. Tutaongozwa na dira ya elimu
inayochochea vijana kujiajiri, inayochochea udadisi, inayochochea
ubunifu, inayochochea uthubutu, nidhamu, weledi na uzalendo.
Tutatengeneza mitaala mipya na thabiti kabisa inayokidhi mahitaji
ya mazingira na changamoto za sasa na mahitaji ya uchumi wa kisasa,
mahitaji ya jamii na mahitaji ya taifa kwa ujumla. Hiyo ndio
itakuwa mihimili ya elimu tutakayowafundisha watoto wetu chini ya
uongozi wangu.
Tutawafundisha watoto wetu kwa lugha zote mbili, ya Kiswahili na
Kiingereza kwasababu ni jambo linalowezekana. Rais Kikwete amefanya
kazi kubwa katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu. Bado
changamoto ipo kwenye walimu wa sayansi na hisabati. Tutaongeza
udahili kwenye vyuo vya ualimu vinavyofundisha masomo hayoili
kupata walimu wengi zaidi.
Kama saikolojia ya mwalimu haijakaa sawa kutokana na changamoto
nyingi, tusahau kuhusu ubora wa elimu. Tunasema ualimu ni wito
lakini haipaswi kuwa adhabu. Tutazitatua changamoto za walimu,
ikiwemo mazingira yao ya kazi, motisha na hamasa yao ya kufundisha
ikiwemo mishahara yao, kupandishwa madaraja, mafunzo yao ya ziada
ya kujiendeleza.
Tutaweka vipimo vipya ya maendeleo ya elimu nchini kwa kupima
uelewa na maarifa ya wanafunzi kwa mambo wanayopaswa kuyajua katika
ngazi husika ya elimu. Hatutaishia tu kusheherekea ufaulu wa jumla
katika mitihani ya mwisho. Pia, tutaweka mfumo wa motisha ya malipo
au kupandishwa vyeo kwa walimu wetu wa shule za Serikali wanaofanya
vizuri
Vilevile, hatutaingiza siasa kwenye maendeleo ya elimu. Tutaweka
uongozi thabiti na wa kizalendo kwenye sekta ya elimu
utakaokabiliana na changamoto za uendeshaji na utawala wa sekta ya
elimu, ikiwemo masuala ya ukaguzi, usimamizi wa walimu,
uidhinishaji na usambazaji vitabu kwenye mashule, upelekaji na
matumizi ya fedha za uendeshaji wa shule na mambo mengineyo.Ili
kuchukua vijana wengi wanaoishia darasa la saba na kidato cha nne,
tutajenga Chuo kikubwa cha ufundi kwenye kila Wilaya ya nchi yetu
kwa kushirikiana na sekta binafsi.Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa
elimu ya juu, Serikali yangu itabadilisha utaratibu na kuweka
utaratibu mpya, wa wazi na wa haki ili kila anayestahili mkopo
apate na apate kwa kiwango kinachotosheleza. Tutaanzisha Mfuko
Maalum, yaani National Education Endowment Fund, kwa ajili ya
kugharamia elimu ya juu kwa wenye mahitaji maalum. Serikali pia
itaweka dhamana ya mikopo wanafunzi katika taasisi binafsi
zitakazokuwa tayari kukopesha wanafunzi. Zaidi ya hapo, tutaanza
utaratibu wa kuviwezesha vyuo na taasisi za elimu ya juu viwe na
mifuko kwa ajili ya kutoa mikopo na misaada kwa wanafunzi. Jambo
jingine kubwa ambalo ningependa kulizungumzia ni tatizo la rushwa.
Limezungumzwa na wengi. Lakini kulizungumzia na kulipigia kelele
suala la rushwa pekee hakulimalizi. Ziko namna mbili
tutakazozitumia kukabiliana na hili tatizo: njia ya kwanza ni
kisheria, kimfumo na kitaasisi; njia ya pili ni kijamii.Kuhusu
kimfumo, nitafanya mabadiliko makubwa mawili. Kwanza, ni kuiwezesha
TAKUKURU kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashitaki watuhumiwa wa
rushwa moja kwa moja mahakamani. Pia, tuanzishe Mahakama Maalum ya
Uhujumu Uchumi ambayo itahusika na makosa ya rushwa; ubadhirifu wa
mali ya umma; ukwepaji kodi; kuiba, kunufaika au kutaka kuiba au
kutaka kunufaika na mali ya umma; na makosa mengine ya aina hii.
Mahakama ambayo itakuwa na jopo maalum la majaji ambalo litafanya
kazi mwaka mzima na kusikiliza na kuhukumu kesi hizi haraka. Kesi
za uhujumu uchumi ziendeshwe wazi na mfululizo na adhabu ziwe kali
sana, kwa mfano ya kifungo cha maisha. Pia tutaanzisha Kurugenzi ya
Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu Uchumi. Tutaiwezesha Mahakama hii
na Kurugenzi hii bila ukomo wa kirasilimali kuifanya kazi hii
vizuri.
Kuhusu kijamii, kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wengine
wa kijamii, nitaanzisha na kuwezesha mjadala mpana kwenye jamii
yetu kuhusu maadili ya jamii. Jamii yetu ijengwe kwenye misingi ya
kuchukia rushwa, ulaghai na njia za mkato za kupata mali. Inapofika
mahala jamii inasheherekea mali ambazo hazina maelezo, inapofika
mahali ambapo jamii inawatukuza wachache ambao wametumia ujanja
kufanikiwa, inapofika mahala ambapo jamii inakuita mjinga
unapostaafu ukiwa hujilimbikizia mali, hapo lipo tatizo ndani ya
jamii. Lazima kujenga jamii tofauti, ambayo wala rushwa wanajiona
kama wanatembea uchi, jamii ambayo inatoa adhabu za kijamii, yaani
social sanctions, ikiwemo kutengwa, ambazo ni kali kuliko adhabu za
kisheria. Mwalimu Nyerere alijaribu kujenga jamii ya aina hii:
jamii ambayo kiongozi wa umma hapaswi kungoja mahakama itamke
kwamba ni mla rushwa. Tunapaswa kuendelea kujenga jamii ya aina
hii. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa. Maadili na malezi na
makuzi kwenye familia pia yana nafasi yake.
Ndugu zangu Watanzania, bila kudhibiti rushwa na wizi hatuwezi
kupata maendeleo. Kwa hiyo, kwa kiongozi yoyote, kama anataka
kuacha rekodi nzuri ya maendeleo, kuitokomeza rushwa ni jambo la
kufa na kupona.
Katika uchaguzi huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya kumaliza
tatizo hili. Rekodi ya uadilifu sio sifa pekee ya uongozi. Lakini
pia sio jambo la kupuuzwa hata kidogo. Namna viongozi wanavyotafuta
uongozi ndio namna watakavyotawala. Tunayo fursa ya kuchagua
viongozi ambao hawatapata kigugumizi kupambana na rushwa. Tunayo
fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatakuwa na madeni ya kulipa.
Sina shaka kabisa kwambamimi ni kiongozi wa aina hiyo.
Ndugu wananchi,
Napenda pia kuzungumzia suala la ardhi. Hili pia ni muhimu
kwasababu mbili: kwanza, ardhi, kwa maana ya umiliki na matumizi
yake, ndio msingi wa yote; na pili, zimeanza kuonekana dalili ya
watu wachache kuhodhi ardhi kubwa na kuanza kuirudisha nchi yetu
kwenye zama za ukabaila. Hakuna maendeleo ya kilimo kama hakuna
uhakika wa matumizi bora ya ardhi na kama hakuna uhakika wa mfumo
wa umiliki wa ardhi. Lazima sasa kuondoa migogoro ya ardhi
isiyoisha kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na Serikali na
kuipa ardhi thamani halisi inayostahili. Kama tunavyobainisha
kisheria na kulinda hifadhi za misitu na mbuga za wanyama lazima
maeneo ya kilimo na mifugo na makazi ya watu nayo yawe hivyo.
Lazima wakulima wamiliki ardhi yao kisheria. Lazima kutenga maeneo
maalumu ya wafugaji yanayomilikiwa na wafugaji kisheria na bila
kusahau korido mahususi za kupitisha mifugo kutoka upande mmoja wa
nchi mpaka mwingine. Serikali yetu itatumia teknolojia mpya ya
satellite katika kupima na kupanga matumizi ya ardhi nchini.
Tutajenga kituo cha kupokea picha za satellite ambacho kitawezesha
kila kipande cha ardhi katika nchi yetu kupimwa, na hati ya
umiliki, yenye picha na mipaka isiyo na shaka, kutolewa na matumizi
ya ardhi hiyokujulikana.Kituo hiki hakigharimu fedha ambazo
tunazishindwa.Kuhusu huduma ya afya, Watanzania wengi, hasa wa
vijijini, bado wana changamoto kubwa kuipata. Kazi nzuri imefanywa
na Serikali ya Rais Kikwete kusogeza huduma hii karibu na wananchi
na kuiboresha. Kazi hiyo tutaiendeleza. Tutaitazama huduma ya afya
kimfumo zaidi na kurekebisha uendeshaji wake.Lakini kubwa
tutakalofanya ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania ana bima ya afya
na anapata matibabu bila kujali uwezo wa kipato chake. Moja ya
namna ya kufanya hili ni kutengeneza Sheria mpya ya kuiunganisha
mifuko yote ya Bima na kurahisisha ukusanyaji na matumizi ya pesa
kwenye vituo vya afya ya msingi. Nchi nyingine za Afrika wamefanya
hivi na kufanikiwa. Na sisi hatuwezi kushindwa. Tutaondoa
ukiritimba na urasimu wa Bohari ya Madawa ya Taifa katika kusambaza
madawa katika vituo vya huduma vya Serikali. Kwa wananchi wa
Tanzania, ukiwauliza leo ni huduma ipi ya jamii bado ni kero kubwa.
Jibu litakuwa ni huduma ya maji. Watanzania wanaopata huduma hii
hawafiki asilimia 60. Maeneo ya vijijini hali ni mbaya zaidi. Ni
jambo la kawaida kwa kina mama vijijini kutumia siku nzima na
kwenda umbali mrefu kupata nusu ndoo kwa familia nzima. Tatizo
kubwa ni uwekezaji mdogo katika sekta ya maji. Ili kukabiliana na
tatizo hili, tutaanzisha Mfuko wa Maji Vijijini pamoja na Wakala wa
Maji Vijijini. Tumeona jinsi Mfuko wa Barabara na Wakala wa
Barabara wa Taifa unavyofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa barabara.
Tumeona jinsi ambavyo Mfuko wa Umeme Vijijini na Wakala wa Umeme
Vijijini ulivyofanya kazi nzuri kusambaza umeme vijijini. Tumeweza
kufanya kazi nzuri ya barabara na umeme kwa kutumia fedha zetu
wenyewe.Utaratibu mpya na msukumo mpya wa kupeleka maji vijijini
utasaidia. Chanzo cha fedha kwa Mfuko wa Maji kinaweza kuwa tozo
maalum ndogo kwenye matumizi ya maji mijini na maji ya kunywa
kwenye chupa. Nina uhakika kabisa kuwa ndani ya miaka kumi tunaweza
kusogeza maji safi, salama na ya uhakika karibu kabisa na kaya zote
nchini kote. Nataka sasa niongelee kuhusu miundombinu. Suala hili
lazima tulipe umuhimu wa kipekee. Uchumi wa nchi unaendeshwa na
miundombinu ya usafirishaji. Rais Kikwete amefanya kazi kubwa, hasa
kwenye miundombinu ya barabara. Na naamini kwamba kabla hajamaliza
muda wake ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kati. Kazi
hii nzuri tutaiendeleza lakini tutaifanya kwa kazi zaidi na maarifa
mapya. Barabara ambazo hazijaisha tutazimalizia na tutaanza
nyingine mpya. Tutahusisha sekta binafsi katika ujenzi wa reli za
kutoka Mtwara hadi Mchuchuma hadi Mbamba Bay. Pia tutafufua reli ya
Tanga hadi Arusha na kuisogeza hadi Musoma.Bandari ya Mtwara
itakuwa bandari kubwa ya uchumi wa gesi na chuma kutoka Liganga na
makaa ya m awe kutoka Mchuchuma.Nimebahatika kufika kwenye bandari
za Kemondo Bay, Mwanza, Nansio na Musoma kwenye Ziwa Victoria;
bandari za Kigoma na Kasanga kwenye Ziwa Tanganyika; na bandari za
Itungi, Manda, Liuli na Mbamba Bay kwenye Ziwa Nyasa. Hizo zote ni
bandari za uchumi na zinahitaji matengenezo mapya makubwa. Kazi hii
tutaifanya. Bandari ya Mwambani ambayo imeahidiwa kwa miaka mingi
nayo tutaanza kuijenga kwa kushirikisha sekta binafsi. Ndugu
wananchi,
Nimezungumzia mambo mengi na mabadiliko makubwa ambayo
tutayatekeleza. Ni dhahiri kwamba baadhi ya haya mambo yatahitaji
rasilimali-fedha za Serikali kuyafanya. Kwa hakika hatuwezi kufanya
mambo yote haya bila uwezo wa Serikali kuongezeka na uchumi
kupanuka.Kiongozi makini hawezi kuzungumzia mambo yote haya bila
kuzungumzia rasilimali za kuyatekeleza.Tofauti na wenzangu, nataka
niwahakikishie kwamba ninazo fikra za namna ya kupata fedha za
kufanya yote niliyoyazungumzia.Kwanza, tutaihusisha sekta binafsi
kwa kina zaidi kutekeleza ile miradi ambayo ni ya kimaendeleo
lakini pia ni ya kibiashara ambapo Serikali haina ulazima kutumia
fedha zake.
Kwa upande wa uwezo wa Serikali, nimefanya utafiti wa kina
kupitia taarifa za Serikali, ripoti za Bunge na sekta binafsi
kuhusu kuongeza uwezo wa Serikali kutimiza majukumu
niliyoyaainisha. Serikali nitakayounda itafanya yafuatayo:(napenda
kwa wale wenye calculator kwenye simu zao tupige hesabu kwa pamoja
hapa)Kwanza, bila kusita wala kuchelewa, nitapunguza misamaha ya
kodi na kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa. Hatua hii
itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni 780kwa
mwaka.
Ili kuwaingiza walipa kodi wengi wapya, hasa kutoka sekta isiyo
rasmi, Serikali yangu itapunguza kiwango cha mapato kwa mwaka kwa
walipa kodi wadogo wanaolipa kodi kwa mtindo wa ukadiriaji. Hakuna
mfanyabiashara atakayetozwa kodi kabla hajatengeneza faida. Lakini
pia tutaweka adhabu kubwakwa wataoshindwa kulipa kodi.
Tutakamilisha vitambulisho vya taifana anuani za makazi ili kuweza
kuwatambua watu wote wanaofanya biashara na kuwatoza kodi. Hatua
hizi itawezesha Serikali kupata fedha za ziada zaidi ya shilingi
bilioni 860kwa mwaka.Tutaongeza ufanisi wa Mamlaka ya Kodi
Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za Kamati ya Spika Kuhusu Mapato na
Matumizi Serikalini, TRA ikiongeza ufanisi kwa asilimia 10 tu,
Serikali itapata mapato ya ziada ya shilingi bilioni 620 kwa mwaka.
Kazi hiyo tutaifanya kwani sio ngumu. Na fedha hizo tutazipata.
Tutakapokamilisha mradi mkubwa wa kufua chuma wa Liganga,
ifikapo mwaka 2020, Serikali itapata mapato ya shilingi bilioni
960. Tutakapokamilisha mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma, Serikali
itaweza kupata zaidi ya shilingi bilioni 800.
Tutahakikisha kwamba ardhi yote inapimwa na kila mwenye ardhi
anayo hati na anatozwa kodi stahiki. Hatua hii itaiwezesha Serikali
kupata zaidi ya shilingi bilioni 520.
Tukiwekeza kiasi kidogo cha fedha kwenye sekta ya nyuki na
kudhibiti uvunaji na biashara haramu ya rasilimali za misitu,
tutaweza kupata fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni 130.Meli
nyingi za kigeni zinavua samaki katika eneo letu bila kutozwa
mrahaba, wala kukaguliwa, wala kutozwa faini. Tutarekebisha Sheria
ya Uvuvi wa Bahari Kuu na kuimarisha Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu
ili kuwezesha haya kufanyika. Hatua hii itaipatia Serikali mapato
ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 350.
Tutadhibiti biashara ya madini ya vito na kuiwezesha Mamlaka ya
Mapato Tanzania kufanya kazi kwa pamoja na urahisi na Mamlaka ya
Ukaguzi wa Madini ili kuhakiki taarifa za mapato ya madini. Hatua
hii itaiongezea Serikali mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi
bilioni 520.
Tutadhibiti uvujaji wa mapato yanayokusanywa katika ngazi za
Halmashauri. Hatua hii itaweza kutupatia kipato cha zaidi ya
shilingi bilioni 200 kwa mwaka.
Sekta ya utalii kwa sasa inatuingizia shilingi karibu trilioni 3
kwa mwaka. Kwa mujibu wa taarifa ya kina ya Benki ya Dunia, ndani
ya miaka kumi, sekta hii inaweza kuingiza shilingi trilioni 30 kwa
mwaka. Ili tuzipate fedha hizo tunapaswa kufanya mambo manne yaliyo
ndani ya uwezo wetu. Kwanza, kufungua, kuwekeza na kutangaza ukanda
wa utalii wa kusini mwa Tanzania; pili, kuongeza aina na idadi ya
watalii wanaotembelea Tanzania na kuainisha vivutio vipya na
mbadala na kuvitangaza. Tatu, kudhibiti mfumo wa kukusanya mapato
ya utalii, ambayo mengi yanapotelea kwa wajanja wachache nchi au
yanalipwa nje ya nchi kwa makampuni ya kitalii ya nje. Mambo haya
tunayaweza, na tutayafanya ili tufikie lengo la mapato ya shilingi
trilioni 30 kwa mwaka ili tuweze kufanya kazi kubwa tulizozianisha.
Pia, serikali ina mali na hisa kwenye biashara mbalimbali ambazo
thamani yake ni zaidi ya shilingi trilioni 10. Tutaweka utaratibu
mzuri zaidi kwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye ofisi ya Msajili
wa Hazina ili tunufaike na mali na hisa hizi. Pia, ndani ya miaka
mitano, kwa hatua mbalimbali, tutayaingiza makampuni makuu manne ya
Serikali kwenye masoko ya hisa Shirika la Nyumba la Taifa, Shirika
la Petroli Tanzania, Shirika la Reli la Taifa, Kampuni ya Simu ya
Taifa na Shirika la Bandari Tanzania. Hatua hii itawezesha
Watanzania kumiliki sehemu muhimu ya uchumi wa nchi lakini pia
kupatikana mapato.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naweza kuendelea kuelezea ni kwa namna gani Serikali
nitakayoiongoza itaweza kuongeza uwezo wake wa kutimiza majukumu
niliyoyaainisha.Hapa bado sijagusia hatua za kubana matumizi ya
Serikali ambazo pia fikra zake tunazo. Tofauti na baadhi ya
wenzangu waliotangulia kuzungumza, sijazungumzia mapato ya gesi kwa
makusudi kwasababu ukweli ni kwamba Rais wa awamu ijayo, hata akiwa
madarakani kwa miaka kumi, bado nchi yetu itakuwa haijaanza kupata
fedha kutokana na gesi. Hata hivyo, ni muhimu kuendelea na
maandalizi ya nchi yetu kunufaika na uchumi wa gesi. Na pia,
tofauti na wenzangu, sijazungumzia kukopa au misaada ya wahisani
kwa ajili ya maendeleo yetu. Ukweli ni kwamba tunao uwezo wa
kufanya mambo yetu kwa kujitegemea huku tukidhibiti deni letu la
taifa. Ninachoweza kusema tu ni kwamba mambo haya nimeyafikiria kwa
kina. Katika kutafakari ni kwa namna gani tutabadilisha hali za
maisha ya watu wetu, sikukurupuka.
Inawezekana mambo niliyoyazungumza kwamba tutayafanya
yakaonekana kuwa ni mengi na ni mzigo. Lakini waswahili wanasema
tembo hashindwi na mkonga wake. Kama nilivyoonyesha, tunao uwezo
kabisa wa kuyafanya. Katika nchi yetu yenye mahitaji mengi, hatuna
anasa ya kuchagua kipi kiwe kwanza. Tunao wajibu kama viongozi wa
ubunifu wa kufanya mambo yote ya msingi kwa wakati mmoja. Tunazo
rasilimali na uwezo wa kuendeleza elimu na kilimo kwa wakati mmoja,
tuna uwezo wa kumaliza matatizo ya madawati nchini, matatizo ya
madawa katika hospitali zetu, matatizo ya mikopo kwa wanafunzi,
matatizo ya maji, matatizo ya mishahara ya marupurupu ya
wafanyakazi na mambo mengi ambayo Watanzania wanayatarajia kutoka
katika Serikali yao.
Haya yote yatawezakana iwapo tutafumua na kusuka upya mfumo wa
utumishi na utendaji wa Serikali ili kukomesha urasimu uliokithiri
Serikalini, ili kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma,
ili kuongeza uwezekano na uharaka wa uwajibishaji wa watumishi wa
umma wanaokiuka maadili ya kazi zao lakini pia ili kurudisha ari,
morali na fahari na heshima kwa watumishi wa umma.
Lakini napenda nirudie, pamoja na yote haya, tiba ya uhakika ni
kuutengeneza uchumi wetu ukue kwa namna ambayo inawajumuisha
Watanzania wa hali zote. Tiba ya uhakikani kwa Watanzania kuumiliki
uchumi wao na kuwa na nguvu ya kiuchumi ya kujiamulia hatma ya
maisha yao. Serikali nitakayoiongoza italisimamia hili. Tiba kubwa
ni nidhamu ya kazi na uwajibikaji wa kila mmoja wetu. Nasimama
mbele yenu nikiwa na bahati kubwa ya kupata malezi ya siasa na
uongozi kwa viongozi waliotangulia wa nchi yetu. Rais Mstaafu
Benjamin William Mkapa aliyefahamu uwezo wangu na kunisaidia kupata
elimu yangu ya Chuo Kuu na kuniwezesha kupata kazi Wizara ya Mambo
ya Nje. Na, Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyeniona nikiwa naye
Wizara ya Mambo ya Nje na kuniteua niwe Msaidizi wake kwenye
kampeni za Urais mwaka 2005, ambapo nilizunguka naye nchi nzima
tukizungumzia kero za Watanzania, na baadaye kuniteua kuwa Msaidizi
wake Ikulu, ambapo nilipata fursa ya kuona na kujua nchi
inaendeshwa vipi, kushiriki katika mikutano yake yote na viongozi
wengine duniani na kuona diplomasia ya kimataifa inaendeshwa vipi,
na kushiriki katika vikao vya Baraza la Mawaziri na kujua maamuzi
makubwa ya nchi yanafanywa vipi.
Namshukuru pia Rais Kikwete kwa kunipa fursa ya kuwa kiongozi
katika Chama chetu. Kwa kuwa Mjumbe wa Sektretarieti ya Chama,
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
ya CCM, nimeshiriki kwenye uendeshaji wa shughuli za kila siku za
Chama chetu na nimekijua vizuri Chama. Nimejua uimara na udhaifu
wake. Na nimeyajua yanayopaswa kufanywa ili kiendelee kuaminiwa na
Watanzania.
Nawashukuru wananchi wa Bumbuli kwa kuniamini niwe Mbunge wao.
Nawashukuru wa kunifanya nionekane na kuendelea kunipenda. Bado
nina deni kubwa kwao kwa imani hiyo.
Napenda nifikie mwisho kwa kusema kwamba ninayo dhamira, uwezo,
maarifa na ubunifu wa kuiongoza nchi yetu kukabiliana na changamoto
mpya, za kizazi cha sasa, changamoto zinazohitaji maarifa
mapya.
Naishukuru sana familia yangu, ikiwemo wazazi na ndugu na jamaa.
Lakini zaidi mke wangu, ambaye tumekuwa wote sasa kwa miaka zaidi
ya kumi, na watoto wetu wawili kwa upendo na uvumilivu.
Lakini kazi ya kuijenga nchi sio kazi ya mtu mmoja. Kiongozi
yoyote anayesema yeye ndio Masia na amekuja kama mkombozi wa taifa,
atakuwa anawalaghai. Mafanikio yangu katika nafasi hii ninayoiomba
na katika kutimiza majukumu yangu yanategemea ushiriki na
ushirikiano wenu. Nachukua nafasi hii kuwaalika katika harakati
hizi. Sigombei nafasi hii kupambana na mtu. Nagombea kupambana na
changamoto za watu. Nikifanikiwa, nitasikiliza mawazo mazuri kutoka
kwa kila mtu, hata ambao sio wana-CCM. Nitakuwa kiongozi wa watu
wote bila kujali dini zao, makabila yao, rangi zao, vyama vyao au
kanda wanazotoka. Nitaongoza kwa namna ambayo Watanzania
watajisikia fahari kuongozwa nami. Sijawa kwenye siasa kwa miaka 30
au 40 kama baadhi ya wagombea, ambao wamepata fursa nyingi na
madaraka makubwa ya kutekeleza yale wanayoyaahidi leo. Lakini
nimekuwepo kwenye uongozi kiasi cha kutosha cha kujua matatizo yako
wapi, nini cha kufanya,na namna ya kufanya, kama ambavyo nimeelezea
kwa kirefu mchana huu. Mkinipa nafasi hamtakuwa mnatumaini tu,
balimtakuwa mnaonyesha dhamira ya kutaka hakika ya mabadiliko
makubwa.
Nafarijika kwamba kwenye Chama chetu wamejitokeza wagombea
wengi. Hili ni jambo jema sana kwani kunaonesha ukomavu wa
kidemokrasia. Lakini ni muhimu sote tukaelewa kwamba kugombea sio
kugombana. Binafsi ndivyo ninavyoelewa na ndio maana sikutumia muda
wenu kumshambulia mtu kwasababu jambo hili halisaidii Watanzania.
Nina imani kubwa kwamba, kwa ukomavu wa Chama chetu, tutabaki
wamoja na imara mara baada ya mchakato huu. Chama chetu kina
dhamana kubwa na kina historia adhimu barani Afrika. Dunia nzima
inatazama mchakato huu wa ndani ya Chama chetu. Matumaini ya
marafiki zetu na matumaini ya wanachama wetu ni kwamba tutachagua
mgombea wetu kwa msingi wa kujiamini na sio kwa msingi wa woga wa
kusambaratika. Mkinichagua mimi kupeperusha bendera ya chama,
nitatumia nguvu zangu zote na utajiri mkubwa wa hekima ndani ya
chama chetu kuvunja makundi yote yaliyojitokeza kipindi hiki cha
uchaguzi na kuwaunganisha wana-CCM wote. Mwenyekiti wetu, Makamu
Wenyeviti na Katibu Mkuu na Sekretarieti yakewamefanya kazi nzuri
ya kukiimarisha Chama chetu na kukijengea uwezo. Nitakapokuwa
kiongozi wa Chama chetu nitaanzia walipoishia. Nimekuwa chipukizi
wa Chama hiki. Nimekuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama hiki.
Na nimefikia hadi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama chetu.
Nafahamu changamoto za watendaji wa Chama na Jumuiya mikoani na
wilayani. Wanafanya kazi kubwa. Nitawatazama. Nafahamu Wenyeviti
wetu wa Mikoa na Wilaya, wana mahitaji mahsusi ya kufanya kazi zao
za uongozi wa Chama chetu na usimamizi wa Ilani yetu katika ngazi
zao. Nayajua hayo mahitaji. Naelewa majukumu mapya ya Wajumbe wa
NEC yanahitaji uwezeshaji. Tutayazungumza na kuyafanya. Nafahamu
Makatibu wa Siasa na Uenezi na Makatibu wa Uchumi na Fedha wa Mikoa
na Wilaya wanafanya kazi kubwa na wanastahili kutambuliwa. Chama
chetu kitakuwa salama chini ya uongozi wangu.Tutaendelea na kazi
nzuri inayofanywa sasa na viongozi wetu ya kukiimarisha Chama chetu
ili kiendelee kuwa tumaini la Watanzania.Nimalizie kwa kurudia
kwamba sigombei nafasi hii kupambana na mtu bali kupambana na
matatizo ya watu. Nataka kushirikiana nanyi wote tuijenge Tanzania
Mpya. Nataka uongozi wangu uwe mwanzo wa Tanzania Mpya, ya miaka 50
ijayo. Tunataka tujenge taifa la Watanzania ambao kila mmoja ana
fursa, uwezo na nguvu ya kiuchumi ya kupata mahitaji yake na
kuendesha maisha yake. Tunataka kujenga taifa ambalo wananchi
hawabebi mzigo wa maisha unawaelemea. Tunataka kujenga taifa la
watu wenye sauti na kauli juu ya Serikali yao. Haya mambo sio
ndoto. Yanawezekana kabisa. Viongozi huwekwa na Mungu. Ninapoomba
uongozi huu, namuomba Mungu anipe fursa ya kuwaongoza watu wake
kupitia ridhaa yao. Kama mgombea, namuomba Mungu anipe uwezo,
hekima na busara ya kupokea matakwa yake katika mchakato huu. Na
kama kiongozi, namuomba anipe hekima ya kuwaongoza watu wake na
kushughulikia mashauri yao kwa haki na ukweli. Na kubwa zaidi,
namuomba Mungu aendelee kuibariki nchi yetunawatu wake.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.1